Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

VITA YA KAGERA: Tanzania yauteka mji wa Masaka-13

32877 Pic+kagera Tanzania Web Photo

Sat, 22 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

BAADA ya kuviteka vilima vya Kikanda, Nsambya na Simba, sasa kazi iliyofuata ni kuteka miji ya Masaka na Mbarara. Vikosi vilivyoelekea Masaka havikupata tabu kama vile vilivyoelekea Mbarara. Brigedia Silas Mayunga aliyekuwa akiongoza Brigedi ya 206 ndiye aliyekutana na hali ngumu zaidi.

Kiasi cha kilomita 45 kutoka mpaka wa Tanzania, karibu na mji wa Gayaza vifaru viwili vya Tanzania vya kikosi cha Luteni Nshimani vilipigwa kombora na majeshi ya Idi Amin.

Kwa jinsi Nshimani alivyokasirika, alianza kuwakimbilia maadui waliorusha makombora hayo. Kitabu cha War in Uganda kinasema alipokuwa akiwafukuza kwenye barabara ya kuelekea ufukweni mwa Ziwa Nakivale, Luteni Nshimani aligutuka kuwa alikuwa akielekea kwenye hatari kubwa.

Karibu na kona mmoja ya barabara hiyo alikutana na mzee mmoja mwanamume aliyekuwa akipita eneo hilo. Alimsimamisha na kumuuliza kama ameyaona majeshi ya Amin maeneo hayo. Mzee alimjibu kwamba wote wameshakimbia.

Wakati Nshimani alipogeuka na kuelekea kwenye kona ya barabara hiyo, mtikisiko mkubwa wa milio ya risasi za bunduki za SMG ulitikisa dunia katika eneo hilo. Risasi hizo zilikuwa zikipigwa kutoka pande tatu.

Watanzania walikuwa wameingia kwenye mtego mbaya kuliko wowote katika vita yote ya Tanzania dhidi ya Uganda. Milio ya risasi ilidumu kwa muda fulani, na ilipotulia hatimaye, tayari Watanzania 25 walikuwa wameshapoteza maisha. Haya yalikuwa ni mauaji makubwa zaidi kwa wanajeshi wa Tanzania kuliko wakati mwingine wowote wa kipindi chote cha vita ile.

Shambulio hili lililofanywa na askari wa Idi Amin lilikuwa ni mojawapo ya yale machache waliyofanya kwa umakini mkubwa kipindi chote cha vita.

Shambulio la Ziwa Nakivale likawatia hasira majeshi ya Tanzania, lakini hawakuvunjika moyo. Wakasonga taratibu kuelekea Masaka upande wa mashariki na Mbarara upande wa magharibi. Katika njia nzima kulikuwa na mapigano karibu katika kila kitongoji—mengine madogo na mengine makubwa.

Maeneo ambayo kulikuwa na mapigano makubwa ni pamoja na miji ya Kyotera, Kalisizo, Bukeri, Sanga, Miakitele na baadhi ya maeneo mengine. Wakati wote huu kusonga mbele kulifanyika kwa tahadhari kubwa kuliko ilivyokuwa kabla ya shambulio la Nakivale.

Wanajeshi wa Jeshi la Amin wakawa wanakimbia ovyo na kufyatua risasi ovyo. Wakihofia mizinga ya Tanzania, askari wa Amin walianza kujificha kwenye miji kwa imani kuwa Tanzania ingesita kupiga mabomu maeneo ya raia na hata kama wangepiga mabomu hayo basi raia wa Uganda wangekasirishwa sana na wanajeshi wa Tanzania na hivyo kushirikiana na askari wa Amin.

Lakini hali ilikuwa kinyume. Raia walikuwa tayari wameshaikimbia miji hiyo hata kabla askari wa Amin hawajafika wala wale wa Tanzania. Kutokana na sababu hiyo, wanajeshi wa Tanzania hawakuwa na hofu ya kutumia mizinga yake kushambulia miji hiyo kwa sababu hawakuwa na hofu ya kuwapo kwa raia katika maeneo hayo.

Vikosi vilivyoelekea Masaka havikupata tabu kama vile vilivyoelekea Mbarara. Brigedia Silasi Mayunga aliyekuwa akiongoza Brigedi ya 206 ndiye aliyekutana na hali hiyo.

Kwa mujibu wa kitabu cha War in Uganda: The Legacy of Idi Amin (uk. 82), wapiganaji wa Tanzania walipofika umbali wa kilometa kama 30 kusini mwa mji wa Masaka walikutana na kijana wa Kitanzana ambaye aliwaambia alitekwa na majeshi ya Idi Amin na kupelekwa Uganda sasa alifanikiwa kutoroka na alikuwa njiani kurudi nyumbani. Walipomhoji zaidi aliwaambia wanajeshi hao kuwa ameacha zaidi ya raia 2,000 wa Tanzania katika kambi ya mateso ya Kalisizo.

Lakini walipofika Kalisizo hawakukuta hata raia mmoja wa Tanzania aliyekuwa ameshikiliwa na, badala yake, waliwakuta askari, wapata 600, wa Amin wakisubiri kushambulia. Huenda tayari walikuwa wameachiwa baada ya kupata habari kuwa majeshi ya Tanzania yanakaribia.

Askari wa Amin waliokuwa wakiwasubiri askari wa Tanzania ili wawashambulie, walianza kufanya hivyo. Lakini walipopigwa mzinga wakajikuta wameyeyuka kama samli kwenye kikaango. JWTZ haikuishia hapo.

Ikaendelea kushambulia zaidi kutokea pande tatu. Askari wa Amin wakachanganyikiwa zaidi. Walipoona hali kwao inazidi kuwa ngumu, waliobahatika kukimbia walianza kukimbia ovyo kuelekea Masaka. Zaidi ya askari 200 wa Amin waliuawa siku hiyo katika shambulio hilo moja la Kalisizo.

Walionusurika kuuawa na wakabahatika kukimbia, walikuwa wakipiga mayowe njia nzima kuelekea Masaka. Askari wa Amin ambao hawakuwa eneo la tukio, lakini wakawaona wenzao wakikimbia kwa hofu huku wakipiga mayowe, nao wakajiunga nao na kuanza kukimbia ovyo. Askari wengine waliopata habari za yaliyotukia walivunjika mioyo na wakapoteza hamu ya kuendelea na vita.

Baada ya ushindi wa Kalisizo, Jeshi la Tanzania walikuwa na nafasi nzuri zaidi za kusonga mbele kuelekea Masaka, lakini badala yake walitulia wakaanza kujipanga.

Usiku wa kuamkia Jumamosi ya Febriari 24, 1979, mji wa Masaka ukawa umezingirwa na JWTZ kwa pande tatu na, baada ya muda mfupi, brigedi za 201 na 208 zikaanza mashambulizi. Sehemu ya kwanza kushambuliwa ilikuwa ni kambi ya jeshi ya Kikosi cha Suicide kilichoachwa peke yake kulinda mji wa Masaka. Vikosi vingine vilikuwa vimetoweka kuelekea Lukaya. Walipoelemewa, kikosi cha Suicide nacho kikatoweka, kikakimbilia Villa Maria.

JWTZ walikuwa na amri ya kuiteketeza Masaka. Mji uliteketezwa. Ilipofika jioni ya Jumamosi ya Februari 24, mji wa Masaka ukawa tayari umeharibiwa vibaya, na sasa majeshi ya Tanzania yakaridhika kwamba Idi Amin ameanza kulipa gharama za kuteka ardhi ya Tanzania. Awamu ya pili ya vita ikawa imemalizika. Sasa ikaingia awamu ya tatu. Nini kilifuata baada ya Masaka kutekwa?

Tukutane toleo lijalo.

Soma zaidi: VITA YA KAGERA: Majeshi ya Tanzania yashambulia vilima vitatu Uganda-12



Columnist: mwananchi.co.tz