Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Wabunge wetu na bajeti ya “jicho la huruma”, tutafika?

Thu, 21 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Bunge la Bajeti linaelekea mwisho. Tumesikia mengi na kujifunza mengi. Tumewasikia wabunge wetu, wengine wakiunga mkono, wengine wakipinga, wakishauri, wakisinzia na wengine wakikwepa vikao vya Bunge. Asilimia kubwa ya wabunge wetu tumewasikia wakiishukuru serikali kwamba miradi ya maji, kilimo, barabara, hospitali, shule na mingine, imetekelezwa kwa vile serikali imekuwa na “jicho la huruma”.

Tumewasikia baadhi ya wabunge wanajigamba kujenga zahanati, shule, barabara katika majimbo yao. Wengine wananunua madawati, vitanda vya hospitali na kutengeneza visima vya maji na kulipa ada za wanafunzi katika majimbo yao. Kwa maneno mengine nao wanayaangalia majimbo yao kwa “jicho la huruma”.

Ugonjwa huu wa “kuangaliwa kwa jicho la huruma” umeenea na kusambaa kila kona ya taifa letu. Hata juzi wakati bajeti ya mwaka huu ikisomwa, wananchi walikuwa wakiisubiri hotuba ya Bajeti ije na “jicho la huruma”.

Ugonjwa huu ni mbaya kiasi kwamba hata nguvu za kuhoji zimepotea na kuyeyuka. Tunaambiwa bajeti iliyopita haikutekelezwa asilimia zote, na kusema kweli sehemu nyingine kilichopangwa na kupelekwa huko havina uwiano hata kidogo.

Tumewaona wachache wanaohoji ni kwa nini kila mwaka malengo hafikiwi. Walio wengi hawahoji. Je, bajeti ya mwaka huu itafikia malengo au hapana? Kuna mbinu gani za kuhakikisha bajeti inatekelezwa asilimia zote? Badala ya kuuliza maswali haya ya msingi, tunakaa na kusubiri kwa matumaini yasiyokuwa na matumaini na kubembeleza “jicho la huruma” lielekee upande wetu.

Serikali inayokusanya kodi, serikali iliyopata dhamana ya kuitawala na kuiongoza nchi, badala ya kutimiza wajibu wake, inakuwa na “jicho la huruma”! Inalazimika kumpendelea mbunge mmojammoja na kulisaidia jimbo lake kulingana na jinsi anavyowasilisha kilio chake; kwa kupiga magoti na kutoa machozi.

Tumesikia mara nyingi waheshimiwa wabunge wakisema “Mheshimiwa Waziri… Napiga magoti mbele yako, naomba unitupie jicho la huruma kwenye jimbo langu, shule, hospitali na barabara”.

Hayo yakitendeka, mbunge anaishukuru serikali kwa “jicho la huruma”. Na wananchi wanamsifu mbunge wao kwa kuwaletea barabara, maji na umeme, wakati vyote hivyo vinatokana na kodi za wananchi na rasilimali za taifa letu.

Kwa nini mbunge asisimame kifua mbele na kuikumbusha serikali wajibu wake wa kutoa huduma? Akatetea kwa nguvu zake zote haki ambayo ni lazima wananchi wake waipate bila masharti wala upendeleo wa aina yoyote ile.

Mbunge ni macho na midomo ya wananchi anaowawakilisha. Hili ni muhimu sana likaleweka kwa wote; wabunge walifahamu na wananchi wanaowakilishwa walifahamu kwa undani kabisa.

Kazi za mbunge

Swali langu la msingi katika makala hii ni je, sisi Watanzania tunafahamu kazi za wabunge? Na je, wabunge wetu wanafahamu kazi zao na wajibu wao? Tunaweza kuzifahamu kazi za mbunge, kwa kuangalia kazi za Bunge, maana mbunge, ni mwakilishi wa jimbo (wananchi) katika Bunge.

“Sehemu ya pili ya Bunge itakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Katiba hii.” Ibara ya 63(2), pia na Ibara ya 64(1) inaelezea kazi za Bunge, juu ya kutunga sheria.

Hivyo basi, mbunge, ni mwakilishi wa jimbo lake katika chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kina madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake.

Iwapo kazi ya mbunge ni kuisimamia na kuishauri serikali, kwa nini mbunge alie, aipigie magoti serikali na kuishukuru kwa kazi inazopaswa kufanya?

Inawezekana pia kwamba hata wananchi wanafikiri kwamba kazi za mbunge ni kujenga madaraja, ni kuleta maji, ni kuleta umeme, ni kusalimia misiba na kujenga shule.

Kama hivyo ndivyo, ndio maana wale wanaohimiza elimu ya uraia si wa kupuuzwa. Ni lazima serikali isikie kiliko hiki na kuweka nguvu zote katika kufundisha elimu ya uraia.

Fikra za mbunge

Wakati wa uchaguzi mkuu wa 2010, nilibahatika kupata kipeperushi cha mbunge wa sehemu fulani kilichokuwa kikimnadi na kuelezea misaada mbalimbali aliyoitoa kwa wanajimbo wake.

Anasema: “Nilisaidia upatikanaji wa majeneza pamoja na kusafirisha marehemu kutoka wilaya yangu walikopata ajali ya treni mkoani Dodoma na kushughulikia majeruhi kwa kuwawahisha hospitali ili kupata matibabu ya haraka.

“Nilifanikisha uletaji wa mwili wa marehemu (anamtaja jina) kutoka Dar es Salaam. Nilisaidia sana uwezekano wa usafiri wa ndege pamoja na usafiri wa gari wa kutoka uwanja wa ndege kwenda alikozikwa.

“Nilitoa baiskeli kwa mlemavu wa viungo yenye thamani ya Sh60,000 na Sh100,000 kumnunulia mlemavu mwingine baiskeli ya gurudumu tatu.

“Nilimsaidia mama mtu mzima kupata haki zake zilizokuwa hatarini kupotea bure mkoani Dodoma

ee(Sh40,000) nauli ya kutoka Dar es Salaam waliokuwa wamekwama.

“Niliwasafirisha vijana wawili kutoka jimboni mwangu waliokwama Dar baada ya kudanganywa waende huko kwamba wangepatiwa ajira.

“Nilitoa ada ya mtoto wa mzee wa mahakama ya Mwanzo aliyekuwa akisoma sekondari ya kata.

“Tarehe 24/6/09 milihudhuria mazishi ya Mzee mmoja (anamtaja) aliyezikwa huko Mtana na kuchangia Sh100,000 kama rambirambi.

“Nilisafirisha maiti ya mkereketwa wa CCM (anamtaja) aliyefariki Julai 2009 huko Mbeya na kuzikwa kijijini kwao Mtakuja. Pamoja na gharama nyingi nilizolipia, pia nilichangia Sh50,000 kama rambirambi.

“Nilisaidia mkazi wa kitongoji fulani (anamjata) msaada wa fedha kufuatia kuunguliwa moto nyumba yake.

“Nina hakika nimetoa michango mingine mingi kwa wanajimbo na kwa watu wengine pia ambao hawatoki jimboni mwangu. Nyinyi ndiyo mtanikumbusha mengine niliyoyasahau.”

Mbunge hajafanya kazi yake

Ningepata nafasi ya kumkumbusha ndugu yetu huyu ni kwamba kati ya yote aliyoyataja hakuna hata moja linalohusiana na kazi yake ya ubunge. Labda alitaka kujitangaza kwamba yeye ni raia mwema, hivyo anafaa kuchaguliwa kuwa mbunge. Hata hivyo, bado ana kazi ya kujifunza na kuzifahamu kazi za mbunge.

Wabunge wengine wanafanya kazi ya kugawa fedha kwa wapiga kura wao ili wawatambue kwamba wao ni wabunge.

Mimi mwenyewe kwa macho yangu, si kuambiwa, mwaka fulani kabla ya kura za maoni za CCM nilimwona mbunge wa jimbo fulani, akiwatupia wapiga kura wake pesa.

Akiwa na gari lake na kipaza sauti chake mkononi, aliwataka wananchi wamtambue kwamba yeye ni mbunge wao, na kwamba yeye ana pesa. Hivyo alitoa pesa kwenye mkoba wake na kuwatupia wananchi.

Watu walikanyagana na kuumizana wakigombea pesa hizo. Kila mtu alishangaa huyo mtu alikuwa na pesa kiasi gani. Hata matajiri kama Bill Gate wa Marekani, hawajafikia kiasi cha kuwatupia watu pesa, sembuse mbunge, tena wa nchi masikini kama Tanzania.

Hili ni tukio lililofanywa na mtu mwenye akili timamu, tena mbunge.

Mbunge anaweza kuishauri serikali kujenga shule, lakini si kazi ya mbunge kujenga shule kwa pesa zake binafsi, akifanya hivyo, itakuwa si kwa vile ni mbunge, bali ni kwa vile atakuwa raia mwema mwenye uwezo na roho ya kuwasaidia wananchi wenzake.

Mbunge anaweza kutoa sukari kama vile wananchi wenye nia njema na uwezo wanavyofanya, lakini si kwamba ni kazi ya mbunge, kugawa sukari, kana kwamba asipotoa sukari au vitenge atakuwa hakufanya kazi yake ya ubunge.

Hata hivyo, si lazima kila raia mwema kuingia bungeni. Raia wema, ambao tunao wengi, wanaweza kuendelea na kazi yao ya kuihudumia jamii kwa matendo yao mema.

Wanasiasa wenye uwezo wa kujieleza na kueleza kile walichotumwa na wananchi, wenye uwezo wa kuchambua na kuiweka sawa miswada mbalimbali inayowasilishwa bungeni, wasomi, wazalendo na wenye moyo wa kukubali kutumwa, wapewe nafasi ya kuwatumikia wananchi bungeni.

Padre Privatus Karugendo,

+255 754 6331 22

[email protected]

Columnist: mwananchi.co.tz