Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

VITA YA KAGERA: Yusufu Lule aondolewa madarakani-30

35325 Pic+vita VITA YA KAGERA: Yusufu Lule aondolewa madarakani-30

Wed, 9 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

HAKUNA vita visivyokuwa na gharama. Katika toleo lililopita tuliona gharama ambazo Tanzania na Uganda ziliingia kutokana na vita hiyo. Gharama ambazo Tanzania ilitumia ni Dola 500 milioni za Marekani. Askari wa Tanzania waliouawa katika mapigano kwenye vita hiyo ni 373 na takribani raia 1,500. Askari 600 miongoni mwa 3,000 wa Libya nao waliuawa.

Ingawa vita vilimalizika hatimaye, hali ya kisiasa nchini Uganda haikutulia. Ndani ya siku 68 tu Profesa Yusuf Lule aliondolewa madarakani na Baraza la Ushauri la Taifa (NCC). Sasa endelea...

Wakati vita dhidi ya Iddi Amin ikimalizika, tayari Uganda ilikuwa kwenye mgogoro wa kisiasa. Kumwondoa Amin madarakani lilikuwa jambo moja, lakini kuleta utulivu wa kitaifa lilikuwa jambo jingine.

Profesa Yusuf Lule aliapishwa Ijumaa ya Aprili 13, 1979. Siku chache baada ya kuapishwa alianza kupuuza maazimio yaliyofikiwa kwenye mkutano wao wa Moshi ambayo yaliwekwa kwenye katiba ya Umoja wa Kitaifa wa Kuikomboa Uganda (UNLF).

Katiba ya UNLF haikumpa Rais madaraka makubwa yakiwamo yale ya kuwateua mawaziri wake. Mamlaka makubwa yaliwekwa mikononi mwa Baraza la Ushauri la Taifa (NCC), lakini Lule alitaka mamlaka makubwa awe nayo Rais. Mgogoro ulianzia hapo.

Profesa Lule na washauri wake akiwamo Dk Andrew Lutaakome Kayiira, walianza kufanya uamuzi mkubwa na uteuzi mkubwa bila kuishirikisha NCC wala kupata ridhaa yake.

Matendo hayo yaliwakasirisha sana maofisa wa UNLF na wajumbe wa NCC. Lule aliwajibu kwa kuwaambia kuwa maazimio yaliyopitishwa kwenye mkutano wa Moshi hayakuwa na nguvu ya kisheria na kwamba yeye ataendelea kutekeleza majukumu yake kwa kutumia katiba iliyokuwapo kabla Amin hajatwaa madaraka—katiba iliyotengenezwa na Dk Milton Obote ambayo ilimpa Rais madaraka makubwa.

Lule kupuuza Azimio la Moshi kulianza kuonekana pale aliposhindwa kuhudhuria hafla ya kuapishwa kwa wajumbe wa NCC. Hafla hiyo ilipopangwa kufanyika upya, Lule alihudhuria, lakini baada ya kutoa hotuba fupi aliondoka kabla ya wajumbe kuapishwa, jambo lililowakasirisha zaidi.

Bila kuishirikisha NCC, Lule aliendelea kuwateua mawaziri na manaibu waziri aliowataka yeye. Aliwateua mawaziri 24 na manaibu wake 20 na hao moja kwa moja wakawa wajumbe wa NCC, wakiwazidi kwa idadi wajumbe waliochaguliwa katika mkutano wa Moshi.

Wajumbe wa NCC walikerwa zaidi pale Lule alipowapatia kila waziri wake Dola 5,000 za Marekani kama posho ya ukarabati wa nyumba zao. Walipomuuliza kulikoni akaamua kumpa kila mjumbe kiasi hicho cha fedha kutoka kwenye mfuko wa Serikali iliyofilisika—lakini wajumbe wa NCC waligoma, hakuwa na jibu.

Yote haya yalikuwa yakifanyika wakati Kampala ikiwa katika hali ya hatari. Milio ya risasi ilikuwa ikisikika kila siku hasa usiku na miili ya watu ikiwa inaokotwa kila asubuhi.

Wakati mgogoro kati ya Profesa Lule na NCC ukifikia hatua mbaya, Rais wa Tanzania, Mwalimu Nyerere aliwaita viongozi wa Serikali ya Uganda na kukutana nao Mwanza. Lule naye alifika Mwanza kukutana na Nyerere. Alifuatana na Paulo Muwanga na watu wengine. Walipata chakula cha mchana kilichoandaliwa na Nyerere katika Hoteli ya Mwanza.

Kitabu cha New African Yearbook 1991/92 kinasema katika mabadiliko ya baraza la mawaziri la Lule, kumi kati ya 19 walikuwa ni Wabaganda. Na baada ya kukutana na Nyerere mjini Mwanza alifanya mabadiliko mengine na kuongeza mawaziri sita wengine.

Mara baada ya kupata chakula, Muwanga akapokea taarifa kutoka Kampala kwamba Redio Uganda imetangaza mabadiliko ya baraza la mawaziri na kwamba hata yeye mwenyewe ameguswa. Aliondolewa Wizara ya Mambo ya Ndani akapelekwa Wizara ya Kazi. Hatua hii ilimkasirisha sana Muwanga, kwa mujibu wa kitabu cha UPC and National-Democratic Liberation in Uganda cha Yoga Adhola.

Mwandishi wa kitabu cha Guardian Angel: Volume Two: The Moshi Conspiracy, Dk Arnold Spero Bisase anasema Muwanga aliapa lazima amshughulikie Profesa Lule.

Mabadiliko ya baraza la mawaziri bila NCC kushirikishwa sasa ikaonekana kuwa Lule amekuwa sugu—haambiliki. Waliona kuwa amekuwa na kiburi sana hata akafanya mabadiliko ya baraza la mawaziri wakati ameonywa na Nyerere kwamba akiendelea na tabia hiyo basi yeye (Nyerere) hataweza kumuokoa.

Nyerere alimwambia Lule afuate Azimio la Moshi linalotaka mamlaka makubwa yawe ni ya NCC na si ya Rais. Lule alimsikiliza Nyerere, lakini ni kama hakumsikia.

Ijumaa ya Juni 8, 1979 wajumbe wa NCC waliokuwa na hasira walikutana mjini Kampala na kupitisha azimio la kumtaka Lule akabidhi teuzi zote “haraka sana” kwa NCC ili zijadiliwe na kuidhinishwa.

Siku nne zilipita bila NCC kupata jibu. Wajumbe wakakutana tena na kupitisha azimio jingine lililomtaka Lule atekeleze matakwa yao “mara moja”. Hata hivyo hawakupata jibu.

Jumanne ya Juni 19, 1979 NCC wakakutana tena. Wakati huu hawakukutana Kampala, bali ni kwenye Ikulu ya Entebbe. Walianza mkutano wao saa 9:22 alasiri chini ya mwenyekiti wao, Edward Bitanywaine Rugumayo.

Lule naye alihudhuria mkutano huo. Alipotakiwa kujibu kwa nini alipuuza maazimio ya NCC, alijibu hakufanya hivyo kwa sababu huko kungemaanisha “kuhusisha masuala muhimu ya kikatiba”.

Mjadala mkubwa uliendelea, kwa mujibu wa kitabu cha Upc and National-Democratic Liberation in Uganda. Mazungumzo ya wajumbe wengi ni Azimio la Moshi. Ingawa Lule alijitetea sana, alibanwa.

Alisema hakuwahi kupata mawasiliano yaliyotumwa kwake na NCC, lakini barua ya NCC aliipeleka Rugumayo mwenyewe ofisini kwa Lule.

Muda mfupi baadaye Profesa Paulo Wangoola akasimama. Akatoa hotuba ndefu. Akasema, “demokrasia imewekwa majaribuni ... Uamuzi unafanywa nje ya NCC ... Lule ameibaka UNLF ... Tumefikia mahali pagumu sana. Kuna ombwe la kisiasa. Rais (Lule) haikubali UNLF na hatuwezi kuwa na Rais asiyeikubali UNLF. Ingawa Lule alifanya kazi muhimu kutuleta Kampala, sasa anatukwamisha.”

Wangoola akahitimisha kwa kuleta hoja ya kutokuwa na imani na Profesa Lule. Mjadala mrefu ukaanza na kuendelea hadi usiku wa manane.

Hatimaye ilipohitimu saa saba kamili usiku, kura za siri zikapigwa. Dakika 35 baadaye matokeo yakatangazwa. Wajumbe 18 waliunga mkono hoja, 14 walipinga. Rugumayo akamgeukia Lule na kumwambia kuwa yeye si Rais wa Uganda tena. Baada ya kumwambia hivyo Lule, aliwageukia wajumbe na kusema, “Waliomwodoa Lule (yeye) kwenye kiti chake pia wamewaondoa na mawaziri wake”.

Lule, pamoja na wajumbe wengine tisa wa NCC wakasusa na kuondoka kikaoni. Lule akakoma kuwa Rais wa Uganda cheo alichokitumikia kwa siku 68 tu.



Columnist: mwananchi.co.tz