Dar es Salaam. Ni matukio ambayo maelezo yake yanafanana, lakini ongezeko la kutokea kwake limeibua sintofahamu; ni kuhusu watuhumiwa kufariki wakiwa mikononi mwa polisi.
Baadhi ya watuhumiwa wamefariki kutokana na kupigwa risasi “wakati wakijaribu kutoroka”, “kupigwa risasi na wenzake” wakati akiwaongoza polisi kwenda kuonyesha maficho na wengine kupigwa na polisi baada ya kutokea kutoelewana.
Wako pia walionusurika kifo kutokana na kutotendewa vyema na polisi kama mwanamke mmoja mkoani Morogoro, aliyejifungulia nje ya kituo cha polisi baada ya kukamatwa kwa tuhuma zinazomkabili mumewe na baadaye kutopewa msaada na polisi alipojisikia uchungu.
Tukio la mwisho kabla ya habari hii ni lile lililotokea Mwanza ambako askari waliokuwa doria walipiga watuhumiwa waliokuwa wamewakamata na kusababisha kifo cha mmoja aliyejulikana kwa jina la Christian Enock.
Hilo ni moja ya matukio kadhaa ya watu kupoteza maisha wakiwa mikononi mwa polisi baada ya kukamatwa kwa tuhuma za uhalifu.
Mbali na matukio hayo kufanana, hata sababu zinazotolewa baada ya watuhumiwa kufariki zinafanana; “walikuwa wakijaribu kuwatoroka polisi ndipo walipopigwa risasi na kupoteza maisha wakiwa wanapelekwa hospitalini”.
Sababu nyingine imekuwa ni ile ya “katika kurushiana risasi na polisi” au “mtuhumiwa kuuawa na majambazi wenzake wakati akijaribu kuonyesha walipo” au “wakati akionyesha wanapoficha silaha”.
Kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Januari, Mwananchi imebaini kuwepo kwa matukio kama hayo katika mikoa tofauti, huku Dar es Salaam, Mwanza, Mara, Mbeya, Geita na Pwani ikiongoza.
Tukio lililopewa nafasi kubwa na vyombo vya habari ni lile la askari mmoja wilayani Tarime aliyemuua kwa kisu Chacha Heche Suguta wakati akiwa kwenye gari la polisi baada ya kukamatwa usiku akiwa baa.
Wakati huo, kamanda wa polisi wa Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe alisema kijana huyo, ambaye ana uhusiano na John Heche (mbunge wa Tarime Vijijni), alikuwa na mgogoro na mmoja ya askari waliokuwa wamemkamata, na kufikia hatua ya kutaka kushikana.
Alisema kijana huyo alikuwa na kisu kiunoni na polisi walifanikiwa kumpokonya na baada ya kutokea kutoelewana, askari huyo aliposhindwa kujizuia na kumchoma kisu.
“Ni jambo la kusikitisha mtuhumiwa kufariki dunia akiwa chini ya mikono ya polisi. Inaonekana ni heri uwe chini ya majambazi kuliko mikono ya polisi,” alisema John Heche baada ya kupata taarifa hizo.
Heche alitoa kauli hiyo baada tu ya taarifa za kuuawa kwa mdogo wake, ambaye alibishana na polisi wakati akiwa baa kabla ya kukamatwa.
Hadi sasa, polisi imesema waliohusika wako chini ya ulinzi na uchunguzi unaendelea ili wakibainika kuwa walifanya makosa, wachukuliwe hatua za kisheria.
Juhudi za gazeti hili kumpata Mkuu wa Jeshi la Polisi kuzungumzia suala hilo hazikufanikiwa na hata lilipompata msemaji wa chombo hicho, Barnabas Mwakalukwa, hakutaka kuzungumzia suala hilo.
Badala yake alimtaka mwandishi wetu awatafute makamanda wa polisi wa mikoa ambayo matukio hayo yametokea ili wazungumzie.
Mwananchi ilipomtafuta Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba kuzungumzia kuhusu mwenendo huo, alisema hadi sasa anafahamu tukio moja.
“Hakuna ushahidi wa raia mwingine kufia mikononi mwa polisi,” alisema Waziri Mwigulu akirejea tukio la Suguta kuchomwa kisu wakati alipoulizwa na mwandishi wetu mkoani Kilimanjaro mwishoni mwa wiki iliyopita.
“Mbali na tukio la Mara, hamna tukio lenye evidence (ushahidi) kwamba mwananchi amefia mikononi mwa Polisi na sisi tuna utaratibu. Jeshi la Polisi linaongozwa na misingi ya kazi.
“Hii ya kwamba wananchi wamefia mikononi mwa polisi, watu wasiijumuishe sana kwani itatengeneza chuki kwa wananchi na polisi kitu ambacho si sahihi. Na Watu wasitumie fursa hiyo kuona kuna tukio limetokea na kujumuisha kuwa watu wanafia mikononi mwa polisi.”
Waziri Mwigulu alisema raia hukimbilia polisi kuepuka wananchi wenye hasira wakati wanapofanya makosa, na hivyo haiwezekani wakawa wanafia mikononi mwao.
Kuhusu tukio la kuchomwa kisu kwa Suguta, alisema tayari hatua zimeshachukuliwa.
“Tukio la Mara polisi walishalielezea kwa kirefu na tulishalichukulia hatua na kutoa rai tukio kama hilo lisijitokeze tena maeneo mengine. Taasisi yetu inaongozwa kwa mujibu wa sheria,na nisisitize waendelee kufanya kazi kwa misingi ya sheria,” alisema Mwigulu.
Pamoja na msimamo huo wa Waziri Mwigulu, matukio yaliyokusanywa na gazeti hili yanaonyesha kuwa watuhumiwa wamekuwa wakipoteza maisha chini ya ulinzi kwa sababu na mazingira yanayofanana.
Matukio hayo yalitokea jijini Dar es Salaam, Kigoma, Arusha, Mara, Geita, Morogoro, Pwani na Mbeya.
Katika moja ya matukio hayo, polisi mkoani Kigoma iliripoti kuwa watu wawili wanaotuhumiwa kwa ujambazi waliuawa Machi 20 katika pori la Makere mkoani Kigoma baada ya kupigwa risasi na wenzao.
Wakati huo, kamanda wa polisi wa mkoa, Martin Otieno alisema watuhumiwa hao waliokuwa mikononi mwa polisi, walipigwa risasi na majambazi wenzao kwa lengo la kuwakwamisha wasionyeshe silaha zilipo.
Tukio kama hilo lilitokea Juni 3 mkoani Shinyanga ambako watu wanne wanaodaiwa kuwa ni majambazi waliuawa kwa kupigwa risasi na polisi wakati wakijaribu kuwatoroka askari waliokuwa kwenye msako.
Wakati huo, kamanda wa polisi wa mkoa, Simon Haule alisema tukio hilo lilitokea eneo la makaburi ya Kitwana kata ya Busoka wilayani Kahama.
Tukio jingine lilihusisha kijana aliyekuwa akishikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuteka malori matano eneo la Milade barabara kuu ya Singida-Mwanza na kuwapora abiria mali. Polisi walisema walimuua kijana huyo wakati akijaribu kumvamia askari na kumnyang’anya silaha ili atoroke wakati akiwa chini ya ulinzi.
Wakati huo, kamanda wa polisi wa mkoa huo, Thobias Sedoyeka alisema mtuhumiwa alikamatwa akiwa amejificha kwenye nyumba iliyopo eneo la Kindai, Singida Mjini na alikutwa akiwa na pikipiki iliyoonekana katika tukio la utekaji wa magari.
Katika tukio jingine, familia ya Mapunda wa Mtera wilayani Mpwapwa iliususa mwili wa ndugu yao Simon Mapunda (24), ikidai alifariki akiwa polisi wa kituo cha Mtera.
Simoni alikamatwa na polisi mmoja mchana wa Mei 26 kwa kile kilichoelezwa alikuwa na ugomvi na kijana mwenzake.
Msemaji wa familia, Msafiri Gondwe alisema wakati huo kuwa polisi walimkamata Mapunda wakimtaka akatoe maelezo kituoni ingawa ugomvi wao ulishasuluhishwa.
“Tuliomba kumuwekea dhamana, lakini polisi walikataa, siku hiyo hiyo jioni wakati tukijiandaa kumpelekea chakula, tulipata taarifa za msiba kwamba Simoni amefariki na wakati huo polisi walikuwa wanatafuta namna ya kuuondoa mwili huo,” alidai.
Wakati huo, kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma Gilles Muroto alipoulizwa juzi kuhusu tukio hilo, alimtaka mwandishi kutoka kwenye kelele ili ampigie tena.
Hata hivyo alipopigiwa hakupokea lakini alipotumiwa ujumbe alijibu kwa ufupi: “Nalifuatilia utafahamishwa.” Lakini jana alipoulizwa tena alisema hawezi kulizungumzia jambo hilo kwa kuwa alikuwa kwenye kikao.
Gondwe alisema walipofika hospitali ya mkoa wa Dodoma juzi, madaktari waliufanyia uchunguzi mwili wa Simon lakini wakasema hawawezi kutoa majibu ya moja kwa moja hadi vipimo vifanyike.
Tukio jingine la mtuhumiwa kufariki au kuuawa akiwa mikononi mwa polisi, lilitokea Machi 30, jijini Dar es Salaam ambako polisi walimuua ilimuua mtu ambaye jeshi hilo lilisema lilimkamata akiwa na bastola na kukiri kuhusika katika matukio ya ujambazi.
Mtu huyo aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa eneo la Buza ambako Jeshi la Polisi lilisema alikuwa alijaribu kuwatoroka askari wakati akiwapeleka kuwaonyesha sehemu wanapoficha silaha na majambazi wenzaake.
Wakati huo, kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa alisema mtuhumiwa alikamatwa akiwa na bastola na alipohojiwa alikiri kuhusika na matukio kadhaa ya ujambazi maeneo ya Mbagala na Kibiti.
Mkoani Geita pia kulikuwa na tukio kama hilo. Kamanda wa polisi mkoa, Mponjoli Mwabulambo, alisema Panda Kinasa (36) aliyetuhumiwa kuwa kinara wa utekaji watu aliuawa kwa kupigwa risasi makalioni akiwa chini ya ulinzi akijaribu kuwatoroka polisi baada ya kuwapeleka kwenye mashimo alikokuwa ametupa miili ya watu wawili wilayani Bukombe.
Wakati matukio hayo yakitokea, wanasheria wanaona kama sheria zinazotoa utaratibu wa namna ya kushughulika na mtuhumiwa, hazifuatwi kikamilifu.
“Mtuhumiwa anaweza akafariki akiwa mikononi mwa polisi kwa sababu za kawaida za kiafya, lakini kama ni kwa kuteswa au kupigwa hadi kufa kuna utaratibu wa kusimamia hilo,” alisema mwanasheria wa kujitegemea, Charles Rwechungura.
“Kuna sheria inayolinda haki za wananchi lakini pia upo utaratibu wa kisheria unaosimamia Jeshi la Polisi katika kutekeleza majukumu yake.”
Kauli hiyo inalingana na ile aliyoitoa Waziri Mwigulu baada ya mwanamke kujifungulia nje ya kituo cha polisi kutokana na askari kutozingatia haki zake za kisheria.
Mwanamke huyo alikuwa mjamzito anayetazamia, lakini alipowaambia kuwa anasikia machungu walimpuuza na badala yake wakamhamishia nje ambako alijifungua akiwa kwenye majani.
Tukio hilo lilisababisha Bunge kuhoji na Mwigu akasema bayana kuwa si haki mtuhumiwa kufanyiwa vitendo hivyo, lakini moto ulipozidi Spika John Ndugai akaamuru kamati ya Bunge ichunguze.
Akizungumzia vifo hivyo vya watuhumiwa mikononi mwa polisi, Rwechungura, ambaye amewahi kuongoza Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alisema sheria inataka hata askari anayesababisha kifo achukuliwe hatua.
“Sheria imeeleza mambo mazuri na inatoa haki kwa wote endapo ikisimamiwa vizuri,” alisema Rwechungura.
“Mtu akifariki akiwa mikononi mwa polisi anapimwa kujua chanzo cha kifo. Ndiyo maana unaweza kusikia askari fulani amekamatwa kwa kusababisha kifo.”
Naye John Seka (wakili), alisema kifo chochote kinapotokea, uchunguzi unapaswa kufanywa na maoni ya pande tofauti kusikilizwa na endapo kutakuwa na utata mtu anapaswa kulalamika na kufungua kesi mahakama ya Korona.
“Hatua ya kwanza ni kulalamika kwa mkuu wa kituo cha polisi husika ili kufungua jalada la uchunguzi, kisha uchunguzi wa kitabibu ili kujua chanzo cha kifo. Kama kuna utata kesi itafunguliwa na utaratibu wa kutafuta haki utafuatwa,” alisema Seka.
Lakini msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakalukwa hakutaka kuzungumzia suala hilo linaloonekana kuendelea kutokea mikoa tofauti, na badala yake akasema waulizwe makamanda wa mikoa ambayo matukio hayo yanatokea.