Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Yanga haina damu, hewa na chakula

12860 Pic+yanga TanzaniaWeb

Mon, 20 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tazama na hata zikawepo klabu za Simba na Yanga, nazo zikadumu kwa zaidi ya miaka 50 na zikawa zinakimbilia muongo mmoja wa maisha. Akatokea mtoto mmoja wa maajabu aitwaye Azam, akajaribu kuwapiku na maisha yake yakarejea katika “jalala la mazoea” ambalo halijawahi kuondoka kwenye mboni na akili zetu.

Na hata ilipokuwepo kasi ya Singida United kutaka kufanya mapinduzi ya kisoka, wakaisahau tabia njema nao wakafanya dhambi ya kuhusiana na Yanga na hata haikueleweka ni wapi wamepata akili ya kuleta utani kwenye usajili katika kipindi tulichotegemea watakuwa imara kujidhatiti. Ikawa usiku na ikawa asubuhi, Fei Toto aliyekuwa Singida United akatolewa msaada Yanga.

Naam, sio dhambi itakayowatafuna Singida United na Yanga peke yake bali itakuwa dhambi inayoendelea kutafuna soka la Tanzania na ambayo itatupeleka kuzimu kwenye adhabu ya milele ya kutokufanikiwa kwenye maisha ya soka wakati Sudan Kusini wakipanda taratibu na baadae watakuwa visiki tusivyoweza kuving’oa ili tufanikiwe.

Ni yupi aliyesema Tanzania hatukutakiwa kufanya vizuri katika soka tangu miaka hamsini iliyopita ambapo babu zetu walifanikiwa kwenda kwenye hatua ya mataifa ya Afrika? Yupi aliyeshindwa kuwa na aibu na kuhakikisha kuwa tunafanya vyema kwa maana ya vilabu vyetu kuweza kufika mbali katika hatua za klabu bingwa barani Afrika na Shirikisho?

Taifa lenye walau watu milioni 55 kwa sasa lilitakiwa kuwa kwenye misingi inayoeleweka. Unatamani “fly over” za TAZARA zingekuja wakati ambao Yanga na Simba tayari zina viwanja. Sahau kuhusu maandiko yote niliyoandika hapo juu kwenye kukufikirisha kiimani lakini dhambi inayonyanyasa roho yangu ni hii aliyokuwepo Yanga sasa hivi.

Yanga ni moja ya timu zilizofanya vibaya zaidi kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho kwa sasa. Wachezaji hawana motisha, viongozi hawaelewi kipi kinaanza na kipi kinamalizikia na mashabiki hawafahamu chanzo cha matatizo ni kipi. Kwa kifupi hakuna mwenye majibu ya maswali mengi ambayo yapo kwenye vinywa vya kila mmoja.

Angalia mduara huu. Wachezaji wana swali kwa uongozi, uongozi una swali kwa mashabiki, mashabiki wana swali kwa uongozi, kisha uongozi unahoji wachezaji na baadaye wachezaji wanahoji washabiki. Imekuwa sayansi ya mzunguko ambayo kila kimoja kinahusiana na kingine katika kushindwa kutekeleza yanayohitajika.

Lakini unamweka wapi shabiki ambaye hajatengenezewa msingi mzuri wa kuhudumia klabu yake? Unamlaumu vipi Mhilu ambaye ndo kwanza amepewa majukumu ya kuhakikisha anaifumua Gor Mahia wakati akiwa anasikia taarifa za nahodha wake Kelvin Yondani kuwa aligoma ili aongezewe mshahara?

Lakini tatizo kubwa lingine ni kuwa unamkata kichwa kiongozi yupi ambaye ameshindwa kutekeleza majukumu yake wakati mashabiki bado wanaamini kuwa mwokozi ni Yusuph Manji pekee?

Katika dunia ya kisasa, unaweza kusema Yanga ipo katika kitengo cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu. Hawana hewa, hawana damu, na hawana chakula kwenye mwili wao. Kwa mahitaji yao, uwezo wa hospitali inayoweza kuwahudumia ni ngumu kuipata na itachukua muda kama watataka kupata suluhu ya yote haya kwa wakati mmoja.

Hakuna mahala Yanga inaweza kupata damu ya kutosha yaani fedha ya kuwatosha kujisimamia kama wanaamini kuwa washabiki wanaweza kuwa wanachanga kupitia njia za simu kisha walipie viingilio uwanjani.

Hakuna namna Yanga inaweza kupata hewa ya kuwapa uhai kwa maana ya uongozi kama hawawezi kuacha jinamizi la Yusuph Manji liondoke.

Na sioni njia yoyote ambayo Yanga inaweza kufanya vyema kimataifa na kitaifa iwapo wachezaji watakosa motisha na ukaribu ambacho ndio chakula cha msingi.

Yanayowakuta Yanga leo, yanaweza kuikuta timu yoyote kwa Tanzania. Hizi klabu zetu zimeundwa kwa porojo na sio misingi inayoweza kusimamia taasisi. Klabu hizi zimeundwa katika misingi ya Gozi la Ng’ombe, kwamba ni ukurasa ambao iwapo nitaondoka leo basi Mwananchi watapata tabu kuweka mrithi na badala yake walete kitu kipya kabisa.

Walitakiwa wawe kama gazeti la Mwananchi, kwa maana ya kwamba Gozi La Ng’ombe ni mojawapo ya kurasa zinazoliunda na hata nikiondoka, uzito wa gazeti hautopungua wala kubadilika na badala yake kutakuwa na msingi mpya wa kurithi ukurasa wangu na maisha yakasonga mbele.

Tofauti ya Simba na Yanga mpaka sasa ni kuwa huku yupo Mo Dewji na huku Manji kapumzika. Iwapo Simba hawatofanikisha taratibu zao, hakuna namna wanaweza kuwa na utofauti na Yanga kwa miaka mitano inayofuata.

Taasisi zinaongozwa na mifumo inayosimamiwa na watu lakini klabu zetu zinatengenezwa na watu wanaosimamiwa na mifumo. Vitu viwili tofauti kabisa na vinavyofanyika kinyume na inavyopasa kuwa.

Hii ndio sababu kubwa vilabu hivi havina uwanja wa mazoezi achilia mbali uwanja wa matumizi ya mechi rasmi. Haviwezi kufanua hivyo kwa sababu Manji aliahidi kuleta wahandisi kutoka China ili wajenge uwanja na sio mwenyekiti aliahidi Yanga italeta wahandisi.

Hizi klabu ni majina ambayo unaweza kuyafanyia biashara kuanzia ngazi ya matawi mpaka wachezaji na vyenyewe visinufaike bali watu husika.

Paul Pogba sio mkubwa kuliko Manchester United, Mohamed Salah sio mkubwa kuliko Liverpool, Cristiano Ronaldo hakuwahi kuikaribia thamani Real Madrid, Lionel Messi anaweza kuondoka Barcelona na maisha yakaendelea.

Haya ndo manufaa yanayotokana na kuwepo kwa mifumo inayosimamiwa na watu lakini wamepita Marais kadhaa Simba na maisha yao hayajawahi kuendelea bila Emmanuel Okwi.

Ni aibu inayoumiza nafsi na roho lakini ndio ukweli tulioamua kuishi nao kinafki kuwa vilabu hivi haviwezi kuishi kisasa. Yanga inafanya vibaya na haiwezi kujitutumua mbele ya Gor Mahia? Inaonekana ni Aston Villa inacheza na Lipuli na wachezaji unaona maumbo yao yanasema “Acha tukubali yaishe.” Inasikitisha kuona Yanga haina hewa, damu na chakula mwilini mwake.

Huu ni uchafu ambao ulitakiwa uwepo kipindi kile ambacho Azam haionyeshi michezo yao hivyo ilikuwa ngumu kwa babu yangu mzee Mallan Agwanda aliyepo Shirati Rorya kuiona. Lakini leo hii ambayo huwezi kumdanganya jezi mpya za Yanga zinafananaje, Yanga yenyewe inaishi kwa dhiki? Aibu kupita kiasi.

Columnist: mwananchi.co.tz