Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Wahuni waliomuita Ruge ‘Scofield’ hawakukosea sana

44154 Edo+Kumwembe Wahuni waliomuita Ruge ‘Scofield’ hawakukosea sana

Thu, 28 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Amevuta pumzi zake za mwisho juzi hapa Johannesburg. Ruge Mutahaba. Ni nadra kwa mtu wa cheo chake, ndani ya taasisi kama Clouds akapamba kurasa za mbele za magazeti nchini. Hizo ni nafasi za waheshimiwa wanapotutoka.

Ndiyo, alikuwa maarufu, lakini umaarufu wake ulikujaje? Sababu ni moja tu. Akili zake! Hakuwa mheshimiwa lakini alitumia akili kufanya mambo mengi. La kwanza ni kuiweka Clouds FM ilipo. Redio inayosikilizwa zaidi nchini. Yeye na mtu anayeitwa Joseph Kusaga ndizo akili kubwa zilizoiweka Clouds ilipo sasa. Kuna wanaosema katika hili, Ruge alihusika zaidi.

Ruge hakuwa mtu wa mayowe kama wanasiasa wetu au sisi tulio katika michezo. Alikuwa mjanja, anatazama mbali, anafanya kitu akiwa nyuma nyuma, baadae kinapofika mbele ndipo wajanja wengine wanagundua nyuma yake kuna Ruge. Ungesikia wanasema ‘Ruge huyo’ au ‘mambo ya Ruge hayo’.

Lawama na sifa zote kuhusu Clouds FM zilimuangukia yeye. Kisa? Wajanja wengine waling’amua kuwa Ruge ndio akili ya Clouds. Kuna wahuni nawafahamu, kina MwanaFA na rafiki zangu wengine wakaamua kumpachika jina la Michael ‘Scofield’.

Scofield ni mcheza filamu wa Marekani aliyecheza movie maarufu ya Prison Break. Alikuwa anatumia akili nyingi za ajabu kuhakikisha mambo yanakwenda. Ndivyo hawa wahuni wakamfananisha na Ruge. Hawakukosea sana.

Baadaye mwenyewe aligundua kwamba alikuwa amepachikwa jina hilo. Hakuwa na neno. Amemaliza pumzi zake za mwisho jijini Johannesburg huku akili yake kubwa ikiwa ni kuwarithisha ujanja vijana wenzake. Akaliweka neno fursa katika mtazamo mwingine. Yote hii ilikuwa ni kujaribu kuwaambia vijana kwamba kuna nafasi tofauti za kuyashinda maisha.

Akili zake zilikuwa tofauti kidogo. Namkumbuka kwa kukaa nyuma katika dili nyingi bila ya kelele. Tunaishi katika zama ambazo viongozi wetu wanapenda sana kuonekana kwamba wao ndio wanafanya mambo makubwa. Ni tofauti na watu wanaojigamba kila kukicha ‘mimi ndiyo kila kitu..’ ‘unanijua mimi? Mimi ndiye ambaye..’

Mungu ampumzishe panapostahili ‘Bwana Scofield’. Ruge Mutahaba. Mtu fulani hivi mwenye akili nyingi ambaye kitu kilichomuweza ni kifo tu sio mambo mengine.



Columnist: mwananchi.co.tz