Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Waandishi, wadau wamlilia mwenzao wa Mwananchi aliyefariki dunia

50889 Pic+waandishi

Sun, 7 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza/Bukoba. Waandishi na wadau wa habari Kanda ya Ziwa wamemlilia aliyekuwa mwandishi wa habari wa kujitegemea wa gazeti la Mwananchi wilayani Ngara, Shaaban Ndyamukama aliyefariki dunia jijini Mwanza usiku wa kuamkia jana.

Miongoni mwa waliomlilia Ndyamukama ni mwenyekiti mstaafu wa CCM Mkoa wa Kagera, Pius Ngeze aliyesema alimfahamu Shaaban kupitia maandiko yake kwenye vyombo mbalimbali vya habari alivyovifanyia kazi.

“Nilimfahamu zaidi Shaaban kwa habari zake alizokuwa akiziandika kwenye gazeti Mwananchi. Aliandika habari nzuri bila upendeleo ambazo wengine walihofia kuziandika. Hata niliposikia sauti yake kwenye radio alizokuwa akiripoti nilikuwa makini kumsikiliza,” alisema Ngeze.

Mwandishi wa gazeti la Tanzania Daima mkoani Kagera, Antidius Kalunde aliyekuwa jijini Mwanza pamoja na Ndyamukama wakishiriki mafunzo ya uandishi wa habari za haki za binadamu, alisema taarifa za kifo hicho zilimshtua kwa sababu licha ya kuugua wakati mafunzo yakiendelea, hakuonyesha dalili ya kuzidiwa.

“Kuna wakati Ndyamukama ndiye alikuwa akituongoza washiriki kuwapongeza watoa mada. Ni vigumu kuamini kuwa hayuko nasi tena duniani,” alisema Kalunde.

Jijini Mwanza, watu kadhaa wakiwamo waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali walijitokeza Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sekou-Toure kuuaga mwili wa Ndyamukama uliosafirishwa kwenda nyumbani kwao Muleba, Kagera kwa maziko.

Mratibu wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd Kanda ya Ziwa, Peter Saramba aliyewaongoza waandishi wenzake kumuaga mwenzao, alisema kifo cha Ndyamukama kimeacha pengo katika tasnia ya habari kutokana na uwezo wake wa kutafuta na kuandika habari bila hofu, upendeleo wala woga.

“Wakati wa uhai wake, Ndyamukama alikuwa tayari kufanya lolote lililo ndani ya uwezo wake kutafuta na kuripoti tukio linalotokea ndani au nje ya eneo lake la kazi. Kuna wakati alikuwa akifuatilia na kuandika matukio yanayotokea mkoani Kigoma licha ya yeye kuishi Ngara,” alisema Saramba.

Samidu Shabani, ambaye ni baba mdogo wa marehemu aliyeongoza ndugu, jamaa na marafiki wakati wa kushughulikia usafirishaji wa mwili wa marehemu Ndyamukama aliwashukuru wadau wa habari waliojitokeza kushirikiana na familia kufanikisha shughuli hiyo.

“Nawashukuru Mwananchi (Mwananchi Communications Ltd) kwa msaada wao wa hali na mali; familia tumefarijika jinsi walivyouchukulia msiba huu kwa uzito mkubwa,” alisema Samidu.

Pia, Rukia Swedi ambaye ni shangazi wa Ndyamukama licha ya kuwashukuru waliojitokeza kuaga mwili, alisema kifo hicho kimewaondolea wana familia mtu mcheshi na mkarimu aliyejitolea kwa hali na mali kuwasaidia wengine.

Marehemu Ndyamukama alizikwa jana jioni kijijini kwao Nshisha wilayani Muleba.



Columnist: mwananchi.co.tz