Kuvunjwa mikono, kuachwa na makovu mwilini pamoja na athari hasi za kiwango kikubwa zaidi kwa maana ya vifo ni matukio mbalimbali yaliyotendwa na yanayoendelea kutendwa dhidi ya wanafunzi huku sababu kubwa ikihusisha adhabu ya viboko.
Jambo la kusikitisha zaidi ni kuwa, utolewaji wa adhabu hizo haufuati taratibu, kanuni pamoja na miongozo husika iliyowekwa.
Shabaha ya mzazi ama mlezi ni kumpatia fursa ya kimasomo mtoto wake na hivyo mwalimu hana budi kutimiza wajibu wake kwa uadilifu mkubwa wa kumpatia mwanafunzi elimu stahiki, malezi na miongozo yakinifu ili kumkuza na kumuendeleza kimwili, kimtaala na kitabia.
Mara nyingi kusudio la mwalimu ni katika kumjenga na kumrekebisha kwani ikumbukwe kuwa mwalimu ndiye mlezi wa mwanafunzi katika kipindi chote cha maisha yake awapo shuleni.
Inatazamiwa kuwa kila mwanafunzi anayeandikishwa shule atahudhuria masomo yake mpaka hapo atakapomaliza elimu yake katika ngazi aliyoandikishwa. Aidha, mwanafunzi awapo shuleni anatakiwa kufuata sheria zote za shule ili kumuwezesha kufuatilia masomo yake ipasavyo.
Hata hivyo, wapo baadhi ya wanafunzi ambao ni watovu wa nidhamu isivyo kawaida jambo ambalo hupelekea walimu kuwachukulia hatua za kinidhamu, ikiwa ni pamoja na kuwapa adhabu ya viboko.
Tunapenda kuwakumbusha wazazi, wanafunzi, walimu, washika dau pamoja na wananchi wote kuwa mnamo mwaka 2002, Serikali kupitia Wizara ya Elimu ilitoa Waraka wa Elimu (Na.24) kuhusu adhabu ya viboko ukielekeza utaratibu mahususi wa adhabu ya viboko.
Adhabu hiyo inaweza kutolewa endapo kutatokea utovu wa nidhamu uliokithiri ama kwa makosa ya jinai yaliyotendeka ndani ama nje ya shule yenye mwelekeo wa kuishushia shule heshima. Waraka huu pia unaongeza kuwa adhabu ya viboko itakayotolewa sharti izingatie ukubwa wa kosa, umri, jinsi na afya ya mtoto na isizidi viboko vinne kwa wakati mmoja.
Nani mwenye mamlaka ya kumuadhibu mwanafunzi kwa viboko? Waraka wa Elimu kuhusu adhabu ya viboko umeweka bayana kwa kumuidhinisha Mwalimu Mkuu wa shule husika ama mwalimu mwingine atakayepokea ridhaa ya uteuzi wa kimaandishi.
Utaratibu huo utafanyika kila wakati pindi ambapo kosa linalostahili adhabu ya viboko linapotendeka. Aidha, waraka huu unaonya kuwa mwanafunzi wa kike anapaswa kupewa adhabu ya viboko na mwalimu wa kike tu, uamuzi huo utatenguliwa endapo shule husika itamkosa mwalimu wa kike na si vinginevyo.
Waraka umeweka wazi kuwa kila mara adhabu ya viboko inapotolewa sharti iorodheshwe katika kitabu maalum kilichotengwa kwa kusudio la kujaza taarifa zihusuzo adhabu husika.
Kwa kuwa waraka unamtambua mwalimu mkuu kama mtu mwenye mamlaka ya kutoa adhabu ya viboko kwa mwanafunzi husika basi unamtaka pia atie saini yake katika kitabu hicho maalum kila adhabu ya viboko inapotolewa.