Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ya Costech na vuguvugu la Uchaguzi Mkuu 2020

11872 Costech+pic.png TanzaniaWeb

Sat, 21 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ukusanyaji wa maoni ya wananchi unaweza kuwa ni uwanja mpya wa mapambano ikiwa nchi inaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kama ilivyodhihirika katika mvutano mdogo uliosababishwa na utafiti uliofanywa na taasisi ya Twaweza hivi karibuni.

Kivumbi bado kinaendelea kutimka juu ya matokeo ya utafiti huo ambayo, pamoja na mambo mengine, yameonyesha kushuka kwa umaarufu wa Rais John Maguful, ukilinganisha kiwango cha awali na marais waliomtangulia.

Wiki iliyopita, Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) iliibua gumzo, kwa kukusudia kuwawajibisha wakusanyaji wa maoni ya wananchi kwa kile ilicho dai ni kufanya hivyo bila ya kufuata taratibu zilizoainishwa kisheria.

Barua chanzo cha yote

Katika barua ambayo imesambaa mitandaoni na Costech kukiri kuiandika, Tume hiyo inaitaka Twaweza ijieleze kwa nini isichukuliwe hatua za kisheria kwa kukusanya maoni ya wananchi bila kuwa na kibali.

Wananchi na wadau wengine hata hivyo walizidi kuchanganyikiwa baada ya Kaimu mkurugenzi mkuu wa Costech, Dk Amos Nungu kutokubali kueleza katika mkutano wake na waandishi wa habari, ni chini ya kifungu gani cha sheria Tume ilikusudia kuiadhibu Twaweza.

Wakati Dk Nungu akikiri kwamba ni kweli waliiandikia Twaweza, anawashtua waandishi waliokuwapo katika mkutano huo baada ya kukataa kuelezea kwa kina uamuzi huo wa Tume kuikabili Twaweza baada ya kuchapisha utafiti wake kuhusu maoni ya wananchi kuhusu siasa nchini.

Kukataa huko kwa Costech kueleza kinagaubaga msingi wa kisheria wa hatua yake wa kuiandikia Twaweza, kuibua ubashiri mwingi kutoka kwa wananchi na wadau mbalimbali nchini.

Maoni ya wadau

Baadhi ya wabobezi wa mambo katika masuala ya siasa, wanaharakati na utafiti wameonya dhidi ya kustawi kwa taharuki na mvutano dhidi ya maoni ya wananchi.

Maria Sarungi-Tsehai, mkurugenzi wa kampeni ya Badili Tanzania, anadhani kwamba sakata kati ya Costech na Twaweza lina msukumo wa kisiasa na kwamba hiyo ni dalili kwamba suala la ukusanyaji wa maoni ya wananchi linaweza kuwa la kiutatanishi huko mbeleni.

“Twaweza wameendelea kutoa tafiti zao kuhusu maoni ya wananchi katika mada mbalimbali. Ukweli ni kwamba mwaka jana utafiti huohuo wa maoni ya wananchi kuhusu ukubalikaji wa viongozi akiwemo Rais ulichapishwa na kutangazwa na hatukuona swali lolote kutoka kwa Costech,” alisema akikataa kuwa huenda ni suala la kikanuni.

Nick Kasera Oyoo, ni mshauri wa masuala ya utafiti na mawasiliano wa taasisi ya kitafiti ya Midas Touché East Africa, anasema kuwa wakusanyaji wa maoni ya wananchi, kama Twaweza, ni wadau wakubwa wa maendeleo na kwamba zoezi hilo halifanywi wakiwa na “matokeo mfukoni.”

“Hatufanyi (tafiti) kwa lengo la kubomoa, bali kujenga,” aliongeza. “Lakini kama (Costech) watataka (tuwaombe kibali kufanya hizo tafiti) wanapaswa wapitie mchakato wa kisheria kulifanya hilo agizo liwe la kisheria.”

Kuna jipya Twaweza?

Hii si mara ya kwanza kwa Twaweza kutoa matokeo ya maoni ya wananchi ambayo wao huyaita ‘Sauti za Wananchi.’ Kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, shirika hilo lilitoa matokeo ya utafiti ambao ulimwonyesha mgombea wa urais kwa tiketi ya CCM, John Magufuli kuwa mbele ya mpinzani wake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa.

Twaweza pia wametoa matokeo ya tafiti kama hizo kadhaa chini ya uongozi wa awamu ya tano – na hakuna ulioibua mzozo kama huu uliochapishwa hivi karibuni.

Au ni tafsiri za kisheria?

Fatma Karume, Rais wa Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS), anasema Twaweza hawakuvunja sheria yoyote katika utafiti wao wa hivi karibuni.

Fatma anasema kwamba maoni ya wananchi na tafiti za kisayansi (scientific research) ni vitu viwili tofauti na kwamba Costech, ambao ni wataalamu katika nyanja hizo, walipaswa kujua zaidi.

“Nadhani ni muhimu sana kwa wale wanaochaguliwa (teuliwa) kuongoza mashirika tofautitofauti ya serikali (umma) kuwa waelewa wazuri wa sheria zilizoanzisha mashirika hayo vinginevyo wanaweza kutumia vibaya madaraka yao,” anasema wanasheria huyo.

Maoni huwapa watu sauti

Semkae Kilonzo ni mratibu wa Policy Forum, mtandao wa asasi za kiraia 76 za Kitanzania anayeamini kwamba jaribio lolote la kuminya ukusanyaji wa maoni ya wananchi ni uingiliwaji wa haki za binadamu.

“Maoni ya wananchi ni muhimu kwa demokrasia iliyokomaa kwani huwapa watu fursa ya kutoa maoni yao kuhusu namna wanavyoongozwa,” anasema.

Akigusia zaidi uamuzi wa Costech, Kilonzo anaongeza: “…pia inahatarisha uhuru wa kuhoji ambao ni muhimu kwa watunga sera na wafanya maamuzi wakiwa wanatafuta suluhu sahihi na za kibunifu kwa matatizo kadhaa ya kijamii.”

Naye Samuel Muthuka, ambaye ni meneja wa taasisi ya kitafiti ya Ipsos-synovate kwa Tanzania anashauri kwamba ni muhimu mashirika na taasisi mbalimbali za kiserikali kunyoosha na kupangilia vizuri majukumu yake ili kuepusha sintofahamu katika jamii.

Tatifi ni nini?

Inawezekana Costech ilitumia sheria ya kiujumla inayoipa mamlaka Tume hiyo ya kuhifadhi na kusajili shughuli zote za kitafiti nchini na kuhakikisha kuwa tafiti hizo zinakidhi na kufuata “kanuni na taratibu za kitaifa.”

Kifungu 5(1) cha Sheria ya Na. 7 ya 1986 iliyoianzisha Costech inasema kwamba Tume itakuwa ni chombo kikuu cha ushauri kwa Serikali kwenye mambo yote yahusianayo na tafiti za kisayansi na maendeleo ya kiteknolojia nchini.

Wakati huohuo miongozo ya kitafiti ya Costech yenyewe inaielezea tafiti kama “aina yoyote ya uchunguzi wa kina, majaribio au tathmini iliyokusudiwa kuendeleza au kuchangia kwenye elimu ya ufahamu (body of knowledge).

Tafiti zinazoangukia katika dhana (definition) hii ya utafiti (research) ni zile ambazo mara nyingi hupelekea kubuniwa njia (design) mpya, bidhaa (product) au ‘processes’ (mtiririko wa vitendo (actions) au hatua (steps) zinazochukuliwa ili kufikia mwisho fulani) kwa ajili ya kuimarisha hali ya maisha ya binadamu.

Kilichofanywa na Twaweza Wataalam wa masuala ya kitafiti wameuelezea utafiti unaozozaniwa wa Twaweza kama ukusanyaji wa maoni ya wananchi unaojikita katika ufahamu, mitazamo na uzoefu wao wa masuala mbalimbali na si utafiti wa kisayansi na hivyo haupo chini ya mamlaka ya Twaweza. Wamesema tafiti za aina hiyo haziendani hata kidogo na dhana ya tafiti iliyotolewa na Costech iliyoelezewa hapo juu.

Lakini kwa asili yake ya kitakwimu, vyanzo vimelijulisha Mwananchi kuwa Twaweza imekuwa ikishirikiana na NBS, ambayo, kwa mujibu wa sheria ya takwimu ya 2015, inawajibika na uthibiti na usimamizi wa ukusanyaji na usambazaji wa taarifa zote za kitakwimu.

Baadhi ya wananchi, wakionekana kushangazwa na namna ambavyo Costech imelishughulikia suala la Twaweza, kwamba huenda kuna msukumo fulani.

+255 716 874 501

Columnist: mwananchi.co.tz