Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Wanaowalinganisha Bobi Wine, Lissu wanakosea?

Wed, 3 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanamuziki wa Pop wa Uganda aliyegeuka mwanasiasa, Robert Kyagulanyi ‘Bobi Wine’, kama utani amegeuka nyota wa siasa za Afrika Mashariki. Tukio lake la kukamatwa, kuteswa na kufunguliwa mashtaka limevuma na kuvuta hisia za vyombo vya habari vikubwa duniani.

Jinsi Bobi Wine alivyohojiwa na taasisi kubwa za habari, kisha mahojiano hayo kuruka kwenye televisheni, redio na mitandaoni, haiachi swali kwamba dunia inajua kile ambacho kinaendelea Uganda. Bahati nzuri Bobi Wine amekuwa jasiri na mwenye uthubutu mkubwa, hivyo hakuogopa kuzungumza kila alichonacho.

Bobi Wine ni mwanasiasa mchanga ambaye aina ya siasa zake zinawavutia zaidi vijana na Waganda wenye kuhitaji matumaini mapya. Ni mbunge kwa mwaka mmoja na miezi miwili tu sasa, kwani alichaguliwa kuwakilisha Manispaa ya Kyadondo Mashariki katika uchaguzi mdogo uliofanyika Juni 29 na kuapishwa Julai 11, mwaka jana.

Bobi Wine ni mbunge huru, yaani aligombea na kushinda bila chama. Na hakuna mwenye uthubutu wa kupinga ukweli kuwa tangu kuingia kwake bungeni, amekuwa mwiba kwa chama tawala, NRM na chama kikuu cha upinzani, FDC. Alianza kwa ushindi wake alipovigalagaza vyama hivyo.

Baada ya hapo, kila unapofanyika uchaguzi mdogo, Bobi amekuwa akipanda jukwaani kuwafanyia kampeni wagombea binafsi na kushinda uchaguzi. Matokeo ya karibuni zaidi ni Manispaa ya Arua, alimuunga mkono Kassiano Wadri, aliyekuwa mgombea binafsi na kumwezesha kushinda.

Uchaguzi wa Arua ndiyo uliosababisha Uganda itazamwe zaidi duniani, kwani Rais Yoweri Museveni alikwenda kwenye manispaa hiyo kumfanyia kampeni, mgombea wa NRM, Nusura Tiperu, lakini alishindwa. Museveni akiwa Arua, inadaiwa alizomewa na msafara wake ulipigwa mawe na wafuasi waliokuwa wakiimba “Bobi Wine Rais”.

Hicho ndicho kikawa chanzo cha Bobi, Wadri, wabunge wengine binafsi kukamatwa kwa tuhuma za kumfanyia fujo Rais Museveni na kumrushia mawe. Bobi alifunguliwa mashtaka ya kumiliki silaha za moto kinyume na sheria pamoja na uhaini. Kesi ya umiliki wa silaha za moto ilifutwa, ya uhaini na kumrushia mawe Rais zinaendelea.

Ni kweli kuwa Uganda hali ni ya wasiwasi mkubwa na Bobi anaibuka na kuonekana shujaa kwa sababu anapaza sauti katikati ya wasiwasi. Hata hivyo, ukipima jicho la dunia kwa Uganda na Bobi, unastaajabu kuona linazidi lile lenye kumtazama mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu na shambulio lake la risasi.

Lissu alipigwa risasi nyingi Septemba 7, mwaka jana, katika shambulio lisilopingika kwamba malengo ya waliomshambulia yalikuwa kumuua. Utata wa mazingira ya shambulio lake na kuvuma kwa jamii ya watu mithili ya mazimwi, inayoitwa “watu wasiojulikana”, ni mambo yaliyopaswa kumvuta Lissu na vyombo vingi vya habari vya kimataifa.

Kwa mwenye uelewa wa mambo, anafahamu kwamba si Bobi aliyekuwa akipiga simu na kuomba mahojiano na Al-Jazeera, VOA, BBC, CNN na kadhalika. Ni rahisi kutambua kuwa kulikuwa na watu waliokuwa wakifanya kazi kubwa ili kumkutanisha Bobi na vyombo vikubwa vya habari duniani ili ulimwengu ujue mengi ya Uganda kupitia kinywa cha mwanasiasa huyo kijana.

Kwanza alikuwa anaumwa na ilielezwa kwamba alienda Marekani kwa matibabu. Hata hivyo, kazi aliyofanya ya kuujuza ulimwengu kuhusu Uganda, inatosha kuonesha kuwa hata safari yake Marekani pengine ulikuwa mkakati wa kuhakikisha anakutana na jumuiya ya habari za kimataifa na kutema nyongo aliyonayo kuhusu Uganda, siasa, haki, sheria na utawala bora.

Nafasi ya Chadema na Lissu

Waganda walikuwa na agenda yao kuhusu utawala wa Rais Museveni na wakaona Bobi kwa vile misukosuko aliyoipata ilivuta hisia za ndani na nje ya nchi, ingekuwa rahisi kumtumia kufikisha kile walichokikusudia. Na utaona kwamba mafanikio yao ni makubwa.

Lissu alihamishiwa Nairobi, Kenya kwa matibabu kutoka Hospitali ya Mkoa wa Dodoma usiku wa Septemba 7, mwaka jana. Januari mwaka huu, alipohamishiwa Brussels, Ubelgiji kwa matibabu zaidi, alikuwa anaweza kuzungumza. Ikumbukwe kuwa Lissu aliwahi ‘kulihutubia taifa’ akiwa Hospitali ya Nairobi.

Hapa ni kufikisha ujumbe kwamba alikwenda Ubelgiji akiwa na ufahamu wa kutosha na uwezo wake wa kuzungumza ulikuwa mzuri. Tangu akiwa Hospitali ya Nairobi, Lissu alithibitisha kuwa ufahamu wake ulikuwa timamu na mdomo haukuwa na shida yoyote. Kwa hiyo kukutana na waandishi wa habari na kuzungumza lilikuwa jambo lenye kuwezekana.

Tangu alipofika Brussels ni zaidi ya miezi nane. Kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kuratibu mahojiano na vyombo vya habari vya kimataifa. Ni kweli amekwenda kwa ajili ya matibabu, lakini haishindikani kuandaliwa mikutano na vyombo vya habari ili azungumze na dunia.

Kwa uzito wa matukio, aliyoyapata Bobi ni madogo mno ukilinganisha na yaliyomfika Lissu. Risasi nyingi zilielekezwa kwake na kupenya mwilini, leo hii Mungu amemponya. Anatakiwa apate nafasi pana aujuze ulimwengu kuhusu shambulio lake na uwepo wa watu wasiojulikana.

Ukipima daraja la kisiasa, Bobi ni mwanasiasa mchanga mno. Lissu ni wa kiwango cha juu. Alikuwa Rais wa Jumuiya ya Sheria Tanganyika (TLS), kipindi aliposhambuliwa. Ni mwanasheria na mwanaharakati wa muda mrefu. Ni mbunge kwa muhula wa pili. Unaweza vipi kumlinganisha Lissu na Bobi?

Kuhusu mahabusu, inawezekana kipindi hiki akiendelea kutibiwa ndiyo amepumzika mwaka mzima bila kulala mahabusu. Vinginevyo, yalikuwa ni maisha yake. Alikamatwa na kuwekwa korokoroni, alipoachiwa alizungumza tena. Alifunguliwa mashitaka na kushikiliwa na polisi, alipofika mahakamani alitumia ujuzi wake wa sheria kupata dhamana.

Lissu pia ni Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa muhula wa pili sasa. Zaidi ni Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria. Vyeo vyote hivyo vinathibitisha ukuu wa Lissu kwenye siasa. Ni kiongozi wa kiwango cha juu. Hivyo, shambulio la risasi dhidi yake halipaswi kuitetemesha Tanzania peke yake, bali dunia nzima.

Inafahamika kuwa Lissu anaumwa, kwa hiyo hawezi kuratibu mawasiliano na jumuiya ya habari za kimataifa yeye mwenyewe. Badala yake inatakiwa kuwe na watu wa kuifanya hiyo kazi. Uongozi wa Chadema ulipaswa kulishughulikia hili. Kinyume chake, pengine wamemwachia Lissu mwenyewe. Hawezi!

Matokeo yake, wakati Bobi alipofanya mahojiano na Al-Jazeera, CNN, VOA na BBC, Lissu alikuwa akisomwa mitandaoni kuhusu andiko lake alilomkosoa Waziri wa Sheria na Katiba, Pamagamba Kabudi kuhusu kauli yake kwamba hata maraisi wa Marekani walipigwa risasi na kuuawa na wauaji hawakukamatwa.

Ni kweli, Kabudi hakusema kweli katika mkutano wa diaspora Marekani kuhusu marais wa Marekani waliouawa kwa risasi. Anzia Abraham Lincoln mwaka 1865, James Garfield (1881), William McKinley (1901) hadi John Kennedy (1963), wote hao waliowapiga risasi walikamatwa, kuuawa papo hapo au kuhukumiwa kifo.

Sikosoi Lissu kuandika ufafanuzi huo wenye kumrudi Kabudi, ukizingatia hoja husika ilimhusu yeye, maana alishambuliwa kwa risasi na wahusika mpaka leo hawajapatikana na hakuna hata fununu ya kupatikana kwao. Hoja ni kwa nini awe wa kuishia kuandika mitandaoni wakati anaweza kutoa sauti na ikavuma kimataifa?

Columnist: mwananchi.co.tz