“Niliwahi kuagiza pochi nzuri niliyoipenda lakini nilipolipa na kuletewa ikawa ni pochi ya kitambaa. Sikuweza kubadilisha nikalazimika kuendelea kuitumia hivyo hivyo,” anasema Josephine Victor, mjasiriamali wa jijini Dar es Salaam.
Josephine anafanya biashara ya chakula na mara nyingi hutumia mitandao ya kijamii kutangaza bidhaa zake. Kutokana na mazoea hayo anasema inakuwa rahisi kwake kununua chochote atakacho mtandaoni ingawa changamoto zilizopo huwa zinamuumiza.
Josephine ni mmoja kati ya wengi wanaoumia mtandaoni hasa wanaponunua kutoka kwenye vyanzo ambavyo si salama.
Keneth Ephrahim ni mpiga picha wa sherehe na matukio mbalimbali jijini hapa ambaye ili kuboresha huduma zake aliagiza kamera ya kisasa kutoka mtandao wa ebay lakini hakupata alichokitarajia.
“Ebay ni tovuti kubwa ya mauzo lakini ukiingia mtandaoni utakutana nazo nyingi. Nadhani sikuwa makini kiasi cha kutosha, badala ya kuingia kwenye tovuti halisi nikaingia kwenye nyingine yenye jina linalokaribiana na hilo, nilipoteza hela zangu,” anasema Ephrahim.
Kupoteza fedha kwa biashara inayofanyika mtandaoni haiwakuti wananchi wa kawaida peke yao bali hata kampuni hasa zinapotaka kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi.
Mwaka jana pekee kwa mfano, kampuni saba ziliripoti ubalozi wa Tanzania uliopo nchini China kutapeliwa mamilioni ya Shilingi walizolipia bidhaa walizozihitaji.
Baadhi ya kampuni hizo, balozi wa Tanzania nchini humo, Mbelwa Kairuki anasema zilituma fedha ila hazikutumiwa bidhaa zilizoagiza na nyingine zilituma fedha lakini bidhaa walizotumiwa ni tofauti na walichotegemea.
Balozi anasema utapeli huo umezisababishia hasara ya Dola 300,000 kampuni hizo hivyo kuwataka Watanzania kuwa makini wanapojihusisha na kampuni za mtandaoni.
“Ubalozi unapenda kutoa angalizo kwa Watanzania wanaotaka kufanya biashara na kampuni za Kichina wanazozipata kwa njia ya mtandao kuchukua tahadhari ili kuepuka kutapeliwa,” anasema Mbelwa.
Kupunguza uwezekano wa kutapeliwa, anasema ubalozi upo tayari kuwasaidia wafanyabiashara huku akibainisha hatua wanazopaswa kuzizingatia.
Anasema kwa mwananchi yeyote au kampuni inayotaka kununua bidhaa mtandaoni kutoka China basi ahakikishe analijua jina kamili la kampuni anayotaka kufanya nayo biashara.
Vilevile, anasema “ni muhimu kulijua jina la Kichina la kampuni husika kwani mfumo wa msajili wa kampuni nchini China unatambua majina ya Kichina tu.”
Licha ya jina la kampuni, ni vizuri kupata majina kamili ya Kichina ya mhusika wa kampuni unayewasiliana naye na itapendeza zaidi ukimuomba utambulisho wake wa akaunti ya Wechat.
Kabla ya kutuma fedha, anasema ni muhimu kujiridhisha (due diligence) juu ya uwepo wa kampuni husika na kupata taarifa za uwezo wake kimtaji na rekodi ya biashara.
“Mwenye kuhitaji huduma hiyo anaweza kuwasiliana na ubalozi wa Tanzania nchini China kwa baruapepe [email protected] au ofisi ya mwakilishi wa uchumi na biashara wa ubalozi wa China nchini Tanzania,” anasema Mbelwa.
Baada ya kuthibitisha sifa na uwezo wa kampuni husika kufanya biashara inayokusudiwa, ni muhimu kuingia mkataba wa biashara utakaokuwa na taarifa za pande zote mbili.
Baada ya kukamilika kwa mkataba huo, njia salama zaidi ya kufanya malipo ni kutumia huduma ya ‘letter of credit’ inayotolewa benki zote za biashara inayokupa uwezo wa kuzuia malipo endapo muuzaji amekiuka makubaliano ya mkataba.
Kwa ununuzi mkubwa unaozidi Dola 20,000 balozi anashauri kuweka kipengele cha ukaguzi kabla ya kusafirishwa kwa mzigo (pre-shipment inspection) katika mkataba ili kujiridhisha iwapo bidhaa iliyotumwa ndiyo iliyoagizwa.
“Endapo hatua hizi zitazingatiwa, ubalozi unaamini itapunguza kwa kiasi kikubwa uwezekano wa Watanzania kutapeliwa mtandaoni,” anasema Mbelwa.
Ingawa changamoto za kiteknolojia zinajitokeza, uhusiano wa Tanzania na China umedumu kwa zaidi ya miaka 50 sasa huku zikisaidiana na kushirikiana katika maeneo tofauti.
Kati ya mwaka 1990 na 2017, takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) zinaonyesha China imewekeza zaidi ya Dola 5.9 bilioni za Marekani hivyo kuifanya iongoze orodha ya mataifa yaliyowekeza kiasi kikubwa zaidi nchini.
Baadhi ya wataalamu wa masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wanasema Watanzania wanapenda sana kutumia mitandao lakini hawana elimu ya kutosha hivyo inakuwa rahisi kwao kutapeliwa.
Mpaka Desemba 2018, takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha kulikuwa na zaidi ya watumiaji milioni 23.14 wa intaneti inayowapa fursa ya kuwasiliana na watu kutoka maeneo tofauti duniani.
“Watu waache kuhemka. Wengi wakisikia kuna kitu fulani mtandaoni basi hukimbilia huko. Kwa wanaoagiza bidhaa za biashara watumie mawakala au benki za biashara,” anashauri James Mahinya, mtaalamu wa Tehama wa kujitegemea.
Mahinya anatoa mfano wa Benki ya Dasheng kutoka China hata za hapa nchini kwamba zina mtandao mkubwa wa mawasiliano na ufuatiliaji unaoondoa uwezekano wa kutapeliwa hivyo zitumike kufanikisha miamala ya biashara.
“Kuna wizi mkubwa sana unafanyika mtandaoni. Benki za kimataifa pamoja na kampuni zimeshatapeliwa kwa njia za kisayansi hivyo wananchi wanapaswa kuwa makini zaidi,” anashauri Mahinya.
Mkurugenzi wa masuala ya kisekta wa TCRA, Dk Emmanuel Manase anasema mawasiliano ya intaneti yanafanikisha mambo mengi hivi sasa na wengi wanaoyatumia vizuri wanafurahia urahisi uliopo.
“Huwa tunasisitiza mawasiliano yatumike kwa maendeleo na miamala ya fedha ifanyike baada ya kupata taarifa sahihi,” anasema Dk Manase.
Kwa upande wake, kaimu mkurugenzi mkuu wa Kamisheni ya Teknolojia na Mawasiliano Tanzania, Samson Mwela anasema mtandaoni kuna matapeli kama ilivyo kwenye maeneo ya kawaida yaliyozoeleka na wasiokuwa makini wanapoteza fedha zao.
Naye anasisitiza juu ya kuiridhisha na mtu au kampuni unayowasiliana nayo mtandaoni kabla ya kufanya malipo pamoja na kununua chochote kutoka kwenye mifumo inayofahamika na kueleweka.
“ukinunua kutoka kwenye tovuti zinazofahamika na kuaminika unajiweka kwenye usalama zaidi wa kutopoteza fedha zako. Mtandaoni kuna matapeli wengi,” anasema Mwela.