Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

VITA YA KAGERA: Vita yamalizika, JWTZ waendelea kutamba Uganda- 28

35025 Pic+kagera Idd Amin

Mon, 7 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kutekwa kwa mji wa Arua kukawa ndio mwisho wa Vita vya Kagera. Vita iliyoanza rasmi Oktoba 1978 kwa majeshi ya Iddi Amin kuvamia na kuteka eneo la kaskazini mwa Mto Kagera ikamalizika kwa majeshi ya Tanzania kuteka miji mingi ya Uganda na hatimaye kumaliza kwa kuuteka mji wa Arua.

Askari wa Iddi Amin waliofanikiwa kuyatoroka majeshi ya Tanzania walikimbilia Zaire na Sudan huku wakiapa kuwa wanakwenda kujipanga ili waje kuishambulia Serikali mpya ya Uganda.

Siku moja baada ya mji wa Arua kukombolewa, askari wa Tanzania walikutana na vijana wawili wakikimbia kuelekea kusini wakitokea upande wa Sudan.

Walipohojiwa walisema walitekwa kusini mwa Kampala na askari wa Amin waliokuwa wakikimbia kuelekea kaskazini mwa mji huo na kwamba, walipelekwa kusini mwa Sudan bila hiari yao pamoja na vijana wengine ambako waliambiwa wangepewa mafunzo ya kijeshi na siku moja wangerejea Uganda.

Kwa mujibu wa kitabu cha Kuzama kwa Idi Amin cha Baldwin Mzirai walipokuwa wakipelekwa Sudan, “vijana hao pamoja na wengine wawili, waliruka kutoka kwenye lori la kijeshi lililokuwa likiwasafirisha, wakakimbilia msituni...”

Kitabu cha War in Uganda kinasema vijana hao walisimulia kuwa wao pamoja na wengine watatu walifanikiwa kuruka kutoka kwenye lori kabla halijafika kwenye mpaka wa Uganda na Sudan na kwamba wenzao watatu walioruka pamoja, wao walionekana na waliuawa kwa kupigwa risasi walipokuwa wakijaribu kutoroka.

Vijana hao waliwaambia askari wa Tanzania kuwa kulikuwa na maelfu ya vijana wengine katika kambi hiyo iliyokuwa ikiendeshwa na Luteni Kanali Yakobo Abiringa ambaye alikuwa maarufu kwa jina la ‘999’. Walisema walipewa shilingi 600 za Uganda. Na kama ushahidi, waliwaonyesha wanajeshi hao fedha hizo.

Askari wa Brigedi ya Minziro walijisikia fahari sana kuhitimisha Vita vya Kagera baada ya kuuteka mji wa Arua. Brigedia Ahmed Kitete alifika hadi Koboko, kijijini alikozaliwa Iddi Amin, kiasi cha kilomita 40 kaskazini mwa mji wa Arua.

Hata hivyo alikuta kijiji hicho kilikuwa kimeshakimbiwa na watu na hivyo hakukuwa na dalili yoyote ya kuwapo kwa askari wa Amin. Baadaye ilijulikana kuwa wakazi wa kijiji hicho walikuwa wamekimbilia Zaire ambayo mpaka wake uko umbali wa chini ya kilomita moja.

Ingawa awali Watanzania waliambiwa kuwa katika kijiji cha Koboko, nyumbani kwa Amin, Iddi Amin alikuwa amejenga nyumba ya kifahari, Brigedia Kitete na askari wake hawakuiona nyumba hiyo. Walichokuta ni nyumba ya kawaida tu ya Amin ambayo nayo, kama zilivyokuwa zile nyingine ilikuwa imeporwa kila kitu.

Gazeti la New York Times la Jumatatu ya Juni 4, 1979 liliripoti kuwa katika kijiji cha Koboko, “Watanzania walikuta tu mbwa mmoja na kuku mmoja na hakukuwa na dalili nyingine yoyote ya uhai. Wanavijiji 1,000 au zaidi walikuwa wameshakimbia ... nyumba ya Amin ilikuwa imeporwa.”

Jenerali Silas Mayunga aliungana na Brigedi ya Minziro kukamilisha siku za mwisho za vita. Walivinjari kuanzia Koboko na kupita mpaka wa Uganda na Zaire hadi mpaka wa Uganda na Sudan. Upande wa Uganda watu walikuwa wamekimbia na kuvuka mpaka.

Kila baada ya kilomita chache Jenerali Mayunga na Brigedia Kitete walikuwa wakisimamisha msafara wa askari wao na kusoma ramani. Walikuwa wakifanya hivyo kuwa na uhakika kuwa hawavuki mpaka wa Uganda na kuingia nchi nyingine kama Zaire au Sudan.

Kabla msafara huo haujafika mpakani mwa Uganda na Sudan, Mayunga aliamuru vifaru na mabasi kusimama. Askari waliteremka kutoka kwenye vyombo hivyo na kutembea kwa miguu hadi mpakani. Eneo lote hilo lilikuwa limekimbiwa.

Umbali wa mita 300 kuvuka daraja dogo ndipo ulipo mpaka wa Sudan na Uganda. Umbali wa mita nyingine 300 ndani ya Sudan walionekana wanajeshi wa Sudan wakiwa na silaha zao zikiwa zimeelekezwa kwa askari wa Tanzania. Nyuma ya wanajeshi wa Sudan kulikuwa na maelfu ya raia ambao walidhaniwa kuwa ni Waganda, pamoja na magari kadhaa yaliyokuwa na namba za usajili za Uganda.

Watanzania walijisikia vibaya kidogo kuwapo eneo hilo huku wakiwa wameelekezewa silaha na askari wa Sudan. Ingawa askari wa Tanzania waliwapungia askari Sudan, Wasudani hawakupunga.

Mayunga hakuona sababu ya kuendelea kukaa eneo hilo na kuwafanya Wasudan hao kuendelea kuwa na wasiwasi juu yao. Ingawa walitaka kupiga picha mpakani mwa Uganda na Sudan, waliamua wasifanye hivyo.

Hadi muda huo Iddi Amin hakujulikana alikokuwa. Katika makala ya gazeti la The Monitor la Uganda toleo la Jumapili ya Mei 8, 2016 chini ya makala How Amin escaped from Kampala, askari wa Amin waliokutana naye siku za mwisho za utawala wake—Luteni Kanali Galla na Staff Sajini Taban Alai—walikaririwa na gazeti hilo wakikumbuka maneno waliyoambiwa na Iddi Amin.

Sajini Alai anakumbuka Amin akimwambia, “Bunduki uliyobeba sasa ni baba yako, ni mama yako, ni dada yako ni kila kitu kwako. Usisalimu amri kwa yoyote. Nakwenda Libya kupata silaha na msaada na nitarudi kuendelea kupambana. Kuwa hodari na ilinde Arua hadi nitakaporudi.”

Ni kweli kwamba Iddi Amin alikwenda Libya kama alivyoahidi, lakini hakurudi kama alivyoahidi.

Wakiwa mpakani mwa Uganda na Sudan, Jenerali Mayunga aliwaita askari wake, akatoa hotuba fupi akiwaambia: “Mmemfundisha Iddi Amin somo ambalo hatalisahau kamwe.” Kisha akawaamuru kurejea Koboko.

Askari wa Tanzania walikumbatiana. Vifaru na mabasi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) vikageuka na kuondoka mpakani. Hadi kufikia Jumapili ya Juni 3, 1979, askari wa Tanzania walikuwa wametembea umbali wa kilomita 12,000.

Soma zaidi: VITA YA KAGERA: Mapambano yaendelea, majeshi ya Tanzania yauteka mji wa Arua-27

Itaendelea kesho



Columnist: mwananchi.co.tz