Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Wanawake wakigundua jambo hili, tumekwisha

13934 WANAWAKE++PIC TanzaniaWeb

Mon, 27 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tumezichezea sana akili za wanawake. Tulianza kwa kuwaambia kuwa sisi ni bora zaidi yao. Wakanywea, wakawa wadogo wakiamini hakuna kiumbe duniani chenye ‘manguvu’ na ‘maakili’ ya ajabu zaidi yetu. Wakatusujudia, wakatuona ni miungu watu, tena labda sio kutuona ni miungu mtu, bali mungu wa pili.

Na nguvu tuliyoitumia kuhakikisha hili linafanikiwa sio ndogo. Tumetumia vitabu vya dini, vinavyosomeka kwamba Mungu baada ya kuumba kila kitu, akatuumba sisi wanaume na kutupa uwezo wa juu ambao hata malaika hawakuwahi kuwa wao, yaani kama ingekuwa enzi hizi za kiteknolojia tungesema Mungu katengeneza mashine yenye programu toleo jipya.

Kisha vitabu vya dini vikasogea sentensi kadhaa mbele ndipo neno mwanamke likajitokeza, sentensi zikasomeka kwamba mwanamke akatokea ubavuni mwa mwanaume— yaani sawa na kusema bila mwanaume, kusingekuwa na mwanamke.

Ikaendelea mbele, ikaandikwa mwanamke akashawishiwa na shetani ili akamshawishi mwanaume wale tunda la mti wa kati na ikawa hivyo; hii ikamaanisha mwanamke alikuwa ni mdhaifu, tukaibeba na kuileta hadi leo mwaka 2018, na bado kuna wanawake kupitia sisi wanaamini wao ni wadhaifu.

Vitabu vikaendelea, vikaanza kuandika kuhusu mashujaa waliokuja kutetea ulimwengu, karibu asilimia 98 ya mashujaa wote walikuwa ni wanaume. Nuhu mwanaume, Musa mwanaume, Yesu (Isa bin Mariam) mwanaume, Yusufu mwanaume, Mohammad (S.A.W) mwanaume. Kisha asilimia kidogo tukawazungumzia wanawake, huku karibu asilimia 60 ya waliotajwa wakiwa ni wa upande mbaya.

Tukaweka vitabu vya dini pembeni, tukaja na historia. Tukawaambia kuhusu uhuru wa taifa kubwa kama Marekani, kisha tukawachorea michoro inayosema kuwa uliletwa ama kupiganiwa na wanaume kwa asilimia 98.

Uhuru wa Tanzania pia, wa Kenya, Uganda, Afrika Kusini na karibu wa kila taifa duniani ulipiganiwa na asilimia 98 ya wanaume. Kwa maana ya kwamba sisi ndiyo viumbe wenye nguvu au ni vipi?

Tukaja kwenye maendeleo ya dunia, tukasema kila kitu kilikigunduliwa na sisi wanaume. Gari, ndege, kompyuta, mashine ya kuchapisha gazeti, viatu hadi sufuria na vijiko — vyote ni sisi mwanaume. Kwamba kwa kipindi hicho wao wanawake walikuwa wanafanya shughuli gani?

Matokeo ya yote hayo leo hii wanawake wanahangaika kulazimisha kufanana na sisi— kitu ambacho sikiafiki kwa kiasi fulani. Kwa sababu kama unataka kupiga hatua, kama unataka kuwa bora zaidi, hutakiwi kupambana kuwa bora kwa kiasi sawa na aliye bora.

Unatakiwa kuhakikisha unakuwa bora zaidi ya aliyekuzidi ubora. Yaani kama wanawake wanataka kufanya mageuzi, wasihangaike kuwa kama sisi, au kuwa sawa na sisi, wahangaike kuwa bora zaidi ya sisi wanaume.

Tuwafundishe hili mabinti zetu, kuna mabadiliko italeta.

Columnist: mwananchi.co.tz