Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Watoto wapewe kazi zinazolingana na uwezo wao

11159 Waotot+pic.png TanzaniaWeb

Tue, 10 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kwa miezi kadhaa nimekuwa nikifuatilia kazi za kimasomo wanazopewa watoto wa madarasa ya awali kwa minajili ya kuzikamilisha wakiwa nyumbani. Nimefuatilia kazi za darasa la kwanza, la pili na la tatu kwa baadhi ya masomo ikiwemo sayansi na hesabu.

Niliamua kufuatilia kazi hizi kwa lengo la kuelewa dhima hasa ya kazi hizi hasa baada ya kuwa nimestushwa na kazi aliyokuwa akiifanya mtoto wa rafiki yangu mwaka jana.

Mtoto huyo, kwa wakati huo akisoma darasa la tatu kwenye shule zinazotumia lugha ya Kiingereza maarufu kama English Medium, alikuwa akifanya kazi za somo ambalo kwa Kiswahili tunaweza kuliita Sayansi na Teknolojia.

Nilishangazwa kuona mtoto wa miaka tisa kama yule anafanya maswali ambayo mimi niliyafanya nikiwa kidato cha kwanza sekondari. Sikuelewa mantiki ya kazi za namna ile kwa mtoto wa umri ule.

Rafiki yangu mwenye mtoto alitetea kazi zile akiamini zinamsaidia mtoto kupanua uwezo wake kuliko ilivyokuwa enzi zetu. Sikuafikiana naye kwa hivyo niliamua kufanya utafiti mdogo kujiridhisha.

Naamini na wewe, kama mzazi, unao uzoefu wa mazoea haya ya watoto kurudi nyumbani na kazi za shule. Je, unafikiri ni kwa kiwango gani kazi hizo zinamsaidia mwanao?

Umuhimu wa kazi za nyumbani

Binafsi sikumbuki ni lini nikiwa shule ya msingi niliwahi kwenda nyumbani na kazi za shule. Kazi zote za masomo zilikamilika ndani ya muda wa shule na tuliporudi nyumbani hatukuwa na ‘presha’ ya kufanya kazi za shule na sidhani kama tulipungukiwa kitaaluma.

Walimu wetu walipohisi kuna maeneo tunahitaji mkazo zaidi, tulilazimika kwenda shule mapema zaidi lakini sikumbuki ni lini nikiwa darasa la tatu nilikaa mezani nyumbani kufanya hesabu zinazotakiwa na mwalimu kesho yake.

Sina maana ya kubeza umuhimu wa kazi za nyumbani kwa wanafunzi. Ninafundisha walimu na ninawapa wanafunzi wangu kazi za nyumbani. Nafahamu zina faida kubwa mbili.

Kwanza, kumpa mwanafunzi wasaa wa kujifunza kwa kina zaidi maarifa anayokutana nayo darasani. Mwalimu anapompa mwanafunzi kazi hizi, nia inakuwa kumhimiza kufanya mazoezi zaidi na hivyo kuimarisha uelewa wake.

Lakini pia, kazi hizi humsaidia mwanafunzi kuyafanya maarifa anayojifunza darasani kuwa sehemu ya maisha yake. Ndio maana tunawashauri walimu wanapotoa kazi za nyumbani, wajitahidi kuhakikisha zinamfanya aoanishe kile alichojifunza na maisha yake nje ya darasa.

Changamoto nilizozibaini

Katika kufuatilia kazi wanazopewa wanafunzi wetu, nimebaini changamoto kubwa tatu. Mosi, watoto wanapewa kazi zisizowasaidia kupanua uelewa wao.

Kazi nyingi wanazopewa ni marudio ya mambo yale yale wanayojifunza darasani, hivyo zinawahimiza kukariri kuliko kuelewa.

Nimekutana na mfano wa mtoto wa darasa la tatu anayefundishwa sifa za viumbe hai, akiwa na maswali yaleyale yaliyofundishwa darasani. Kwa hiyo mtoto huyu anapokwenda nyumbani atajikuta akirudia kilekile alichofundishwa na mwalimu darasani kwa kukariri zaidi.

Katika mazingira kama haya, ile mantiki ya kazi za nyumbani kumpa fursa mtoto kujifunza kwa kina zaidi kile alichokisikia darasani inapotea, kwa sababu mtoto anajikuta anafanya kazi ya kurudia kile ambacho angeweza kukifanya akiwa darasani.

Pili, kazi nyingi wanazopewa wanafunzi haziwapi fursa ya kutosha kuoanisha maarifa ya darasani na maisha yao ya kila siku. Mtoto anapewa maswali yasiyomfanya afikiri nje ya wigo wa darasa na hivyo kazi hizo zinakuwa hazimwongezei tija inayokusudiwa.

Kuna mantiki ipi kwa mfano, kumpa mtoto maswali 20 ya hesabu akayafanyie nyumbani wakati kimsingi angeweza kuyafanya katika muda wa darasani? Kama mwalimu ana dakika 40 za kufundisha, kwa nini maswali haya yasiwe sehemu ya somo?

Lakini tatu, kazi nyingi wanazopewa watoto zinaonekana ama kuwazidi uwezo wao au haziandaliwi kwa umakini. Kuna kazi niliona mtoto wa darasa la pili anatakiwa ataje tabia hatarishi zinazoweza kuambukiza virusi vya Ukimwi.

Matarajio yangu ni kwamba ingetosha kumfundisha vitu vya kawaida kama kuchangia mswaki, vitu vyenye ncha kali, kugusa damu ya mwenzako na tabia nyingine zinazolingana na uelewa wa mtoto.

Lakini nilishangaa mwalimu anataka mtoto wa darasa la pili ataje ngono kama njia moja wapo na matumizi ya kondom kama mbinu ya kujikinga na virusi vya Ukimwi. Nikajiuliza busara ya maswali kama haya ni nini?

Kazi za aina hii ndizo zinachangia udanganyifu wa wazazi kuzifanya kwa niaba ya watoto ili tu ionekane mtoto ameelewa. Lakini je, hilo ndilo lengo? Kuna sababu gani ya kuwapa watoto kazi zinazowakuza kabla ya wakati wao?

Pengine hili ni tatizo la maudhui ya mtalaa unaotumika kufundishia lakini kuna ukweli pia kuwa shule nyingi zinazotumia lugha ya Kiingereza huona ufahari kuwapa watoto mambo mengi ya kujifunza kwa wakati mmoja. Lengo, nafikiri, ni mkakati wa kibiashara zaidi.

Ushauri kwa walimu

Kadri inavyowezekana, mwalimu atumie muda wa darasani kutoa maswali ya ziada ndani ya kipindi chake. Tuwaache watoto watumie muda wao nje ya darasa kushiriki shughuli nyingine zenye tija sawa na masomo.

Pale inapolazimu kutoa kazi za ziada zinazohitaji muda zaidi, mtoto apewe kazi zinazojenga ujuzi zaidi badala ya kumkaririsha maarifa yaleyale aliyojifunza darasani.

Kazi za kusoma hadithi, kwa mfano, zinaweza kuendeleza vizuri zaidi kile alichojifunza darasani na wakati huo huo mtoto akikuza uwezo wake wa kusoma.

Aidha, badala ya kumpa mtoto maswali yanayorudia alichojifunza darasani, mwalimu ampe mtoto maswali yanayomsaidia kuona kile alichojifunza darasani katika maisha yake halisi.

Lakini pia ni muhimu kuzingatia mazingira halisi aliyonayo mtoto. Hakuna sababu ya kumpa mtoto kazi atakazolazimika kupata msaada wa mtu mwingine kwa lengo tu la kujiridhisha amepata ‘vema.’ Tusifanye maigizo yasiyomsaidia mtoto.

Blogu: http://sw.globalvoices.org Twitter: @bwaya

Columnist: mwananchi.co.tz