Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Vitendawili na utajiri uliositirika ndani yake

11813 Erasto+Duwe TanzaniaWeb

Tue, 14 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Vitendawili ni kipera cha fasihi simulizi katika utanzu wa semi ambacho hutegwa kama fumbo ili mmoja aweze kutegua au kutoa jibu.

Vitendawili vimekuwa vikitumiwa zaidi kwa watoto kwa lengo la kubungua bongo zao kwa kuwafikirisha kwa haraka na kutoa majibu.

Mmoja anaposhindwa kutegua kitendawili, ili yule aliyetega kitendawili hicho aweze kutoa jibu hana budi kutajiwa mji mpaka atakaporidhia.

Kwa ujumla, vitendawili vimekuwa vikichukuliwa kama vile kipera maalumu kwa ajili ya kuwachangamsha na kuwaburudisha watoto.

Watu wazima kwa muktadha huu wamekuwa wakihusishwa zaidi na methali kuliko vitendawili. Hata hivyo, vyote ni vipera vya semi na vina dhima mbalimbali katika jamii.

Kwa upande wa uundwaji wake, vitendawili vinaundwa kutokana na uzoefu wa mambo na matukio mbalimbali yanayopatikana na kutokea katika mazingira ya jamii husika.

Mabadiliko yanayotokea katika jamii husika kwa namna moja au nyingine huathiri vitendawili hivyo. Kwa sababu hiyo, vipo vitendawili ambavyo utegaji wake ni uleule, lakini majawabu yake yamekuwa yakibadilika kulingana na mabadiliko ya matukio, wakati na mazingira katika jamii.

Licha ya msisitizo mkubwa wa dhima ya vitendawili unaowekwa katika kuburudisha watoto au kuwafikirisha, vitendawili vina dhima kubwa nyingine zikiwamo za kufundisha maadili na mila za jamii, kutunza kumbukumbu za kihistoria na kuonyesha maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia.

Kama ilivyo kwa vipera vingine vya fasihi simulizi ambavyo vina dhima mbalimbali katika jamii ndivyo ilivyo pia kwa vitendawili. Mintaarafu dhima ya kufundisha maadili katika jamii, baadhi ya vitendawili kwa namna vilivyoundwa na maudhui yake, vinatoa miiko fulani ya kimaadili katika maisha.

Kwa mfano, kitendawili kama vile ‘Nyumbani kwetu nina papai bivu sana lakini kulichuma/kulila siwezi; jibu lake ni ‘kaka au dada’. Methali hii inamaanisha kuwa ndugu wa damu moja mathalani kaka na dada hawatakiwi au ni mwiko kwao kuwa na uhusiano wa kimapenzi.

Kuhusu vitendawili kutunza historia ya jamii, kitendawili ‘Bibi kizee katupwa jalalani’ ambacho jibu lake ni machicha ya nazi, kina majibu mengine yanayoendana na historia ya jamii. Majibu hayo ni kama vile Mwarabu au Mzungu.

Kuwapo kwa majibu mengi ya kitendawili hiki kunatokana na mabadiliko ya kihistoria yaliyopata kutokea katika jamii. Hapo awali kabla ya ujio wa wageni na shughuli walizozifanya, kitendawili hicho kilitegwa na majibu yakawa ‘machicha ya nazi’.

Baada ya ujio wa Waarabu na utawala wa wakoloni wa Kijerumani na Kiingereza, kitendawili hichohicho kilitegwa na kubadili majibu kutokana na historia ya watu hao.

Halikadhalika, vipo vitendawili vinavyoonyesha kipindi cha kutawaliwa na wakoloni na kutamalaki kwa sayansi na teknolojia. Kwa mfano, kitendawili kama ‘kandokando ya barabara ya kwenda kwetu pamesimamishwa watumwa waliofungwa minyororo shingoni’ jibu lake ni nguzo za umeme au simu.

Hata hivyo, kiendawili hiki ingawa kinaonyesha kuwapo kwa maendeleo ya sayansi na teknolojia bado kinataja utumwa kuakisi matukio ya kihistoria yaliyopata kutokea.

Kitendawili kingine kinachoonesha maendeleo ya sayansi na teknolojia ni ‘Jani la mgomba laniambia habari zinazotokea ulimwenguni kote.’ Jibu lake ni ‘gazeti au jarida’.

Vitendawili kama vilivyo vipera vingine vya kifasihi, vina dhima mbalimbali muhimu kulingana na mitazamo na uhakiki wake, licha ya dhima ile ya kuwachangamsha watoto na kuonekana kwamba lengo lake zaidi ni kubungua bongo za watoto.

Columnist: mwananchi.co.tz