Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Wanafunzi wafahamishwe kuwa siasa ni ajira

14324 Joseph+Chikaka TanzaniaWeb

Tue, 28 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Pamoja na ukweli kuwa siasa hujumuisha mfumo wa maisha ya jamii husika, lakini bado kuna ugumu wa kupata tafsiri ya moja kwa moja.

Hata hivyo, ni vema watu wakatambua kuwa mifumo mbalimbali ya maisha ya kila siku haiwezi kutenganishwa na siasa.

Neno siasa linaweza kuwa na tafsiri nyingi, mojawapo ni ni njia ya kufanya maamuzi katika jamii, taifa au dunia nzima. Sehemu muhimu ya siasa ni majadiliano kati ya watu mbalimbali wenye nguvu au mamlaka.

Pia, siasa ni mfumo wa utekelezaji wote wa mkataba kati ya watawala na watawaliwa. Na, msingi huo wa utawala huanzia katika katiba na demokrasia ambayo ni serikali ya watu, iliyochaguliwa na watu, inayoongozwa na watu kwa manufaa ya watu.

Mwanafalsafa Aristotle, anaeleza kuwa siasa ni shughuli ya kimaadili inayohusiana na ujengaji wa jamii bora yenye usawa.

Jamii hiyo huundwa na binadamu, na kuwa binadamu huyo ni mnyama wa kisiasa anayeishi kwenye jamii ya kisiasa; hivyo, kila kitu ni siasa.

Siasa ni sayansi na taaluma

Siasa ni somo ambapo watu hujifunza elimu ya Sayansi ya Siasa kama ilivyo kwa masomo mengine. Sayansi ya siasa huchambua mifumo mbalimbali ya utawala na serikali duniani na namna ya kubadili upepo wa kisiasa pale mambo yanapokuwa ‘tete’.

Siasa kama sayansi na taaluma hutumia njia, mbinu na mikakati ya kisayansi na kuendeshwa kulingana na utafiti unaozingatia njia na matokeo ya kisayansi. Matokeo yanayopatikana, hufanyiwa kazi kupitia ilani mbalimbali za vyama ambazo kimsingi hupaswa kuakisi mipango mikakati ya nchi husika kwa muda mfupi na mrefu.

Hivyo, vyama vya siasa hupaswa kushindanishwa katika uwezo wao wa kuweza kutekeleza vizuri kimkakati yale malengo au dira ya maendeleo ya nchi kwa kipindi fulani cha utawala.

Siasa ni taaluma na siyo porojo. Wapo watu wanaodhani kuwa kila mpango usiotekelezeka ni zao la siasa.

Kwa mfano, mara nyingi tumeshuhudia watu wakisema kuwa “ah, hizo ni siasa tu”. Wakimaanisha kwamba siasa ni kitu ambacho hakina utekelezaji. Hiyo si tafsiri sahihi ya sayansi ya siasa kama taaluma.

Siasa kama sanaa

Siasa huwa sanaa kwa namna wanasiasa wanavyoweza kucheza na kujibadilisha kulingana na miktadha. Leo huweza kuimba wimbo huo mzuri na kesho wimbo huo huo huchuja na kuja na sera nyingine shawishi.

Mahitaji ya jamii ya jana na kesho huweza kutofautiana hivyo ni wazi wanasiasa ‘manguli’ huwa na uwezo wa kucheza na nyakati zote hizo kwa maslahi yao ya kisiasa (mara chache kwa maslahi ya jamii).

Ni vema wanafunzi na vijana wetu wakafahamu kuwa mwanasiasa yeyote huanza na maslahi yake ya kisiasa. Kwa sababu asipoweza kutetea maslahi yake ya kisiasa atawezaje kumtetea mtu mwingine?

Hivyo, siasa kama sanaa ni kama mchezo. Kila mchezo una kanuni zake. Kwa mfano, mara nyingi jamii imekuwa ikiwashangaa baadhi ya wataalamu ambao ni bobezi katika kada zao pale wanapoanza kufanya siasa na kuweka usomi wao pembeni.

Kanuni za mchezo huo huwalazimisha wacheze hivyo kwa maslahi yao, kinyume na hivyo hushindwa siasa.

Wakati mwingine mwanasiasa mbobezi mwenye shahada ya uzamili au uzamivu hupaswa kufikiri na kutenda kama vile mtu asiyeenda shule au aliye na ufahamu wa darasa la saba, alimradi tu analinda maslahi ya kisiasa.

Ni vema wanafunzi wetu wakajifunza kuwa siasa ni kama sanaa lakini usanii huo unaweza kuhusishwa na nguvu za dola. Hilo linashadadiwa na mwanazuoni Okwudiba Nnoli katika maandiko aliyokusanya kuwa siasa hujumuisha mchakato unaohusisha uchukuaji wa madaraka yaani nguvu ya dola.

Sanaa hiyo ya kutumia madaraka au nguvu ya dola kwa maslahi ya umma hutafsiriwa kuwa siasa safi na yenye maana kwa jamii.

Siasa ni ajira, amani na uchumi

Siasa ni ajira safi yenye ujira mzuri kama zilivyo ajira nyingine zinazolipa vema. Kama siasa ni ajira, basi lazima kutakuwapo dhana ya mwajiri na mwajiriwa. Nchini, bado wananchi hawajatumia uwezo wao wa kuwaajiri wanasiasa.

Hii ni kwa sababu ya mifumo ambayo huonyesha kuwa mwajiri wa wanasiasa ni vyama vyao vya siasa. Hivi huwa na uwezo wa kumsajili au kumfuta uanachama mtu.

Kwa kuwa ni ajira basi inapaswa kutoa fursa ya amani. Pasipo amani baadhi ya ajira hufa. Siasa si chuki wala ugomvi au uhasama. Siasa inapaswa kuchochea matumaini, upendo na heshima kwa binadamu.

Siasa na uchumi ni vitu visivyopishana. Mwanazuoni Harold Lasswell anaeleza kuwa siasa inaingia katika uchumi kwa maana ya kuwapo kwa mgawanyo wa rasilimali katika jamii.

Ili mgawanyo huo wa rasilimali uweze kutokea, lazima mgawaji wake awe mwenye madaraka akimaanisha mwenye nguvu za dola.

Makala haya yatukumbushe kuwa siasa safi ndiyo msingi wa jamii na taifa bora. Pia, siasa haiwezi kutenganishwa na mifumo na shabaha ya elimu ya jamii. Kwa sababu hiyo, hatuna budi kwa pamoja kuwafundisha watoto, vijana, wanafunzi kuwa siasa ni mojawapo ya ajira.

Nao ni vema wakaondokana na dhana kuwa siasa ni mchezo mchafu ambao husababisha wanasiasa hasa kutoka bara la Afrika kuonekana kuwa ni waongo, wezi, wauaji na wenye uchu wa madaraka.

Columnist: mwananchi.co.tz