Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Wasauzi walivyomsahau Nyerere na Tanzania yake

34662 Nyerere+pic Tanzania Web Photo

Fri, 4 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Nazurura katika jiji la Johannesburg tangu Desemba 24. Krismasi imenikuta hapa. Siku saba baadaye mwaka mpya umenikuta hapa. Nazurura tu sina jipya sana. Mji wao upo kimya kwa sababu wazawa au Wasauzi kama tunavyowaita wana tabia za ‘kichaga’. Nyakati hizi wanakwenda makwao kutambia kula sikukuu.

Wachache waliobaki naendelea kupiga nao soga katika mabaa. Soga zile zile ambazo huwa napiga na wale waliokwenda makwao. Wanaijua Tanzania? Wanamjua mtu anayeitwa Julius Kambarage Nyerere? Wanajua tulivyowasaidia katika ukombozi dhidi ya makaburu?

Majibu yao yanategemea na umri wao. Wakati mwingine nabakia kumshangaa Mwalimu. Sijui kwa nini aliamua kuwapambania watu ambao baadae wangemsahau. Ukipiga soga na Wazee wa Afrika Kusini wanamkumbuka Mwalimu na wanaheshimu harakati zake.

Ukipiga soga na vijana wala hawana habari na Mwalimu. Hawamjui. Wachache wamemsoma shuleni. Hawajui jinsi Tanzania ilivyokuwa kiongozi wa harakati za wapigania uhuru. Hawajui chochote, sana sana wanatushangaa kwa umaskini wetu na jinsi tunavyozamia nchini kwao kusaka riziki.

Kumbe ni bora Mwalimu angekuwa bize na masuala ya uchumi wa nchi yake tu. Binadamu hawana fadhila. Binadamu pia hawahifadhi kumbukumbu. Sifa chache ambazo tumebakiwa nazo zinaondoka na wazee wanaofariki kila pembe ya Afrika.

Napata faraja nikipiga soga na wazee wa Afrika Kusini lakini nikipiga soga na vijana naumia moyoni. Wanaongea lugha za maudhi tu kuhusu umasikini wetu. Wanachojua wao ni kusifia fukwe za Zanzibar. Basi. Kumbe huwa wanakuja kulewa kule na kuondoka zao.

Hotuba za viongozi wetu wa kileo zimejaa majigambo mengi ya Tanzania na ukombozi wa bara la Afrika lakini ukweli ni kwamba haijamsaidia sana Mtanzania wa kawaida aliyechoka na jembe lake pale Newala. Katika siku za usoni tusirudi tena katika mtego wa kusaidia wengine kabla hatujajisaidia.

Nchi nyingi ambazo tulisaidia kuzikomboa kwa sasa zinatucheka kiuchumi. Ni ukweli unaoumiza, lakini kinachoumiza zaidi ni pale unapokutana na kijana wa Afrika Kusini aliyevaa mlegezo ambaye haijui hata sura ya Mwalimu Nyerere na anatoa maneno mengi ya kebehi.

Ikifikia hatua hiyo napiga glasi yangu ya mwisho ya mvinyo, nasonya, naondoka zangu. Ikiwa unadhani inapozungumzwa Tanzania huwa inazungumzwa na watu wa marika yote nje ya mipaka. Hapana. Vijana wa kileo wamesahau.



Columnist: mwananchi.co.tz