Siku mbili baada ya kukutana na makamanda wa Jeshi la Wananchi Novemba mosi, 1978, Mwalimu Nyerere alilitangazia Taifa kuhusu “uvamizi wa Idi Amin na uamuzi wa Tanzania wa kumpiga”. Akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwenye ukumbi wa mikutano wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, Mwalimu Nyerere alieleza uvamizi huo na jinsi Tanzania ilivyoamua kupambana na majeshi ya Idd Amin.
“Nimewaombeni mkusanyike tena hapa niwaelezeni jambo ambalo kwa sasa wote mnalijua. Lakini naona si vibaya nikieleza. Nitajaribu kueleza kwa ufupi.
“Wakati nilipokuwa ziarani Songea kuanzia juma la pili la mwezi uliopita (Oktoba), zilitangazwa habari kutoka Uganda kwamba jeshi la Tanzania limeingia Uganda na limechukua sehemu kubwa na kuua watu ovyo.
“Siku zilipotangazwa habari hizo nilikuwa nimekaribishwa chakula cha jioni na vijana wetu wa jeshi pale Songea, na nikakanusha. Na kwa kweli nikachukua nafasi hiyo kuvishutumu vyombo vya habari vya nje ambavyo vinapenda kutangazatangaza uongo wa Amin,” alisema Nyerere.
“Kila anapotangaza uongo, wao huurukia na kutangaza kama kwamba ni kweli. Huo ndio uliokuwa uongo wake wa kwanza, na aliendelea endelea.
“Baadaye akabadili sura, akaongeza uongo wa pili katika shabaha hiyohiyo kuwa Watanzania wanaua watu ovyo na kwamba wanasaidiwa na majeshi kutoka Cuba. Uongo huo nao tukaukanusha.
“Kwa hivyo, alivyozidi kusema habari hizo za uongo tuliendelea kuzikanusha na kuzipuuza. Lakini Alhamisi akatuma ndege za kivita Bukoba. Vijana wetu walizitupia risasi zikakimbia. Siku hiyohiyo ikarudi tena moja, ikaangushwa.
“Ijumaa zikaja ndege eneo la Kyaka. Zikatupa mabomu. Vijana wetu walizitupia risasi, na mbili zikaangushwa.”
Nyerere pia alizungumzia ndege za Tanzania zilizopotea uwanjani wakati zikitoka Dar es Salaam kwenda Mwanza ambazo kutokana na kasi yake zilihisiwa kuwa ni za adui na kutunguliwa. Nyerere alisema Tanzania imechoshwa na uongo huo wa Idi Amin na hivyo wameamua zikionekana ndege za kivita, zitunguliwe.
“Kwa hiyo vijana wetu wamekwishaambiwa kuwa ndege za kivita zikionekana, zipigwe. Kama vile zile za Bukoba na Kyaka zilipigwa, basi na hizi zikapigwa zilipofika Musoma. Walidhani ni za adui. Tukapoteza ndege tatu,” alisema Nyerere.
“Lakini katika mambo ya vita ajali hutokea. Na vijana hawa walishaambiwa ndege zikionekana zipigwe. Wangeziacha? Wanajuaje ni za adui? Kwa hiyo ikatokea bahati hiyo mbaya.
“Matukio haya hatukuyatangaza. Hata kule kupigwa kwa ndege za Amin hatukutangaza. Hatukutangaza kwa sababu hatukutaka jambo lenyewe kulipa uzito mno. Tulisema akiendeleaendelea kuleta ndege zake, tutaendelea kuziangusha kila zinapokuja.
“Uwezo wa kuziangusha upo, na mwenyewe alijua uwezo upo. Ni vizuri akijua yeye. Tulijaribu. Tulikuwa tunaepuka kulipa uzito jambo lenyewe ambalo mwanzo wake ni uongo kabisa wa kuzua.”
Nyerere alisema jinsi Idd Amin alivyoendelea kuidanganya dunia na jinsi Tanzania ilivyomjibu hadi alipoamua kuvamia.
“Sasa Jumatatu ndiyo akaivamia nchi yetu. Akaingiza majeshi yake kwa nguvu, nguvu kubwa. Yakachukua sehemu kubwa. Yakaingia ndani mpaka Kyaka. Hii tukatangaza kwa sababu lilikuwa ni jambo la kweli na yeye kama kawaida yake akakana akasema haikutokea hivyo,” alisema Nyerere.
“Akaendelea kusema kwamba Watanzania ndio wako Uganda, ndio wamechukua sehemu ya Uganda. Akakana ukweli huo. Lakini tukawaeleza jamaa na mabalozi walioko Dar es Salaam kuwa huo ndio ukweli.
“Huyu mtu ameivamia nchi yetu. Sasa jana ametangaza mwenyewe kwamba ni kweli majeshi yake yameivamia nchi yetu na yamechukua sehemu hiyo ya Tanzania iliyoko kaskazini mwa Mto Kagera na kwamba tangu sasa, eti sehemu hiyo ni ya Uganda na itatawaliwa kijeshi kama Uganda inavyotawaliwa.”
Alisema kauli hiyo ya Idi Amin iliisaidia Tanzania kutangaza kutokea kwa uvamizi huo.
“Sasa hiyo ndiyo hali. Tufanye nini! Tunayo kazi moja tu. Watanzania sasa tunayo kazi moja tu—ni kumpiga,” alisema Mwalimu Nyerere.
“Uwezo wa kumpiga tunao. Sababu ya kumpiga tunayo, na nia ya kumpiga tunayo. Tunataka dunia ituelewe hivyo. Kwamba hatuna kazi nyingine.
“Na tunaomba marafiki zetu wanaotuomba maneno ya suluhu, waache maneno hayo. Kuchukua nchi ya watu wengine siyo kwamba majeshi yamekosea njia na kusema kuwa sasa sehemu hiyo umeichukua na kutangaza vita kwa nchi ile nyingine. Si sisi tuliofanya hivyo. Amefanya hivyo mwendawazimu.
“Na amefanya hivyo kwa jambo ambalo aliwahi kutangaza zamani. Aliwahi kusema zamani kidogo kuwa mpaka wa haki wa Uganda na Tanzania ni Mto Kagera, na kuwa siku moja atachukua sehemu hiyo. Ametimiza hivyo.”
Nyerere aliwaomba marafiki wa Tanzania kuielewa hali hiyo na kuisaidia katika kuyaondoa majeshi ya Uganda na kwamba wale waliokuwa wakitaka suluhu haitawezekana.
“Hatukupenda kufanya hivyo. Maadui zetu ni mabeberu, na kwa hivi sasa wako Kusini. Serikali ya Afrika, hata kama hatupendi matendo ya viongozi wao, hatuwahesabu kama adui wetu,” alisema Nyerere.
“Na kama Amin angekuwa amesema tu kwamba Tanzania ni adui wetu, sisi tungeendelea kumpuuza kama ni maneno hayo. Lakini kafanya kitendo cha uadui, hatuwezi.
“Ameingia Tanzania mwenyewe. Na mtu huyu ni mshenzi. Ameua watu wengi sana. Kwa hiyo nasema tuna kazi moja tu. Tutampiga. Vijana wetu wako mpakani sasa hivi. Wako kule. Wako kule na mapambano yanaendelea.
“Sasa hayo si mapambano ya TPDF peke yake, ni yetu wote. Kwa hiyo ninachowaombeni wananchi, hiyo kazi iliyoko mbele yetu muielewe.
“Pili, tuwasaidie vijana wetu. Kila mtu kwa mahali alipo. Tutaendelea na kila mapambano yanavyoendelea kueleza nini la kufanya na nani afanye nini.
“Tutaelezana wakati wote huo mpaka tumemuondoa huyu nyoka katika nyumba yetu. Na tunawaomba mtulie. Katika mambo haya ya vita, na hasa kama watu mlikuwa mmezoea amani mnaweza kubabaika sana.
“Msibabaike, tulieni. Fanyeni kazi kama kawaida. Lakini mjue vitendo hivyo kazi yake ni hiyo moja; kumpiga mshenzi huyu aliyekuja katika nchi yetu.”
Soma zaidi> VITA YA KAGERA: Wanajeshi wavamia Kagera wapora, wabaka wananchi-2
Soma zaidi> VITA YA KAGERA: Luteni alivyoziingiza vitani Tanzania na Uganda-1