Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Yakizingatiwa haya, shule za serikali zitaepuka kupata matokeo yanayoaibisha

8971 Shule+pic TZW

Tue, 12 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ule usemi maarufu kwamba, “Elimu ni ufunguo wa maisha” sasa unapoteza thamani yake licha ya kuwa bado unabeba ukweli huo. Thamani yake inapotea kutokana na kuporomoka kwa ubora wa elimu nchini hasa kwenye shule za umma.

Wazazi wenye vipato vikubwa au vya kati wanawapeleka watoto wao kwenye shule binafsi, wakiamini kwamba huko watapata elimu bora ambayo itakayowasaidia kufungua njia katika maisha yao ya baadaye.

Ubora wa elimu wa shule za binafsi unajidhihirisha kwenye uelewa wa mtoto anayesoma huko ikilinganishwa na yule anayesoma shule za umma.

Pia, shule za binafsi zinashika nafasi za juu hasa zile za kumi bora kitaifa.

Shule zote zilizoingia kumi bora kwenye matokeo ya kidato cha nne mwaka 2017, zilikuwa za binafsi. Shule hizo ni St. Francis Girls, Feza Boys, Kemebos, Bethel Saabs Girls, Anuarite, Marian Gilrs, Canossa, Feza Girls, Marian Boys na Shamsiye Boys.

Wakati huohuo, shule kumi zilizofanya vibaya kwenye matokeo hayo ni za umma. Shule hizo ni Kusini, Pwani Mchangani, Mwenge, Langoni, Furaha, Mbesa, Kabugaro, Chokocho, Nyeburu na Mtule.

Miaka ya nyuma ilikuwa ni fahari kwa mwanafunzi kusoma shule za umma na ilikuwa ni kipimo cha ufaulu wake.

Wanafunzi waliosoma shule binafsi walikuwa ni wale waliofeli mitihani ya darasa la sasa na kukosa nafasi kwenye shule za umma, hivyo walilazimika kwenda shule binafsi.

Kwa sasa, wazazi hawataki watoto wao wasome shule za umma kwa sababu elimu imeporomoka na wanaamini kwamba, elimu bora inapatikana shule binafsi ambazo zinashika nafasi ya juu ya ubora kuanzia miaka ya 2000.

Hata shule za vipaji maalumu nazo zimepoteza umaarufu wake. Nyingi zinakabiliwa na uhaba wa walimu, kukosekana kwa vitabu na vifaa vya maabara vya kutosha, miundombinu mibovu na usimamizi duni.

Baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi za umma wamebainika kufaulu mitihani yao ya darasa la saba na kuingia kidato cha kwanza licha ya kuwa hawawezi kusoma na kuandika. Hiyo ni aibu kwa Taifa kwa sababu ya uzembe wa baadhi ya watendaji wa serikali.

Machi 18 wakati wa hafla ya kumuaga Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Profesa Idris Kikula, Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa alisema anapokea na kusoma malalamiko mengi kuhusu janga la elimu nchini na akapendekeza kuwepo kwa mjadala wa kitaifa kuhusu elimu ili kulinusuru Taifa.

“Kwanini ukisoma katika orodha ya shule zetu za sekondari kwenye ufaulu wao katika 10 za kwanza ukiangalia unaweza kuwa na uhakika kuwa nane si za serikali ni za watu binafsi. Kama serikali ndiyo mhimili mkuu wa elimu, kuna kasoro gani?” alihoji.

Kiongozi huyo mstaafu aliungwa mkono na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete ambaye alisema Afrika inaweza kupiga hatua zaidi katika kuendeleza elimu, lakini inahitaji kuongeza juhudi kutoka elimu ya msingi hadi sekondari.

INAENDELEA UK 14

INATOKA UK 13

“Kwa kuangalia takwimu, Afrika ni bara la elimu ya msingi,” alisema Kikwete kwenye kongamano lililoandaliwa na Taasisi ya Masomo ya Afrika ya Chuo Kikuu cha Harvard nchini Marekani.

Malalamiko hayo siyo ya viongozi hao pekee, bali hata walimu na wananchi wengine wanalalamika kutokuwa na vitabu vya kutosheleza mahitaji ya wanafunzi huku wakibainisha kwamba darasa la nne hawana vitabu vya kiada.

“Hatuna kabisa vitabu vya wanafunzi wa darasa la nne kwenye shule yetu, tunasikia wameanza kugawa baadhi ya maeneo, lakini kwetu bado hatujavipata,” anasema mwalimu mmoja wa shule ya msingi ambaye hakutaka kutaja jina lake.

Wadau wa elimu wameunga mkono hoja ya kuwa na mjadala wa kitaifa kuhusu elimu hapa nchini na msingi wa mjadala huo uwekwe kwenye lugha ya kufundishia kuanzia elimu ya msingi hadi sekondari.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Leonard Akwilapo amekiri kwamba kuna uhaba wa vitabu kwa shule za msingi nchi nzima, na kwamba , tayari vitabu vya darasa la kwanza hadi la nne vinachapishwa na vingine vimesambazwa shuleni.

Kuhusu kukosekana kwa vitabu kwa darasa la nne, Dk Akwilapo amesema hoja hiyo haina mashiko huku akihoji kama hakuna vitabu, miaka miwili iliyopita wanafunzi walikuwa wanasomaje.

“Kwani kama mtalaa umebadilishwa, mwalimu hawezi kufundisha? Kama hamna vitabu, miaka miwili iliyopita wanafunzi wa darasa la nne walisomaje,” anasema Dk Akwilapo.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Watoaji wa Elimu Wasiotegemea Serikali Kusini mwa Jangwa la Sahara (CIEPSSA), Benjamin Nkonya anasema suala la ubora wa elimu nchini ni pana na linahitaji mjadala kama alivyopendekeza Rais Mkapa.

Ili kuboresha elimu nchini, Nkonya anapendekeza bodi za shule zipewe nguvu ya kufukuza walimu ambao wanashindwa kutimiza wajibu wao. Anasema wakurugenzi wa halmashauri wamekuwa mbali na usimamizi wa shule hizo, hivyo bodi za shule zipewe mamlaka ya kusimamia shule zao.

“Kila mwaka tunaona bajeti ya elimu ikiongezeka, hiyo siyo hoja kwa sasa. Tujadili namna ya kuongeza usimamizi wa shule, wapo walimu hawafundishi kabisa lakini wanapata mshahara kila mwezi na hakuna anayehoji,” anasema Nkonya.

Nkonya ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi nchini (Tamongsco), anapendekeza kuwapo kwa utawala wa sheria katika suala la elimu hasa katika kuchagua walimu wenye sifa na vigezo vya kufanya kazi hiyo.

Anafafanua kwamba jambo jingine la muhimu ni kutenganisha siasa na elimu kwa sababu suala la elimu ni maisha ya watu. Anasema elimu ijengewe misingi ambayo itasaidia kuimarisha ubora wake kwa muda mrefu.

“Profesa Ndalichako (Joyce) awe mkali kama alivyokuwa kwenye Baraza la Mitihani (Necta). Usimamizi wa shule uwe mkali na wakaguzi watimize wajibu wao ipasavyo,” anasema kiongozi huyo.

Akiwasilisha maoni ya kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii kuhusu bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya mwaka 2018/19, mjumbe wa kamati hiyo, Hussein Bashe alisema kazi kubwa ya kufanya ni kutatua changamoto za ubora wa elimu.

“Kamati inaona ni muda muafaka wa kuwekeza katika ubora wa elimu na si bora elimu kwa kuwapo kwa walimu na mitalaa bora,” alisema Bashe katika mkutano wa Bunge la Bajeti unaofanyika jijini Dodoma.

Bashe alisema utafiti uliofanywa na Taasisi ya HakiElimu mwaka juzi, unaonyesha asilimia 37.8 ya walimu ndiyo wenye hamasa ya kufundisha shule za Serikali.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Thomas Mwita anasema shule za umma zinafanya vibaya kwa sababu mazingira ya kujifunzia bado siyo mazuri ukilinganisha na zile za binafsi ambazo zimeandaliwa vizuri.

Anasema wanafunzi wa umma wanatumia muda mrefu kwenda shule wakati wenzao wametengenezewa mazingira mazuri ya usafiri au mabweni ili wawe salama dhidi ya matukio ya unyanyasaji yanayotokea.

“Shule za binafsi zinafanya vizuri kwa sababu uwekezaji wa kutosha umefanyika kumwezesha mwanafunzi kusoma. Shule za umma ziko nyuma kwa sababu mazingira yake ya kujifunzia siyo mazuri na uangalizi wake siyo mzuri,” anasema.

Mwanazuoni huyo anabainisha kwamba mjadala wa kitaifa uanzie kwenye lugha ya kufundishia ambayo ndiyo kikwazo kwa shule za umma. Anasema lugha ya Kiingereza ina vitabu vingi na inamuunganisha mwanafunzi na ulimwengu mwingine ambao unatumia lugha hiyo.

Mwalimu wa shule ya moja iliyopo wilayani Mbozi, Wedingtone Adimeli anasema tangu sera ya elimu bure ilipoanza kutekelezwa kumekuwa na changamoto ya miundombinu hasa vyumba vya madarasa kutokana na wingi wa wanafunzi wanaoandikishwa.

Anasema wingi huo wa wanafunzi unawafanya wasielewe kwa haraka na walimu wanashindwa kuwasimamia kwa karibu zaidi. Anasema ili kuboresha elimu lazima changamoto hiyo itatuliwe na uwiano wa mwalimu na wanafunzi uzingatiwe.

Columnist: mwananchi.co.tz