Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

YALIYOPITA SI NDWELE: Kasaka aanika alivyoongoza G-55 kudai Tanganyika

42072 PIC+KISAKA YALIYOPITA SI NDWELE: Kasaka aanika alivyoongoza G-55 kudai Tanganyika

Mon, 18 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mwaka 1993, Njelu Kasaka akiwa mbunge wa Chunya aliwasilisha bungeni hoja binafsi ya kutaka kuundwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano.

Miaka 26 baadaye, mwanasiasa huyo ameandika kitabu kueleza sababu za kufikia uamuzi huo.

“Mara nyingi nilipokutana na watu mbalimbali waliniuliza kutaka kujua mazingira yaliyokuwepo wakati wa mchakato na kabla ya mchakato wa Hoja ya Tanganyika maarufu kama G-55 kufika bungeni,” anaandika Kasaka katika shukrani zake mwanzoni mwa kitabu hicho kinachoitwa “Maisha, Siasa na Hoja ya Tanganyika”.

“Mimi ndiye niliyewasilisha hoja bungeni Agosti 23,1993. Na kila mara nilipotoa maelezo kwa watu walinishauri niandike kitabu.”

Katika kitabu hicho, Kasaka anaeleza jinsi alivyoitwa sehemu tofauti na viongozi wa juu wa Serikali kama Waziri Mkuu John Malecela, “viongozi wakubwa wa serikali ambao hawakutaka kujulikana” hadi Mwalimu Julius Nyerere alipoingilia kwa kumtuma Joseph Warioba kuwaambia kuwa anataka kukutana nao.

“Kusema kweli kilichokuwa kinamtesa Malecela si hoja ya Tanganyika, bali ni uamuzi wa Serikali yake kuiruhusu Zanzibar kujiunga na (Jumuiya ya Nchi za Kiislamu) OIC kinyume cha Katiba,” anasema Kasaka baada ya kueleza jinsi alivyomkatalia waziri huyo mkuu kuondoa hoja yake bungeni.

Pia anaeleza jinsi Samuel Sitta, ambaye alikuwa waziri wa sheria na katiba wa wakati huo, alivyoishauri serikali mbinu tatu za kuua hoja ya Tanganyika.

Chimbuko la hoja

Kasaka, ambaye Februari 2 alifikisha miaka 77, anaeleza kuwa mpango huo ulikuwa na wakati mgumu kuutekeleza wakati huo kutokana na nguvu ya Mwalimu Nyerere, ambaye licha ya kuachia urais aliendelea kuwa mwenyekiti wa CCM kwa miaka kadhaa.

“Mtu yeyote aliyejaribu kukosoa Muungano alioasisi yeye (Mwalimu) na Sheikh Abeid Amani Karume mwaka 1964 alihesabiwa kama ni mpinga Muungano na ni mtu anayetumiwa na maadui ili kuuvunja au kuusambaratisha,” anasema.

Anasema cha kushangaza alipothubutu kufanya hivyo, wabunge walimshangilia sana na mwisho wa mchango wake alipokea vikaratasi 112 vya pongezi za maandishi na kugundua kuwa wabunge walimshangilia si kwa sababu aliongea jambo walilolijua, bali kwa sababu ya ujasiri tu wa kuyasema matatizo ya Muungano huo hadharani na kwa ufasaha.

Mpango ulivyosukwa

Baada ya mchango huo, kundi la kwanza la wabunge wanane lilikutana naye nyumbani kwa mbunge wa Babati, Mateo Qaresi eneo la Upanga jijini Dar es Salaam Juni 13, 1993.

Anawataja baadhi ya wabunge hao kuwa ni William Mpiluka (Mufindi), Abdallah Nakuwa (Lindi Mjini), Arcado Ntagazwa (Kibondo), Lumuli Kasyupa (Kyela) na Jared Ghachocha (Ngara).

Anaeleza kuwa madhumuni ya mkutano huo ilikuwa kutengeneza mkakati wa namna ya kutekeleza wazo la kuunda Serikali ya Tanganyika na walikubaliana waunde kamati ya kusukuma mbele ajenda ya kuundwa kwa Serikali ya Tanganyika.

“Mimi nilipewa jukumu la kuwa katibu na mratibu wa mchakato huo na Qaresi akawa mwenyekiti wa kamati,” anasema.

Kamati hiyo ilikuwa hatua ya kwanza ya utekelezaji wa hoja yao na hatua ya pili ilikuwa ni kuwashawishi wabunge waunge mkono pendekezo hilo, na tatu ilikuwa ni kulifikisha kwa Naibu Spika Pius Msekwa.

Bunge wakati huo lilikuwa linaongozwa na Spika Adam Sapi Mkwawa, lakini kutokana na matatizo ya kiafya, hakuwapo na uongozi ulikuwa chini ya Msekwa.

Kundi la G-55

Kasaka anasema baadaye kazi ya kushawishi wabunge ilianza na yeye alichapisha karatasi ambayo ilizungushwa kwa wabunge kuwataka wanaounga mkono hoja wajiandikishe na kusaini.

“Haikuchukua muda, wabunge 44 walijiorodhesha na kutia saini. Idadi hii ya wabunge ilichukuliwa ni ya kutosha kuruhusu kumjulisha naibu spika kuhusu kusudio letu, baada ya kutueleza kuwa ilikuwa inawezekana ilimradi tu tuzingatie matakwa ya Kanuni za Kudumu za Bunge,” anasema.

Msekwa aliitangaza hoja kwa waandishi wa habari na kuijulisha Serikali.

“Vyombo vya habari vilipotangaza, umma ukapata habari. Shauku ya wananchi kwa hoja ya wabunge ikawa kubwa sana ingawa Redio Tanzania haikutangaza, ilichapishwa katika vyombo binafsi na gazeti la Mfanyakazi,” anasema.

“Mahudhurio ya wananchi katika viwanja vya Karimjee yaliongezeka sana. Hatukujua kwamba suala la Muungano na hasa kurudishwa kwa Serikali ya Tanganyika lilikuwa na mvuto kiasi hicho.”

Baadaye idadi ikafikia 57, lakini kabla hajaiwasilisha wawili kati yao wakajitoa na kubaki 55.

Aliyeomba kujiondoa ni Donald Ksenha (Dodoma Mjini) na Dk C.C Magoti (Mbunge wa Taifa).

Anasema wakati hamasa ikiendelea, Serikali iliunda timu ya kujadiliana na wabunge iliyoongozwa na Sitta. Wajumbe wengine ni mawaziri Edward Lowassa, Anne Makinda na Mohamed Seif Khatib.

Anasema hatua ya awali ya Serikali ilikuwa kuwataka waachane na hoja hiyo na kuiondoa bungeni, pendekezo ambalo walilikataa licha ya kufanya vikao sita.

Alisema baada ya majadiliano walikubaliana G-55 irekebishe hoja yake kwa kutaka wananchi washirikishwe katika kubadili sera ya CCM ya Muungano wa serikali mbili, jambo walilolikubali.

Lakini jitihada za kutaka hoja ifutwe zikaendelea, huku serikali ikiimarisha timu yake kwa kumuongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Damian Lubuva.

Ndipo baadaye walipobaini kuwa Sitta aliiandikia serikali mapendekezo matatu ya kuua hoja hiyo.

“Kwa kuwa hoja binafsi inahitaji kibali cha Spika kujadiliwa, Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais ambane Spika asitoe kibali na hoja itakufa,” anasema Kasaka.

Mbinu ya pili ilikuwa ni hoja hiyo kupelekwa kwenye mkutano wa wabunge wa CCM ambako serikali itapata muda wa kueleza hatua ambazo itachukua kutatua matatizo ya Muungano, na wabunge wengi wataelewa “hivyo kutokuwa na haja ya kuendelea na hoja”.

Na mbinu ya mwisho ni kuruhusu hoja iwasilishwe bungeni na baadaye Serikali kwa kutumia kanuni za Bunge itafanya mabadiliko kwenye hoja ambayo yatataka hoja nzima iondolewe.

Hata hivyo, Kasaka na wenzake wakaendelea na msimamo wao na baadaye wakaitwa na Malecela kabla ya Mwalimu Nyerere kuwaita na kujadiliana nao.

Anasema Mwalimu Nyerere aliwasikiliza na kuelewa hoja zao kuwa zinatokana na Serikali ya Muungano kutotekeleza wajibu wake na kuwataka waibane ili ifanye kazi yake ipasavyo.

Lakini akawatahadharisha kuwa hoja yao itaua Muungano, akisema hata kama ameambiwa mama yake ni mchawi na dawa yake ni kumuua, hangekubali na kuwashauri wakatafakari.

Kasaka anaeleza jinsi walivyosimama imara hadi hoja yao iliposomwa bungeni na baadaye kupitishwa.

“Niliwasilisha hoja yangu kwa niaba ya kundi maarufu la wabunge la G-55 lililokuwa likiwakilisha wabunge zaidi ya 100, waliokuwa wamejipanga kuunga mkono,” anaandika Kasaka.

Kasaka anaeleza alianzisha hoja hiyo baada ya kuona mfumo wa serikali mbili haufai na kutaka Serikali iondokane nao mapema iwezekanavyo.

Anaeleza kuwa mfumo huo ulikuwa hautoi haki sawa kwa nchi shiriki.

Kasaka anawanukuu wananchi wa Zanzibar wakiushangaa mfumo huo kuwa ni wa ajabu ulimwenguni kwa kuwa “nchi moja haijapewa haki inayostahili na moja imependelewa zaidi kuliko nyingine”.

Anasema baadaye ndipo harakati za kukwamisha utekelezaji wa hoja hiyo ulipoanza.

Anasema Mwalimu Nyerere hakuridhishwa na hatua ya Bunge na katika mkutano wa wabunge wa CCM uliofanyika ukumbi wa Kilimani aliwashutumu Malecela na Horace Kolimba kwa kuruhusu suala hilo lifike bungeni, huku akimkingia kifua Rais Ali Hassan Mwinyi.



Columnist: mwananchi.co.tz