Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Vilio na simanzi vilitawala ajali ya kuzama kwa Mv Nyerere Ukerewe

Wed, 26 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Kiasili, binadamu wameumbwa na tabia ya kusahahu. Lakini kwa wakazi wa Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, hasa kisiwa cha Ukara, Septemba 20 haitasahalika kirahisi maishani mwao.

Hii ni siku ambayo kivuko cha Mv Nyerere kilipopinduka na kugeuka juu chini kikiwa hatua chache kutoka gati la kijiji cha Bwisya.

Ajali hiyo inadaiwa kusababishwa na kivuko hicho kujaza watu na mizigo kuliko uwezo wake.

Watu 230 walipoteza maisha huku wengine 41 wakiokolewa kwa juhudi za wananchi wakishirikiana na kikosi maalumu cha uokoaji kutoka vyombo vya ulinzi na usalama na makundi mengine kutoka ndani na nje ya mkoa huo.

Kati ya watu 230 waliopoteza maisha, watu 88 kutoka kaya 73 walikuwa ni wakazi wa kisiwa cha Ukara chenye jumla ya kaya 600.

Wingi wa watu na mizigo ulitokana na siku hiyo kuwa maalumu kwa ajili ya gulio cha Bugorola linalofanyika kila siku ya Alhamisi.

Matukio yanayokumbukwa

Uhodari wa wakazi wa Ukara, hasa wavuvi waliotumia ujuzi wao wa kuogelea na vyombo vyao vya uvuvi kuokoa watu 40 kabla ya mmoja kuokolewa na vikosi vya uokoaji vilivyowasili siku moja baada ya ajali ni kati ya matukio makubwa yaliyojiri wakati huo.

Fundi kuokolewa saa 48

Tukio la Septemba 22 la aliyekuwa Fundi Mkuu wa kivuko hicho, Alphonse Charahani kuokolewa baada ya kukaa chini ya maji kwa saa 48 tangu ajali ilipotokea Septemba 20.

Pamoja na kukaa kwenye chumba cha injini, Charahani alitumia ujuzi wa ubaharia kwa kujipaka oili chafu mwilini kuzuia maji kumwingia mwilini kupitia kwenye vinyweleo.

Kabla ya kuokolewa, Charahani alikuwa akitumia mbinu ya kibaharia kwa kugonga ukuta wa meli mara tatu ili kufikisha ujumbe kwa waokoaji kuwa kuna mtu hai ndani ya chumba alimokuwemo.

Nguvu ya mitandao ya kijamii

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella ni kati ya watu waliopata wakati mgumu kutokana na nguvu ya mitandao ya kijamii baada ya wengi kujitokeza kushutumu uamuzi wake wa kusitisha uokoaji usiku wa Septemba 20.

Kiongozi huyo alilazimika kuwatumia waandishi wa habari wa vyombo waliopiga kambi kisiwani Ukara kutoa ufafanuzi wa uamuzi huo ili kutuliza upepo wa shutuma na lawama zilizoelekezwa kwake.

Katika ufafanuzi wake, alisema uamuzi wa kusitisha uokoaji ulitokana na ushauri wa kitaalamu kutoka kwa timu ya wazamiaji kutokana na hali mbaya iliyojitokeza chini ya maji nyakati za usiku.

Kamwelwe na wanahabari

Pamoja na kusimamia vyema uokoaji, Waziri wa ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Issac Kamwelwe alitia tembo maji kwa kuonyesha upendeleo kwa vyombo vya Serikali akivisifia licha ya ukweli kwamba hata vyombo binafsi pia vilipiga kambi kijijini Bwisya, Ukara kuwahabarisha wananchi kwa ufasaha na usahihi kila kilichojiri.

Kilele cha tofauti kati ya Waziri Kamwelwe na waandishi kutoka vyombo binafsi kilikuwa Septemba 22 alipogoma kujibu maswali huku akitishia kumsweka mahabusu mmoja wao aliyehoji ni lini Taifa litajifunza na kuchukua hatua kudhibiti ajali za majini zinazosababishwa na uzembe wa usimamizi duni wa sheria na kanuni.

Hata hivyo, akihitimisha kazi ya uokoaji, waziri huyo alirekebisha kasoro hiyo kwa kuungana na Mongella kuvipongeza vyombo vyote vya habari vikiwemo binafsi kwa kazi nzuri ya kuhabarisha umma kwa usahihi, umakini na uzalendo.

Ushauri kutoka kwa wafiwa

Mtoroki Masena, akizungumza nyumbani kwake kijiji cha Bwisya muda mfupi baada ya mazishi ya mke wake, Buhinda Mtoroki na mwanaye Nyanjira Mtoroki, alitaja usimamizi duni wa vyombo vya usafiri wa majini kuwa miongoni mwa sababu zilizosababisha ajali.

Alitolea mfano idadi ya waliofariki dunia na kuokolewa iliyodhihirisha kuwa chombo hicho kilipakia abiria zaidi ya mara mbili ya uwezo wake.

Wakati Mv Nyerere ilikuwa na uwezo wa kupakia abiria 101 na tani 25 ya mizigo, chombo hicho kilipakia abiria zaidi ya 271 baada ya miili 230 kuopolewa, watu 41 kukolewa huku baadhi ya watu wakikosa miili ya ndugu zao waliodaiwa kuwemo ndani ya chombo muda mfupi kabla ya ajali.

Ukara walilia gulio lao

Wakazi wa kisiwa cha Ukara walitumia tukio la ajali hiyo kuiomba Serikali kuanzisha gulio kisiwani humo ili kuwaondolea adha ya kutegemea gulio la Bugorola kupata mahitaji, ombi lililojibiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Ester Chaula kuwataka kupitishia maombi hayo kwenye vikao vya uamuzi kuanzia ngazi ya vijiji na kata.

Kauli kama hiyo pia ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mongella aliyesisitiza ushirikishwaji wa wananchi katika suala la kuanzisha magulio katika maeneo yao.

Wakazi zaidi ya 50,000 wa cha Ukara wanategemea gulio la Bugorola linalofanyika Alhamisi kila wiki kupata mahitaji yao muhimu na njia kuu ya usafiri kati ya maeneo hayo ni ule wa majini ambapo kivuko cha Mv Nyerere kilichopinduka ndicho kilikuwa tegemeo.

Serikali kujenga meli mpya

Akizungumza na wakazi wa Ukara wakati wa mazishi ya kitaifa Septemba 23, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliutangazia umma uamuzi wa Serikali wa kujenga kivuko kipya chenye uwezo wa kupakia abiria 200 na tani 50 ya mizigo ikiwa ni mara mbili ya uwezo wa Mv Nyerere iliyokuwa na uwezo wa kupakia abiria 101 na tani 25 ya mizigo.

Wataalamu, vyombo vya uokoaji

Ajali ya Mv Nyerere ililikumbusha Taifa umuhimu wa kuwa na wataalamu wengi wabobevu wa shughuli za uokoaji pamoja na zana na vifaa, hasa katika Kanda ya Ziwa Victoria ambako kumeshuhudiwa ajali ya pili kubwa iliyoangamiza maisha ya watu wengi.

Ajali ya kwanza katika kanda hiyo ni ile ya kuzama kwa Mv Bukoba iliyopinduka na kuzama Mei 21, 1996 na kusabisha vifo vya watu zaidi ya 800.

Licha ya kuwepo vikosi na kambi kadhaa za Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kikosi cha uokoaji katika ajali ya Mv Nyerere kiliundwa na askari kutoka makao makuu jijini Dar es Salaam na wazamiaji kutoka Zanzibar.

Hata vifaa na vyombo maalumu vya uokoaji zikiwemo meli za kunyanyua na kugeuza kivuko cha Mv Nyerere vilipatikana kutoka kampuni na taasisi binafsi jijini Mwanza.

Utakaso kwa wafiwa

Baada ya kukamilisha taratibu za msiba na maombolezo, wakazi wa kisiwa cha Ukara waliopoteza ndugu katika ajali ya kivuko cha Mv Nyerere ambao siyo waumini wa Kikristo na Kiislamu hutengwa kupitia mila ya Lichumu na Emisilo kwa kuzuiwa kuchangamana na wana jamii hadi wanapotakaswa.

Kwa mujibu wa mmoja wa wazee maarufu wa jamii ya Wakara, Zakaria Chibuga utakaso kwa mume au mke aliyefiwa katika janga au vifo vya kawaida hupatikana kwa njia ya kujamiiana na mtu mwingine nje ya ukoo, kijiji au eneo analoishi mfiwa.

“Mwanaume au mwanamke anayefiwa hulazimika kumtafuta mtu wa kumtakasa kwa kulala naye (kuwa na uhusiano wa kingono); analazimika kwenda kijiji jirani kumtafuta wa kumkatasa ndipo arejee kuchangamana na jamii kwenye eneo lake,” alisema Chibuga.



Columnist: mwananchi.co.tz