Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Yafahamu makundi manne ya watumishi hatari uwapo kazini

59400 Pic+kazini

Fri, 24 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Maisha yetu ya kazi, kwa kiasi kikubwa, yanategemea namna tunavyowafahamu watu tunaofanya nao kazi. Hii ni pamoja na kuelewa tabia zao, hulka zao na misukumo iliyo nyuma ya yale wanayoyafanya.

Uwezo wa kuwafahamu watu unaofanya nao kazi utakusaidia kujua namna gani utaweza kushirikiana nao na tahadhari unazoweza kuzichukua katika utekelezaji wa majukumu yako.

Katika makala yaliyopita tuliona makundi sita ya wafanyakazi. Tuliwaona watu wanaopenda ukamilifu uliovuka mipaka. Tatizo la hawa huwezi kuwaridhisha.

Unachotakiwa kufanya ukiwa nao ofisini ni kuhakikisha unatimiza kile unachoweza. Kundi la pili ni waasi wanaopenda umaarufu wa kuwa kinyume na watu. Huhitaji kuwa karibu nao na ukiweza jiepushe nao isipokuwa kwa mambo ya lazima.

Pia wapo wahanga. Hawa wanafanya kazi kwa bidii lakini hawajiamini. Tambua kazi zao na pale unapoweza watie moyo. Kundi la nne ni wale wachangamfu wanaopenda kuonekana na watu. Hawa tulisema usiwape nafasi ya kuwaeleza mambo yako muhimu.

Kundi la tano tuliwaita waota ndoto. Hawa wanaongea wasichokiishi. Usiwaamini sana unapofanya nao kazi. Kundi la sita ni wafanyakazi wanaopenda kuweka mbele raha kuliko majukumu.

Pia Soma

Weka mipaka unapofanya nao kazi. Leo tunaendelea na makundi mengine manne.

Wema wanaodeka

Hawa wanapenda kuwa karibu sana na watu wenye uwezo na ujuzi unaowanufaisha. Wanapoona una kipaji fulani wanachokihitaji au uko kwenye nafasi fulani inayoweza kuwapendelea watakuganda.

Wana ujuzi mkubwa wa kutumia watu bila malipo na usijue kwa nini unatumia muda mwingi kufanya kazi zao. Kila wanayemganda, lazima wahakikishe kuna namna wananufaika na ujirani wanaoutengeneza.

Mara nyingi watu wa namna hii walilelewa kwenye mazingira ya kudekezwa kwa maana ya kutokufundishwa uwajibikaji wakiwa watoto.

Kulithibitisha hili, wanyime kile wanachotarajia kwako, utaona walivyo wepesi kukasirika na kuzira bila sababu. Hilo lisikushughulishe kwani ni wajibu wako kuwasaidia kutekeleza majukumu waliyonayo kama wakifanyacho hakihitaji uwajibikaji wa pamoja.

Hata kwenye Uhusiano wa familia, hawa ni watu wanaojifikiria wenyewe na kuweka mbele mahitaji yao bila kujali wengine wanahitaji nini kutoka kwao.

Jiwekee mipaka unapofanya nao kazi. Usijitese kuwaridhisha kwa sababu usipokuwa makini utajikuta majukumu yao yanageuka kuwa majukumu yako yasiyo rasmi.

Wavivu wachapakazi

Hawa ni watu wanaoonekana kuwa wema kupindukia. Utawapenda kwa sababu wanajali hisia zako na wasingependa kumwuudhi mtu. Utawaomba wakusaidie kazi, hawawezi kusema hapana hata kama wanajua hawana nafasi. Tatizo linakuja pale wanaposhindwa kutimiza kile walichoahidi kukifanya.

Mwanzoni wanaonekana wako na wewe lakini baadae unaanza kujihisi wanakuhujumu. Ingawa kwa nje wanaonekana ni wema, wema huo hautokani na utashi wa dhati bali namna fulani ya kuficha mapungufu yao. Wanaficha uvivu wao kwa kutaka waonekana wanapenda kujituma. Hii ndio sababu wanakubali kila wanachoambiwa hata kama wanajua hawawezi. Mwisho wa siku wanaishia kukukatisha tamaa.

Chukua tahadhari unapofanya kazi za maana na watu hawa. Kuwa na mpango mbadala mnapokubaliana jambo kwa sababu mara nyingi hawa hutumia muda mwingi kufikiria visingizio kuliko kufanya kile wanachotakiwa kukifanya. Wapunguzie majukumu usiyopenda yaharibike.

Wakombozi wanyanyasaji

Ukikutana na wafanyakazi wa kundi hili lazima ujione una bahati. Wanajua kukuokoa unapokuwa kwenye matatizo. Hawa wakijua unahitaji kujifunza kitu fulani, ni wepesi kukupa msaada unaouhitaji. Watatumia muda na raslimali zao kuhakikisha kinachokusumbua kinapata ufumbuzi.

Tatizo lao ni kwamba wakishakusaidia hawasahau. Siku zote watataka uwaabudu kama namna ya kukumbuka fadhila walizokutendea. Hawa ndio wale watu wasioona aibu kukumbusha walivyokusaidia. Wanajua kukudhalilisha usipoonekana kujali walichowahi kukutendea.

Mara nyingi wanakuwa wamelelewa na watu wasiojali. Wanafidia kile walichokikosa kwa kuwajali wengine. Bahati mbaya ni kwamba wanapokusaidia nyuma yake kunakuwa na agenda ya siri. Wanatumia msaada wao kama mtego wa kukudhibiti. Wanajua wakishakusaidia utawarudishia hisani muda muafaka utakapofika.

Usiruhusu msaada wanaokupa uwe deni litakalokutesa baadae. Kubali msaada wao bila kuwapa haki ya kukudhibiti au kukunyanyasa baadae.

Waadilifu wapiga majungu

Hawa ni aina ya watu wanaopenda kuonekana hawavumilii vitendo visivyo vya kimaadili. Kama huwafahamu utaamini ni watakatifu wanaostahili tuzo ya kulinda maadili ofisini.

Mazungumzo yao yanahusu mapungufu ya watu wengine. Ukikaa nao hutakosa kipya kinachohusu namna wafanyakazi wenzenu wasivyopenda kazi, namna watu wanavyopiga dili, roho mbaya za mabosi, nani anatoka na nani na tabia nyingine zisizofaa.

Hawapendi kuona watu wengine wakifurahia maisha yao na kupata mafanikio. Wamejaa wivu na tabia ya kushindana na hivyo faraja yao ni kukosoa, kuhukumu, kubeza, kudhalilisha na hata kuumiza wengine.

Ukiwafahamu vizuri, hata hivyo, unagundua kuwa hata wao wenyewe hawaishi hayo wanayoyasema. Wepesi wao wa kuona mapungufu ya watu ni kwa sababu na wao ndivyo walivyo.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Mawasiliano 0754870815, twitter: @bwaya

Columnist: mwananchi.co.tz