Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

‘Wanaume hujadili zaidi matukio, wanawake huzungumzia watu’

44652 Pic+wanawake ‘Wanaume hujadili zaidi matukio, wanawake huzungumzia watu’

Tue, 5 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Bila shaka umeshawahi kusikia wanawake wakisutana, au wakijibizana kwa kutoa jambo moja upande huu na kulipeleka upande ule.

Ile hali ya kusutana ni tiba kwa wanawake. Kiasili wanawake wanapokutana hujijadili wao na kwao hiyo ni dawa.

Hivyo unapomuona mwanamke mbea, anasutwa, anajadili wenzake, ujue anatimiza wajibu wa asili yake.

Hali hiyo ni tofauti kwa wanaume ambao mara nyingi hujadili matukio ikiwamo mpira, wanawake waliokuwa nao usiku uliopita na namna ya kupata fedha, lakini hilo huwa tofauti kwa wanawake ambao muda mwingi hujijadili wao kwa wao.

Kwa mfano wanaume hawawezi kumjadili mwanaume mwenzao ni mzuri, lakini wanawake wanaweza kutumia dakika 10 hadi nusu saa kumsifia mwanamke mwenzao au kuwahesabu wanawake wenzao wazuri au wabaya.

Wanayojadili wanaume wakiwa pamoja

Mtaalamu wa saikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Andrew cha nchini Scotland, Profesa Frank Lorenz Müller anasema kuwa wanaume hujadili matukio zaidi ikiwamo michezo waipendayo, maeneo wanayokwenda kwa ajili ya starehe na wanawake.

Anasema ni nadra wanaume kujisifia wao kwa wao au kujadili kuhusu maisha yao hata kwa dakika moja. “Wao wapo tofauti, hujadili matukio zaidi (issues), na yanayotokea nje yao, hawajadili mambo yao binafsi, tabia zao binafsi wala vitu wanavyovifanya,” anasema Profesa Müller.

Anasema ni mara chache wanaume kujijadili wao kwa wao na ikitokea ni kwa sababu maalumu, jambo ambalo ni tofauti na wanawake.

Anafafanua kuwa wanawake wanatumia muda mwingi kujadili mambo yao ni sehemu ya kujiondolea mawazo maishani mwao.

“Ndiyo maana mwanamke akiwa na jambo halimuumizi sana kwa sababu wakikutana wawili au watatu wanaweza kupoteza siku nzima kulijadili.

“Lakini mwanaume anaweza kujadili na wenzake namna anavyoukubali mchezo fulani, akicheka na kufurahi, huku akiwa na jeraha moyoni ambalo hatalisema kwa yeyote na anaweza kuishi nalo hadi akafikwa na kifo, mwanamke hana tabia hiyo, ”anasema Profesa Müller.

Profesa Müller anasema kitaalamu ndiyo maana wanaume wanawahi kufa kuliko wanawake kwa sababu wao hukaa na mambo yao moyoni.

Hoja ya Profesa Müller inatofautiana na mtaalamu wa saikolojia kutoka Wizara ya Afya Dk Omari Ubuguyu anayesema kuwa binadamu yeyote huwaza kulingana na mazingira.

Anasema licha ya ukweli kuwa wanawake hupenda kujadili mambo yao, lakini wanaume hawajadili mambo ya aina moja badala yake hujadili kulingana na mazingira.

Anafafanua kuwa si rahisi mchunga ng’ombe huko maporini katikati anajadili kuhusu mchezo wowote achilia mbali mpira unaopendwa na wengi ilhali hata runinga hana, bila shaka atajadili kuhusu mifugo muda wote.

Dk Ubuguyu anasema nani anajadili nini inatokana na jamii anayoishi na hakuna tofauti ya kimtizamo kati ya wanawake na wanaume zaidi ya msukumo wa jamii wanazoishi.

“Hili suala la nani anajadili nini kati ya mwanamke na mwanaume limekaa kisosholojia zaidi badala ya kibailojia, hakuna tofauti ya kimawazo kati yao, zaidi inatokana na jamii wanazoishi.

“Tofauti yao ni kuwa wanawake wapo vizuri kwenye kujua lugha, mwanamke ni rahisi kujifunza lugha akajua haraka kuliko mwanaume, ilhali wanaume wataalamu zaidi kwenye hesabu na kuangalia yajayo, ”anasema Dk Ubuguyu.

Hata hivyo, kauli ya Dk Ubuguyu inakinzana na ya Jafari Kizugu anayeungana na Profesa Muller kwa kusema kuwa ni kweli wanawake wanaweza kujijadili wao kwa wao kutwa nzima na ndiyo maana wakikaa pamoja hawaishi kugombana.

Anasema “Sijawahi kuona wanawake wakae pamoja zaidi ya wawili na kusitokee mizozo ya kusemana semana, imekuwa hivi tangu enzi na enzi nahisi ndiyo asili yao, ”anasema Kizugu.

“Kuna nyumba niliwahi kuishi, wanawake wote walikuwa wanafanya kazi, wanatoka asubuhi na kurudi usiku, lakini cha ajabu hata hao walikuwa wanagombana wakilaumiana na kusemana vibaya, hii ilinithibitishia kuwa wanapokuwa wanawake mahali lazima wamjadili mmoja wao au wao kwa wao, ” anasema.

Anasema wanaume mara nyingi badala ya kubishana hutafuta suluhisho haraka inapotokea hali kama hiyo na yakiisha yamekwisha na hata wakikutana hawatajadili masuala hayo tena.

Kwa upande wake Marygoreth Athanas anasema kuwa hawezi kukaa na jambo moyoni na ndiyo maana ana furaha muda wote.

Anasema akiwa na jambo linamkera au kumfurahisha lazima atamueleza mtu aliyekuwa karibu naye na haoni kama kuna tatizo kufanya hivyo.

“Nakubali kusutana kupo, lakini inategemea unamwambia au kuzungumza na mtu wa aina gani, mimi marafiki zangu ni watu wanaojiheshimu na ikitokea tukapishana maneno tunaeleweshana na maisha yanaendelea hakuna anayeapa kutozungumza na mwenzake kwa sababu haiwezekani kukaa bila kubadilishana mawazo,” anasema Marygoreth.

Dawson McAllister ambaye ni mtaalamu wa saikolojia kutoka mtandao wa The Hope Line, anasema mwanamke anaweza kulia, kuonyesha mifano, kuonyesha hisia kwa mwanamke mwenzake anapokuwa na jambo hata kama hawajuani.

“Wanaume hujadili hisia zao ndani kwa ndani, mara nyingi hawajui wanataka nini wanapokuwa na jambo, matokeo yake hujaribu kufanya wenyewe jambo wanaloona linawatatiza badala ya kushirikisha wenzao kama wafanyavyo wanawake,” anasema.

Anasema inaweza kumchukua mwanamke mmoja dakika tano kumfahamu mwenzake, kazaliwa wapi, ana watoto wangapi, amesoma hadi hatua gani na ana shida gani kwenye familia yake na uhusiano wake.

Mtaalamu wa saikolojia kutoka Dar es Salaam, Josephine Tesha anasema kuwa wanawake wanavyojadili mambo yao wao kwa wao ni dawa.

Anasema kisaikolojia ipo hivyo na inawasaidia kuondoa msongo wa mawazo na inarahisisha mawasiliano kati yao.

“Wanaume hawajaumbwa hivyo, wao hujadili matukio na si rahisi kujadili mambo yao kama wanawake, ”anasema Tesha.

Anafafanua zaidi, “Wanawake wanapojijadili wao kwa wao hujifunza vitu vipya, ndiyo maana wanawake wanajua vitu vingi vya jamii zinazowazunguka, ni tofauti na wanaume.”



Columnist: mwananchi.co.tz