Aina hii ya kuchepuka huwa kwa wanaume na wanawake ingawa inaripotiwa zaidi kuonekana kwa wanaume. Hii ni kwa sababu ya ukweli kwamba mara nyingi wanaume wanaweza wakakwazika na bado wasifunguke kuelezea walivyokwazwa, lakini wakati huohuo wana kiu ya kulipiza kisasi kwa maumivu waliyoyapata tofauti na wanawake ambao wao kufunguka ni rahisi na ni kawaida kwao.
Mwanaume kwa kawaida anaweza kuamua kutoka nje ya ndoa kwa sababu tu amekasirishwa na kuona haheshimiwi katika mambo fulani kwenye uhusiano au familia. Kwa mfano akihisi hasikilizwi, hapewi kipaumbele, hahudumiwi, anachosema hakifuatwi, anavyotamani havifanywi basi kuna uwezekano mkubwa akaanzisha uhusiano pembeni kwa siri.
Tafiti za kisaikolojia zinasema kwamba mwanaume anapochepuka kwa msukumo wa hali kama hizi, ile hali ya kujihisi anafanya kosa inapungua au kupotea na kwa hivyo anaweza kujihesabia haki kwa kile anachokifanya.
Hii inaweza kumfanya aendelee kuchepuka kwa muda mrefu zaidi tofauti na mwanamke ambaye hata hali hii ikijitokeza wengi huwa wanajihisi kuhukumiwa na kujisikia vibaya mioyoni.
Kuchepuka kwa kulipiza kisasi hutokea pia nyakati ambazo mwanandoa mmoja anahisi kuwa mwenzake ana uhusiano nje, iwe kuna ushahidi au ni tetesi, wengine jambo hili humsukuma na yeye kufanya hivyohivyo ili kutafuta uwiano au ‘kusuuza’ nafsi.
Kwa bahati mbaya matokeo ya tabia hizi yamekuwa hasi zaidi na kwa wengi imesababisha kuharibu uhusiano na ndoa. Nashauri kwamba yanapotokea maumivu au makwazo ya aina yoyote yasihifadhiwe moyoni au kuonewa aibu kuzungumzwa maana visasi havilipi, bali huongeza maumivu na uharibifu zaidi.
Pamoja na kwamba uhusiano nje ya ndoa au kwa jina maarufu siku hizi kuchepuka ni tabia na mazoea ya mhusika lakini tusisahau kwamba zipo sababu ambazo ni zaidi ya tabia. Zipo nyakati ambazo tunashughulikia kesi za ushauri ambazo unaona wazi tabia ya mtu fulani si ya kujitakia au matamanio ya kawaida, lakini kuna udhihirisho wa nguvu inayomsukuma kufanya ngono.
Mtu anaweza kuwa hatamani au hapendi anachofanya, lakini atajikuta tayari ametumbukia kwenye ngono na baada ya kufanya tendo hilo anajuta ingawa bado kesho au keshokutwa atarudi kulekule.
Zipo koo au familia ambazo zina laana kwenye maeneo haya. Unakuta idadi kubwa ya wanaume au wanawake kwenye familia au ukoo fulani wana watoto nje ya ndoa, watoto waliopatikana kabla ya ndoa au watoto wanaopatikana nje ya ndoa lakini mtu akiwa ndani ya ndoa.
Hapa namaanisha mtu ana mke lakini tunasikia watoto wanaletwa au wanasemekana wamezaliwa na baba huyo. Kesi nyingi, na vikao vingi vya usuluhishi vinaketi vikijaribu kutafuta ufumbuzi wa tatizo. Labda mke anaweza kukimbia kwa kuchoshwa na akaolewa mwingine, lakini bado mume anaendelea kuleta watoto wa nje.
Iko mifano ya familia ambazo baba aliwahi kufahamika kuwa na tabia hizi za kuchepuka, na kwa bahati mbaya watoto wake wa kiume au hata wa kike nao wakaandamwa na roho ileile ya baba yao.
Yawezekana isiwe baba ikawa ni mama aliwahi kuwa na tabia hizi, alivyokuwa binti kabla ya kuolewa au hata akiwa na mume wake lakini kile kitu watu walichowahi kukiona kwa mama au baba sasa wanakiona kwa watoto wao.
Hili ni suala la kurithi, na pia laweza kuwa suala la roho inayotembea. Masuala ya namna hii ni magumu kidogo kuyaelewa maana yanaonekana kwa jinsi ya mwilini lakini nguvu yake si ya jinsi ya mwilini, na kwa hivyo uelewa wake unaweza kuchanganya kidogo lakini fahamu tu kwamba yako dhahiri zaidi ya uwazavyo. Kuyashughulikia kimwili, au kuyashughulikia kama vile chanzo ni tabia za kawaida ni ngumu kuleta suluhisho.
Mambo ya kiroho hayana budi kushughulikiwa kiroho. Na endapo kwenye ushauri tunakutana na kesi za namna hii tunamshauri mhusika au wahusika kulishughulikia jambo kiroho zaidi. Kwa bahati nzuri wahusika wanapoelewa na kuanza mchakato wa kiroho ufumbuzi huwa rahisi sana.
Mwisho niseme kwamba hali yeyote ya kutokuwa mwaminifu kwenye mahusiano yako ina nafasi kubwa sana kwenye kuleta uharibifu. Wako walioharibu ndoa zao na zikapasuka wakati bado walikuwa wanazipenda ziendelee kuwepo.
Japokuwa kuchepuka hufanywa kwa siri kubwa lakini mara nyingi siri hizi huwa ni za muda mfupi na kuna nyakati zinavuja au kuibuliwa na hapo ndipo machungu, majuto na machozi hutokea.
Inawezekana kabisa majuto na machozi yakakupa nafasi ya kujirekebisha na kuiboresha ndoa yako iliyopata nyufa baada ya kuchepuka lakini pia inawezekana kabisa ukajuta, ukalia sana na bado usiiokoe ndoa yako maana yamkini mwenzako hatokuwa tayari kuendelea na wewe.
Kama unaipenda ndoa yako basi utailinda, na mojawapo ya namna ya kuilinda ni kuwa mwaminifu.