Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Wiki ya utafiti Udsm ilivyoibua ukweli wa kifo cha Chifu Mkwawa

58746 Mkwawa+pic

Tue, 21 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Historia ya Tanzania inamtaja mtu aliyeitwa Chifu Mkwawa, anayekumbukwa kwa ushujaa wake wa kupambana na wakoloni wa Kijerumani. Hata hivyo, kuna utata wa kifo chake. Maswali ni je, alikamatwa na kuuliwa kwa kupigwa risasi na maadui wake, alijinyonga, alijipiga risasi. Kipi hasa kilichotoa uhai wa roho yake? Utafiti mpya umebaini ukweli wa kifo chake.

Utafiti ni silaha muhimu katika kupima ubora wa chuo kikuu chochote duniani. Taasisi za elimu ya juu zinatakiwa kufanya tafiti ambazo zinalenga kutatua changamoto za jamii kwa kuja na majawabu ya kivumbuzi na kibunifu.

Wiki ya maonyesho ya utafiti iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) ilitoa nafasi kwa chuo hicho kuonyesha aina mbalimbali za utafiti zilizofanywa na wataalamu wake, ukiwamo wa ukweli kuhusu kifo cha aliyekuwa kiongozi wa Wahehe aliyepambana na Wajermani. Huyu ni Chifu Mkwavinyika Munyigumba Mwamuyinga, maarufu kwa jina la Mkwawa

Akifunga maonyesho hayo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako anatoa wito kwa vyuo vikuu vyote nchini kufanya tafiti nyingi na kuzichapisha ili kujiongezea nafasi ya ushindani katika ubora wa vyuo.

Kwa mujibu wa orodha ya vyuo vikuu bora Afrika iliyochapishwa katika tovuti ya www.4icu.org, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimeshika nafasi ya 44 kikifuatiwa na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (nafasi ya 101), Chuo Kikuu cha Dodoma (nafasi ya 147), Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (nafasi ya 175) na Chuo Kikuu cha Mzumbe (nafasi ya 184).

Profesa Ndalichako anasema vyuo vingi vya Tanzania viko chini katika ubora kwa sababu wanaopima ubora wanaangalia kiwango cha tafiti zilizofanyika na kuchapishwa hasa katika taasisi zinazofahamika duniani.

Pia Soma

“Vyuo vyote nchini vitenge fedha kwa ajili ya kufanya utafiti kwa sababu fedha wanazo, wanakusanya ada za wanafunzi. Tunasisitiza utafiti kwa sababu wanaopima ubora wa vyuo wanaangalia utafiti na machapisho katika chuo husika,” anasema.

Ukweli wa kifo cha Mkwawa

Baadhi ya tafiti zilizoonyeshwa katika wiki hiyo ni pamoja na ukweli juu ya kifo cha Chifu Mkwawa

Mhadhiri na mtafiti kutoka Idara ya Mambo ya Kale chuoni hapo, Dk Frank Masele anasema kumekuwa na taarifa mchanganyiko kuhusu kifo cha Mkwawa, baadhi ya taarifa zikisema alijinyonga, nyingine zikieleza kwamba alipigwa risasi na nyingine zikisema alijipiga risasi.

Anasema kutokana na utafiti walioufanya katika pango alimojificha Mkwawa wakati wa vita na wakoloni wa Kijerumani, wamebaini kwamba Mkwawa alijiua kwa kujipiga risasi na ganda la risasi iliyotumika lilipatikana ndani ya pango hilo.

“Ushahidi wa kwanza tulipata risasi aliyoitumia kujiua kwenye pango hilo. Pili, tumechunguza fuvu la kichwa chake na kuona kuna tundu la risasi iliyokuwa inatoka juu ya kichwa na tatu, kuna ushahidi wa diary aliyoandika mjerumani aliyemkata kichwa akimweleza ‘boss’ wake kwamba walikuta amejipiga risasi. Kwa hiyo tumejiridhisha bila wasiwasi kwamba Mkwawa alijiua kukwepa mkono wa wajerumani,” anasema Dk Masele.

Utafiti ulivyofanyika

Anasema alianza kufanya utafiti wake mwaka 2006 Canada wakati akisoma shahada yake ya uzamivu kuhusu zama za mawe za kati, hivyo alikuwa akitembelea mapango mbalimbali kila anaporudi nchini.

Agosti 8, 2010 ndipo alipookota ganda la risasi ambayo Mkwawa aliitumia kujiua kwenye pango lililopo katika kijiji cha Magubiko mkoani Iringa. Anasema alilichukua ganda hilo na kwenda nalo Canada kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Dk Masele anasema akiwa huko Canada aliwatumia picha za ganda hilo la risasi wataalamu wa silaha wa huko Ujerumani ili waweze kuitambua. Walimpa taarifa za risasi hiyo na kwamba ilitengenezwa Ujerumani.

Anasema mwaka 2012 ndipo alitembelea mapango ya Magubiko ambako risasi hiyo iliokotwa. Wakati wanaanza utafiti ilibidi wapite kwenye Makumbusho ya Kalenga. Walipofika huko walibaini kwamba ganda hilo la risasi lilifanana na risasi za Wajerumani zilizohifadhiwa kwenye makumbusho hiyo.

Baada ya hapo, anasema ilibidi waende kwenye kijiji cha Lugalo ambako ndiyo ulikuwa uwanja wa mapigano kati ya Mkwawa na Wajerumani mwaka 1881.

“Tulibaini kwamba kuna mfanano mkubwa wa maganda ya risasi katika maeneo yote matatu. Risasi hizo zilikuwa zikimilikiwa na vikosi vya Wajerumani wakati wa mapigano hayo,” anasema Dk Masele.

Mtafiti huyo anasema bado utafiti unaendelea kwa sababu amepata taarifa wananchi wameokota maganda ya risasi kwenye mashamba yao, hivyo atakwenda tena Iringa kuzichunguza risasi hizo.

Utafiti kuhusu muhogo

Maonyesho hayo ambayo awali yalifunguliwa na Waziri Mkuu msataafu, Mizengo Pinda yalimuibua mwanafunzi wa mwaka wa nne wa shahada ya awali ya Sayansi na Teknolojia ya Vyakula chuoni hapo, Eric Mwageni ambaye ametengeneza virutubisho vya wanga kutoka kwenye muhogo ambavyo vinaweza kutumika kwenye vyakula vingine kama vile biskuti, juisi au maziwa.

Anasema virutubisho hivyo vinasaidia kuongeza wanga mwilini, pia kufanya chakula au kinywaji kisikatike bali kichanganyikane vizuri. Anasema mpaka sasa hakuna mtu anayetengeneza virutubisho hivyo hapa nchini bali vinaagizwa kutoka nje.

“Faida ya huu utafiti wangu ni kwamba tumeuongezea matumizi muhogo ambao unapatikana kwa urahisi hapa nchini. Pia, unaongeza virutubisho mwilini na unaboresha vyakula vingine. Ni rahisi kutengeneza majumbani, huhitaji kuwa na mashine kubwa, ni vifaa vya kawaida kama blenda,” anasema mwanafunzi huo.

Columnist: mwananchi.co.tz