Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

VITA YA KAGERA: Wanajeshi wavamia Kagera wapora, wabaka wananchi-2

31044 Vitapic TanzaniaWeb

Wed, 12 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbali na nchi jirani kama Malawi, Kenya, Zaire (Congo DRC) na Msumbiji, eneo moja lililokuwa katika hatari kubwa ya kushambuliwa na maadui wa nje ni mpaka wa Uganda na Tanzania, lakini haukulindwa vya kutosha.

Chokochoko kati ya Tanzania na Uganda zilianza mwaka 1971. Mwaka uliofuata kukawa na makubaliano yaliyojulikana kama ‘Mazungumzo ya Mogadishu’ yaliyofanyika nchini Somalia Alhamisi ya Oktoba 5, 1972.

Mazungumzo hayo yalikuwa ni usuluhishi wa mgogoro kati ya Tanzania na Uganda. Kwa maana hiyo, Somalia iliepusha vita kati ya Tanzania na Uganda kwa miaka sita tangu 1972 hadi hali ilipovurugika mwaka 1978.

Walioshiriki katika mazungumzo hayo ni mawaziri wa mambo ya nje, ambao ni John Samuel Malecela (Tanzania), Joshua Wanume Kibedi (Uganda) na Umar Arteh Ghalib au Omer Carte Qalib (Somalia). Mwingine ni katibu mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), Nzo Ekangaki.

Mazungumzo ya Mogadishu yalifikia makubaliano kwamba majeshi ya Tanzania yakae kilomita 16 au zaidi kutoka mpaka wa Uganda. Lakini hata nje kabisa ya umbali huo, Jeshi la Tanzania halikuwako. Hilo linadokeza kwamba Tanzania haikufikiria kuwa Idi Amin angeishambulia Tanzania.

Kikosi kilichokuwa na jukumu la kuulinda mpaka wa Uganda ni Brigedi ya 202 ya Tabora chini ya Brigedia Yusuf Himid, ambaye alikuwa akisimamia Kanda ya Magharibi.

Mpakani palikuwa na batalioni ya tatu, yaani kikosi cha askari ambacho kina kombania kadhaa na ambacho ni sehemu ya brigedi au rejimenti. Hiki kilikuwa chini ya Luteni Kanali Morris Singano, ambaye miezi miwili kabla alihamishwa kutoka Mbeya kwenda Kanda ya Ziwa.

Mara baada ya zile ndege tatu za kivita za Uganda zilizoishambulia Tanzania zikiendeshwa na maluteni David Omita, Atiku na Abusala, Singano alituma taarifa hizo Brigedi ya Tabora, lakini Brigedi ilifikiria anachofanya Idi Amin ni kilekile alichokuwa akikifanya kwa zaidi ya miaka sita, kumbe hali ilikuwa tofauti.

Alhamisi ya Oktoba 20, 1978, baada ya mji wa Bukoba kushambuliwa, Mkuu wa Mkoa wa Kagera wakati huo ukiitwa Ziwa Magharibi, Mohamed Nassoro Kissoky, aliitisha mkutano wa viongozi wa CCM na Serikali na kuwaambia kwamba kinachoendelea mpakani ni hali ya kutoelewana tu na kwa sababu hiyo hakuna haja ya kuwa na hofu.

Kissoky aliwasihi viongozi hao wawaambie wananchi kuwa, “sisi ni marafiki wa Uganda na Idi Amin alikuwa mpakani akishikana mikono na watu wetu”.

Lakini wananchi wengi hawakuridhishwa na maneno ya Kissoky kwa sababu ndege za Amin zilikuwa zikionekana mara kwa mara na bado kulikuwa na wasiwasi wa mashambulizi mengine.

Kwa muda wote huu, ukiacha kauli ya Kissoky, hakuna ofisa mwingine yeyote wa CCM wala Serikali ambaye alikuwa ametoa kauli yoyote hadharani kuhusu kinachoendelea kati ya Tanzania na Uganda.

Jumapili ya Oktoba 22,1978 kundi la wanajeshi wa Uganda lilivuka mpaka kuingia Tanzania kunywa pombe. Waliendelea kunywa hadi askari wa Tanzania walipoingia eneo hilo. Huku wakiwa wameanza kulewa, walianza kufyatua risasi ovyo. Askari wa Tanzania nao wakajibu mapigo. Katika mapambano hayo mwanajeshi mmoja wa Uganda aliuawa.

Siku tatu baadaye, asubuhi ya Jumatano ya Oktoba 25, ikaripotiwa kuwa Mutukula ilikuwa ikishambuliwa vikali. Ingawa Kanali Singano alikuwa na wanajeshi wachache na alielekea kuzidiwa, alifanikiwa kunasa mawimbi ya redio iliyokuwa ikitumiwa na Jeshi la Uganda kutokea Kampala.

Kwa mujibu wa kitabu War in Uganda: The Legacy of Idi Amin, mawasiliano ya redio yalifanywa na Luteni Kanali Marajani. Lakini Uganda hawakuweza kuyanasa.

Asubuhi ya Ijumaa ya Oktoba 27, ndipo ndege tatu za kivita za Uganda aina ya MiG-21 ziliposhambulia mji wa Bukoba. Kombora moja kutoka katika ndege hizo lilianguka mita chache kutoka ilipo Hospitali ya Bukoba. Mojawapo ya ndege hizo ilitunguliwa.

Kwa wakati wote huu, vyombo vya habari vya Tanzania havikutangaza chochote kuhusu matukio hayo. Habari za matukio hayo zilisambazwa na wale waliokuwa wakikimbia vita.

Ingawa madhara hayakuwa makubwa, shambulio la Bukoba lilifanya raia kutaharuki na wengi kuukimbia mji. Hadi jioni ya siku hiyo, barabara zote za kutoka Bukoba zikawa zimefurika watu.

Jumatatu, asubuhi ya Oktoba 30 maelfu ya wanajeshi wa Uganda waliingia tena Tanzania kupitia maeneo manne—Kukunga, Masanya, Mutukula na Minziro. Raia wa Tanzania waliojaribu kupambana na majeshi hayo waliuawa.

Mamia ya wananchi wa Tanzania, hususan wanawake, walichukuliwa mateka na kupelekwa Uganda kwenye kambi ya Kalisizo. Kwa mujibu wa kitabu Great Britain’s Policy on the Uganda-Tanzania War (1978-9) cha Elisabeth Stennes Skaar, baada ya kuteka eneo lenye ukubwa wa kilomita 1,800 za mraba, wanajeshi wa Uganda walianza kupora, kubaka na kuua.

Kwa mujibu wa kijitabu cha Daniel Acheson-Brown cha The Tanzanian Invasion of Uganda: A Just War? kwa siku hiyo moja tu zaidi ya Watanzania 1,500 waliuawa. Wanajeshi wa Uganda walipora kila walichoweza kupora, yakiwamo magari. Na magari ambayo yalikuwa mabovu, yaling’olewa vipuri. Uporaji huo ulihusisha hata masufuria na vijiko jikoni.

Kiwanda cha Sukari cha Kagera kiliathirika zaidi na uporaji huo pamoja na ranchi ya Mishenyi. Mifugo iliyoporwa Kagera ikapelekwa Mbarara, Uganda ambako iligawiwa kwa askari na ndugu na marafiki wao.

Baadaye siku hiyo, Redio Uganda ikatangaza kulikomboa eneo la Kagera na kusema sasa mpaka halali wa Tanzania na Uganda ni Mto Kagera. Idi Amin mwenyewe alizuru eneo hilo na kupiga picha na silaha zilizoachwa na wanajeshi wa Tanzania waliokimbia.

Habari za kutekwa kwa Kagera zikamfikia Mwalimu Julius Nyerere. Jumatatu ya Oktoba 30, 1978 Mwalimu Nyerere aliwaita makamanda wa JWTZ nyumbani kwake. Miongoni mwao alikuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Luteni Jenerali Abdallah Twalipo.

Mkutano huo kati ya Mwalimu Nyerere na makamanda wa jeshi ulimalizika saa nne asubuhi, Mwalimu aliamuru kazi ianze mara moja. Siku iliyofuata, Jumanne ya Oktoba 31, katika taarifa ya habari ya saa 1:00 asubuhi, Redio Tanzania Dar es Salaam ilitangaza kwa mara ya kwanza matukio ya kivita katika mpaka wa Tanzania na Uganda.

VITA YA KAGERA: Luteni alivyoziingiza vitani Tanzania na Uganda-1

Itaendelea kesho



Columnist: mwananchi.co.tz