Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Watawala wa Afrika bila ‘warithi’ hakuna kuondoka

13217 Pic+watawala TanzaniaWeb

Thu, 23 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Baada ya shinikizo kubwa na Katiba ya nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kumzuia Rais wa nchi hiyo Joseph Kabila kuendelea kuitawala nchi hiyo hatimaye amekubali yaishe kwa kumtangaza mrithi wake Emmanuel Ramazani Shadary kuwa ndiye mgombea urais kupitia Muungano wa vyama vinavyounda Serikali nchini humo.

Wakati Kabila akibwaga manyanga, jirani yake upande wa Kaskazini, Rais Omar Hassan Al Bashir wa Sudan ameagiza wabunge kutoka katika chama tawala cha National Congress waanze mchakato wa kubadilisha katiba ili kuondoa kipengele kinachomzuia kuendelea kutawala nchi hiyo hadi 2020.

Hii ndiyo kusema kuwa hana mpango wa kuondoka ifikapo mwishoni mwa kipindi chake cha urais.

Kabila amekuwa akituhumiwa na wapigania haki za binadamu wa ndani na nje kuwa katika utawala wake amekiuka haki za binadamu kwa kiwango kikubwa na vilevile amejitajirisha kwa kiasi kikubwa kupitia fedha za umma, hivyo ilikuwa ni mwafaka kumpata mrithi mtiifu kwake.

Kabila ambaye amejaribu karibu njia zote kuendelea kubaki madarakani na kushindikana, amefika mahali ambapo alikuwa hana njia nyingine ila ni kumwingiza Shadary ambaye atamlinda yeye na biashra zake.

Wapo baadhi ya Waafrika ambao wamemsifu kwa kitendo chake cha kuondoka madarakani akiwemo Cyril Ramaphosa ambaye ni Rais wa Afrika Kusini, ambaye zipo habari kuwa ni mwenza wake katika biashara ya madini hukohuko DRC na Ramaphosa hakufanya ajizi alifunga safari kwenda DRC saa 48 tu baada ya Kabila kumtangaza Shadary kuwa mgombea.

Kabila amezidisha miaka mwili katika utawala wake ambao ulitakiwa kwisha 2016. Yeye mwenyewe aliingia madarakani katika mtindo ambao unafanana sana na usultani pale baba yake Laurent Desire Kabila alipouawa na walinzi wake mwaka 2001.

Unapoitazama mifano hii miwili inakupa jibu kuwa kuna baadhi ya viongozi wa Afrika, kama hawajawapata watu waaminifu kwao, basi hawako tayari kuondoka madarakani na wanachoweza kufanya ni kusigina katiba ili waendelee kuwepo katika utawala.

Kwa Rais Bashir inaonekana kuwa hajampata mrithi wake mwaminifu na hivyo ameamua kuwa ni vizuri aendelee kuwapo madarakani kwani mpaka sasa ameishakuwa kiongozi wa nchi hiyo kwa kipindi cha miaka 29.

Bashir ambaye ameshtakiwa katika Mahakama ya Haki za Binadamu na mauaji ya kimbari huko The Hague Uholanzi anaona kuwa kwa sasa wakati haujafika kuondoka kwani mashtaka hayo yawaweza kumpotezea uhuru alio nao hata akiondoka madarakani, hivyo ni jambo la kufa na kupona kuendelea kubaki madarakani.

Zipo habari kuwa Rais Museveni wa Uganda naye anamwandaa mwanaye Muhoozi Kainerugaba kumrithi. Ilikuwa ikitarajiwa kuwa Museveni angemwachia mwanaye siku za karibuni lakini baada ya upinzani kutoka kwa maofisa wa ngazi za juu ndani ya vyombo vya usalama inaonekana jambo hilo limeahirishwa kwa muda, na ili kufanikisha mpango huo kumefanyika mabadiliko ya katiba ili Museveni aendelee kutawala pasipo kikomo na kwa kufanya hivyo kutapunguza mhemuko uliokuwepo miongoni mwa Waganda. Kainerugaba kwa sasa ni msomi mzuri katika masuala ya kijeshi na ni Meja Jenerali akiwa na umri wa miaka 44 na ndiye mkuu wa kikosi maalumu cha ulinzi wa Rais.

Huko Afrika ya Magharibi, Theodore Obiang Nguema wa Equatorial Guenia anamwandaa mwanaye, Theodorin kuwa mrithi wake na amemteua kuwa Makamu wa Rais anayeshughulikia ulinzi na usalama.

Rais mstaafu wa Angola, Jose Eduardo Dos Santos aliitawala nchi hiyo kwa kipindi cha miaka 37 huku wakati mwingine afya yake ikiwa tata lakini hakuondoka mpaka alipompata Joao Laurenco kumrithi. Vilevile Omar Bongo wa Gabon naye alifanya hivyohivyo kwa mtoto wake, Ali Bongo ambaye mpaka leo yupo madarakani.

Wapo waliojaribu lakini mambo hayakwenda vizuri mfano mzuri ni wa Robert Mugabe wa Zimbabwe alitaka mkewe Grace amrithi lakini wanajeshi wakaona maslahi yao yalikuwa hatarini, hivyo wakaamua kumwondoa Mzee na kuyeyusha mipango yake.

Muamar Ghadafi wa Libya baada ya kutawala kwa miaka 42 alikuwa akimwandaa mwanaye, Seif Al Islam lakini vuguvugu la mapinduzi likamwondosha kabla hajafanya hivyo, ilikuwa hivyohivyo kwa Hosni Mubarak wa Misri naye aliondoshwa kabla hajampatia mwanaye zawadi ya nchi.

Afrika viongozi wengi hawapendi kuondoka pasipo kujua hatima yao baada ya kuachia madaraka kwa sababu wakati wakiwa madarakani huwa ni wakati mwafaka wa kujitajirisha kwa kupora fedha na raslimali za nchi, kuhujumu haki za binaadamu, kutawala kwa upendeleo na hata kuendesha biashara zisizo halali wakishirikiana na ndugu zao au wateule wao.

Watawala hujilimbikizia fedha nje ya Afrika na hasa katika nchi za Panama, Uswisi na visiwa vya Uingereza vilivyoko bahari ya Carribean.

Wakati wa kuingia wanatoa ahadi nyingi za kuendeleza watu wao lakini muda mfupi huwa ni adui wa walewale ambao waliahidi kuwa watawasaidia.

Mapambano dhidi ya umaskini, ujinga na maradhi yanakuwa ni sehemu ya mazungumzo lakini vitendo ni kuiba na kuhamisha raslimali za mataifa yao kwenda ughaibuni.

Wakati mwingine wakitaka kuondoka walio karibu nao kama ndugu na wateule wao huwashurutisha kubaki kwani kwa kufanya hivyo nao wanaendelea kura urua.

Mwaka 2008 wakati Robert Mugabe aliposhindwa kwa Morgan Tsivangrai, kiongozi wa MDC, alikuwa tayari kuondoka lakini waliokuwa karibu naye walimkatalia na hatimaye akaendelea na walipoona maslahi yao yanaelelekea kutishiwa mwaka 2017 wakamwondosha madarakani.

Ni jambo la kawaida kiongozi mpya anapoingia wapo watu ambao siku si nyingi za nyuma walikuwa ni wa kawaida lakini huanza kumiliki utajiri ambao hauna maelezo ya jinsi unavyopatikana, biashara kubwa kama usafirishaji zikihusisha ununuaji wa malori, meli na hata ndege ambao huambatana na kandarasi nono kutoka kwa serikali au marafiki walioko nje, husitawisha miradi yao na hata kuwafanya watu waamini kuwa watu hao ni hodari sana wa biashara lakini ndugu yao huyo akiondoka nao wanayeyuka kama barafu kwa sababu mirija ya wizi kwa kisingizio cha biashara huwa imekatika.

Uteuzi wa nyadhifa mbalimbali katika idara za serikali na mashirika ya umma huenda kwa makabila yao au wapendwa wao ambao huendesha magenge ya uporaji wa fedha za serikali na ulaji rushwa pasipo kuguswa na mkono wa sheria na wale wanaohoji hali hiyo huishia kuuawa, kufungwa kwa visingizio vya uchochezi au kuzihama nchi zao na kwenda kuishi uhamishoni.

Makundi haya ambayo ni sehemu ya mtawala hayako tayari kuona kuwa kiranja wao anaondoka, hivyo kila mbinu zitafanyika ili aendelee kusalia madarakani huku wao wakijineemesha na hata inapoonekana kuwa watu wamechoka itaundwa mizengwe mingi na ikishindikana basi kubadilisha katiba ili mwenzao aendelee kuwepo juu ndiyo huwa dawa iliyobaki.

Wapo wale wenye hofu kuwa wakiondoka makaburi ya mauaji na mateso kwa watu wao waliyoendesha katika zama zao yatafukuliwa na kujikuta wakifikishwa mahakamani, hivyo ni lazima taratibu za kuondoka salama zifanyike na anayekuja lazima ajulikane tabia yake kwa mfalme anayeondoka.

Inavyoonekana katika Afrika kuwa kiongozi ni kama sehemu ya mfumo wa mzunguko wa damu ambapo ikitokea kuwa mtawala anaondoka na moyo unashindwa kusukuma damu hiyo, hivyo basi ili kufanikisha uhai wa binadamu huyu ni lazima kuendelea kutawala au kuwa na mbadala wa kuendesha mapigo ya moyo ambapo mtu mwaminifu husimikwa kwa kutumia kila aina ya hila.

[email protected]. 0783 165 487

Columnist: mwananchi.co.tz