Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Wabunge wengi washindwa uchaguzi 1985, alikuwemo John Malecela

102124 Pic+uchaguzi Wabunge wengi washindwa uchaguzi 1985, alikuwemo John Malecela

Sat, 11 Apr 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Baada ya kucheleweshwa kwa muda wa wiki moja kutokana na uhaba wa mafuta ya petroli uliolikabili Taifamwaka 1985, kampeni za wagombea ubunge katika majimbo 169 ya uchaguzi zilianza nchi nzima.

Hata hivyo, uchaguzi ulifanyika katika majimbo 164 tu kutokana na wagombea wa majimbo matano kupita bila kupingwa.

Jumapili Oktoba 27, 1985 ilikuwa siku ya kupiga kura. Rais wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere akifuatana na mkewe, Maria, walipiga kura tawi la Mikoroshoni, Kata ya Msasani wilayani Kinondoni saa 4:00 asubuhi.

Makamu mwenyekiti wa CCM, Ali Hassan Mwinyi, aliyekuwa mgombea pekee wa urais wa Jamhuri ya Muungano, alipiga kura katika kituo cha Shule ya Sekondari ya Lumumba mjini Zanzibar ambako Idris Abdul Wakil, alitumia kituo cha Kikwajuni Juu. Katibu mkuu wa CCM, Rashidi Kawawa alikuwa Jimbo la Liwale.

Kutokana na wingi wa vituo vya kupigia kura, misururu ya wapiga kura kwa mwaka 1985 ilikuwa mifupi kuliko wakati wa chaguzi nyingine zilizotangulia. Kila kituo kilikuwa kinahudumia wapigakura kati ya 350 na 400. Katika nchi nzima kulikuwa na vituo 30,000 vilivyotakiwa kuhudumia wapigakura milioni 6.9 waliojiandikisha.

Baada ya matokeo kutangazwa, ilibainika kuwa wabunge wengi wa Bunge lililopita walishindwa, wakati mawaziri karibu wote waliogombea ubunge walishinda.

Pia Soma

Advertisement
Matokeo ya uchaguzi wa 1985 yalikaribia kushabihiana na yale ya mwaka 1980. Karibu mawaziri wote walishinda, isipokuwa mmoja-- Ole Saibul-- aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, na Naibu Waziri mmoja-- Nizar Nyoni-- ambaye alikuwa Wizara ya Elimu.

Kama ilivyokuwa kwa Ole Saibul katika uchaguzi wa 1980, ndivyo ilivyokuwa John Malecela katika uchaguzi wa 1985. Malecela, ambaye alikuwa waziri wa muda mrefu, aligombea ubunge Jimbo la Chilonwa mkoani Dodoma lakini alishindwa uchaguzi. Malecela ambaye alikuwa Waziri wa Mawasiliano na Ujenzi katika Serikali ya Mwalimu Nyerere, ndiye waziri pekee aliyepoteza kiti chake cha ubunge katika uchaguzi huo.

Hata hivyo, zaidi ya nusu ya wabunge wa kuchaguliwa walikuwa wapya.

Miongoni mwa wabunge wa walioshindwa kutetea nafasi zao ni Nganga Kipuyo (Arusha), Salustian Deengw (Mbulu), Joseph Lemomo (Monduli), Aaron Mpamjije (Kasulu), Martha Weja (Ilala), Patrick Nwila (Mbeya Vijijini), Steven Yilanga (Mbeya Mjini) na Sylvia Kate Kamba (Masasi).

Wengine walioshindwa ni Said Katapala (Mtwara Vijijini), Jalala Kilewa (Kibaha), Bakari Gwaya (Tunduru), Simon Mwaliko (Manyoni), Joseph Monko (Singida Vijijini), Padri Paulo Misigalo (Tabora Mjini, Tobi Mweri (Pangani), Thomas Bwire (Bunda), Balozi Maggid (Tanga) Hussein Hading’oka (Kinondoni), Leons Ngalai (Rombo) na Daudi Makenga Nzukila (Nzega).

Waliotetea nafasi zao ni Austin Kapera Shaba (Mtwara Mjini), Luteni Kanali Ayoub Kimbau (Mafia), Paul Bomani (alikuwa mbunge wa kuteuliwa na Waziri wa Ardhi, Maliasili na Utalii), Amran Halfani Mayagila (Iringa Mjini), Joseph Mungai (Mufindi), Samwel Luangisa (Bukoba Mjini, Cleopa David Msuya (Mwanga na Waziri wa Fedha) na Kingunge Ngombale-Mwiru (alikuwa mbunge wa kuteuliwa na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, na katika uchaguzi huu alishinda kiti cha Kilwa).

Wengine walioshinda ni Guntran Itatiro (Ulanga, na alikuwa Waziri wa Nchi katika Wizara ya Mawasiliano na Ujenzi), Benjamin William Mkapa (alikuwa mbunge wa kuteuliwa na Waziri wa Mambo ya Nje na sasa alishinda kiti cha Nanyumbu), Pius Ng’wandu (Maswa, Waziri wa Nchi katika Wizara ya Maji, Nishati na Madini), Hannington Mfaume (Shinyanga Mjini), Sumbu Gallawa (Singida Mjini) na John Machumba (Ukerewe, Waziri wa Kilimo).

Wengine walioshinda ni Samuel Sitta (Urambo, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Ustawishaji wa Makao Makuu), Luis Kinyonto (Sumbawanga Mjini), Luka Kitandula (Mkinga), Mustafa Salum Nyang’anyi (Kondoa, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Ushirikiano wa Kimataifa), Lumuli Kasyupa (Kyela), Mathias Kihaule (Ludewa) na Basil Mramba (alikuwa mbunge wa kuteuliwa, Waziri wa Viwanda na Biashara na sasa alishinda kiti cha Rombo dhidi ya Leons Ngalai).

Miongoni mwa walioshinda katika uchaguzi huo ni pamoja na wabunge wawili wa zamani, ambao walishindwa baada ya mahakama kutengua matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 1980. Wabunge hao ni Chediel Mgonja (Same) na Abel Mwanga (Musoma Mjini).

Kutokana na sheria, aliyechaguliwa akipatikana na hatia inayohusiana na rushwa haruhusiwi tena kugombea katika uchaguzi kwa miaka isiyopungua kumi, lakini hao wawili walipata msamaha wa Rais.

Katika Jimbo la Arusha, Luteni Kanali Abdulrahman Omari Kinana alishinda kwa kupata kura 25,717 dhidi ya mpinzani wake, Dk Nganga Ashaeli Kipuyo (mbunge wa zamani), aliyepata kura 9,311. Zilipigwa kura 36,166.

Patrick Qorro alishinda jimbo la Karatu baada ya kupata kura 23,271 na kumshinda mpinzani wake, Simon Taimo aliyepata kura 6,438. Kura zilizopigwa katika uchaguzi huo zilikuwa ni 30,026.

Katika jimbo la Mbulu, aliyeshinda alikuwa Phillip Sung’ka Marmo kwa kupata kura 32,797 na kumshinda mbunge wa zamani, Salustian Deengw aliyepata kura 7,943. Amran Halfani Mayagila alishinda Iringa Mjini kwa kura 11,756 dhidi ya Juliana Chota, aliyepata kura 5,398.

Joseph Mungai (mbunge wa zamani), katika Jimbo la Mufindi, alipata kura 47,336 dhidi ya kura 13,441 za mpinzani wake, Joseph Kwilla. Jimbo la Ilala, Kapteni Ukiwaoni Ditopile-Mzuzuri alishinda kwa kupata kura 49,237 dhidi ya mbunge wa zamani, Martha Weja aliyepata kura 27,647.

Katika uchaguzi huu ndipo alipoibuka Augustine Mrema katika Jimbo la Moshi Vijijini. Mrema alishinda kwa kupata kura 38,984 na kumshinda Peter Macha aliyepata kura 34,709.

Katika Jimbo la Mwanga, David Msuya alitetea ubunge kwa kupata kura 20,233 dhidi ya Mwagachi Msangi, aliyepata kura 11,611.

Kwa jimbo la Same, Chediel Mgonja alishinda kwa kupata kura 16,927 dhidi ya Joasi Manento, aliyepata kura 8,270, huku Kingunge Ngombale-Mwiru, ambaye awali alikuwa ni mbunge wa kuteuliwa, alimshinda Saidi Bungara kwa kupata kura 16,798 dhidi ya 4,262.

Katika Jimbo la Morogoro Mjini, Shamim Parkar Khan alishinda kwa kupata kura 14,328 dhidi ya Emile Omar Malinza, aliyepata kura 6,303.

Jimbo la Nanyumbu Benjamin Mkapa, ambaye alikuwa mbunge wa zamani wakuteuliwa, alishinda kwa kupata kura 17,561 dhidi ya Albert Nachunga, aliyepata kura 14,228. Naye Pius Ngw’andu, aliibuka tena kidedea Maswa alipopata kura 28,896 na kumshinda Joseph Singu (11,124).

Jimboni Shinyanga Mjini, Hannington Mfaume alifanikiwa kutetea ubunge wake alipopata kura 10,243 huku Festo Mabonesho Makune akipata kura 9,809. Singida Mjini ushindi ulikwenda kwa Simbu Gallawa baada ya kupata kura 10,450 dhidi ya Mahami Kundya (9,988).

Jimboni Urambo, Samuel Sitta aliendeleza ubunge wake kwa kupata kura 29,331. Mpinzani wake, Hussein Lwali, alipata kura 7,576 kati ya kura 37,720 zilizopigwa.

Naye Stephen Wassira alimshinda mbunge wa zamani wa Jimbo la Bunda, Thomas Bwire. Wassira alipata kura 24,169 dhidi ya 20,752 za mpinzani wake huku katika jimbo la Makete, Tumtemeke Sanga alimshinda vibaya mpinzani wake Wilson Ntuli alipozoa kura 25,152 dhidi ya kura 7,270.

Katika uchaguzi huo, jimbo la Hanang lilimtangaza Frederick Sumaye kuwa mbunge baada ya kupata kura 12,796 dhidi ya Salistian Akunaay Deengw.

Columnist: mwananchi.co.tz