Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

VITA YA KAGERA: Mji wa Lukaya, eneo la maafa kwa Tanzania-15

33150 Pic+kagera Tanzania Web Photo

Mon, 24 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

MPANGO wa kuingia Lukaya ulizishirikisha brigedi tatu ambazo ni 201, 207 na 208. Brigedi ya 201 iliyoongozwa na Brigedia Imran Kombe ilikuwa imejaa wanamgambo ambao wengi wao walikuwa hawajawahi kukabiliana na mapambano ya silaha za moto. Kile kikosi cha Waganda waliompiga Amin kilichoongozwa na David Ojok kiliingizwa pia katika brigedi hii.

Alfajiri Jumamosi ya Machi 10, 1979 vikosi vya Tanzania viliushambulia mji wa Lukaya kwa makombora na kuuchakaza. Kisha wakasubiri kupambazuke. Lakini bila kutambua, kikosi kikubwa cha jeshi la Libya na askari wa Idi Amin walikuwa wamekusanyika upande wa Kaskazini wa Kinamasi na walikuwa wamepewa amri na Idi Amin mwenyewe kuurejesha mji wa Masaka mikononi mwa Uganda ndani ya saa tatu au chini ya hapo.

Askari wa Libya walikuwa wameingia Uganda jana yake, wakiwa na ndege kadhaa ambazo pia zilibeba silaha ndogo na kubwa kama vifaru na mizinga, zilijaza mafuta Nairobi, Kenya kabla ya kuingia Uganda.

Ndani ya ndege hizo yalikuwamo pia magari ya kijeshi kama Land Rover. Lakini silaha iliyotisha zaidi ni “Katushka” ambayo ilitumika kufyatua makombora makubwa. Silaha hiyo ilitengenezwa Korea Kaskazini na haikuwa imetumiwa vitani kabla ya hapo. Jeshi hilo lilikuwa na maelfu ya askari wa Libya na waasi wachache wa PLO. Lilisemekana kuwa ni kikosi kikali katika vita.

Jeshi la Amin na Gaddafi liliingia kazini saa za magharibi wakati giza lilipoanza kutanda. Walipoona brigedi ya Imran Kombe, askari wa Libya wakaanza kufyatua roketi za Katushka. Ingawa roketi hizo hazikuwapiga wanajeshi wa Tanzania, milio mikubwa iliyotokana nazo na miale mikali na mwanga uliotokana nazo zilivyopita juu ya vichwa vya wapiganaji wa Tanzania ilitosha kabisa kuwatia kiwewe wapiganaji wa brigedi ya Kombe ambao wengi hawakuwahi kukutana na mapigano ya risasi, achilia mbali makombora makali kama Katushka.

Baadhi ya wapiganaji katika brigedi hiyo walikimbia. Hata waliobaki, walijikuta hawawezi kufanya chochote. Hata hivyo, hakuna hata mmoja aliyeuawa. Lakini Amin sasa akawa ameurejesha na kuukalia mji wa Lukaya.

Kama askari wa Amin na wale wa Libya wangeendelea na mashambulizi makali zaidi, wangeweza kuyasogeza majeshi ya Tanzania na hata kuutwaa mji wa Masaka kwa sababu kwa wakati huo kilichokuwako katikati ya mji wa Lukaya na Masaka ni vifaru vitatu tu vya Tanzania ambavyo visingeweza kupambana na Katushka ya Libya. Lakini kwa kuzubaishwa na kile walichoona kuwa ni ushindi wa kuurejesha mji wa Lukaya, wao waliamua kupumzika Lukaya.

Mara moja amri ikatolewa kwa vikosi vyote vya Tanzania kubadili mbinu za kivita ili kuichukua tena Lukaya kabla hali haijawa hatari zaidi. Brigedi ya 208, ambayo sasa ilikuwa umbali wa kilomita 60 Kaskazini-Magharibi mwa Lukaya, ilipewa amri ya kugeuka na kurudi kuelekea Lukaya kwa kasi yoyote iliyowezekana na kuvunja mawasiliano ya barabara kati ya majeshi ya Amin na mji wa Kampala.

Vifaru vya Tanzania viliamriwa kusonga mbele na kuanza kushambulia vikali zaidi. Wakati madereva wa vifaru hivyo walipoanza kuonesha hali ya kusita kwenda kushambulia bila kuwa na askari wa kikosi cha miguu, Jenerali Msuguri alimtuma ofisa mwandamizi wa JWTZ kwenda uwanja wa vita kuhakikisha kuwa amri yake inatekelezwa.

Kikosi cha Amin kikisaidiwa na Libya kilikuwa na silaha kali na kingeweza kushinda katika mchezo lakini hakikuwa kimejipanga.

Kwenye njia ya kuelekea Lukaya kulikuwa na Watanzania, askari wa kuikomboa Uganda, majeshi ya Idi Amin pamoja na askari wa Libya. Watu walikuwa wakipishana. Lakini kwa kuwa usiku huo mwanga pekee uliokuwapo ni mbalamwezi, ilikuwa ni vigumu kutambuana.

Kama vile ni aina fulani ya kituko, kikundi cha Kikosi Maalumu (cha kuikomboa Uganda) kilichokuwa kinaongozwa na David Ojok nacho kilipita barabara hiyo kama walivyopita askari wa Amin na wale wa Tanzania na wale wa Libya. Kwa wakati mmoja wote hawa walipita barabara hiyo bila kutambuana.

Askari wa Ojok, wakati wakiwa katika barabara hiyo, waliweza kuwasikia watu wakizungumza Kiswahili na kuwachukulia kuwa hao walikuwa marafiki. Ghafla mmoja miongoni mwao akazungumza Kiluo—lugha ambayo haitumiki Tanzania.

Alisikika akisema “Subiri kupambazuke na tutawaponda hawa Waacholi wajinga.” Kusikia hivyo, Ojok akaamuru wapiganaji wake washambulie. Kwa sababu ya kiza na mwanga hafifu wa mbalamwezi hawakuwa na hakika kama walilenga shabaha zao. Katika mapigano ya usiku huo mmoja, Watanzania wanane na askari mmoja wa Ojok walipoteza maisha.

Wakati hayo yakiendelea, Brigedi ya 208 ilikuwa ikisonga mbele kwa kasi kuelekea Lukaya. Kulipokaribia kupambazuka ilianza kushambulia na kuwarudisha tena nyuma askari wa Amin na wale wa Libya. Mizinga mikubwa ya Tanzania ikaanza kuwasambaratisha Walibya. Wanajeshi wa Idi Amin waliogopa sana kiasi kwamba hawakuthubutu hata kufyatua risasi. Kwa jinsi askari wa Libya walivyochanganyikiwa, walilazimika kukimbia.

Mashambulizi yalipokoma baadaye, askari wa Tanzania walihesabu maiti wakakuta karibu askari 500 wa adui wameuawa katika tukio hilo moja. Miongoni mwa hao waliouawa, zaidi ya 200 walikuwa ni askari wa Libya. Ni askari mmoja tu wa Libya ambaye hakuuawa. Alikamatwa na kuchukuliwa mateka.

Pamoja na ushindi huo, makamanda wa JWTZ waliichukulia Lukaya kuwa ni sehemu ya maafa kwa Watanzania. Kama isingekuwa ni ama uzembe au kutokujimudu kwa jeshi la adui, kwa hakika jeshi la Tanzania lingeondolewa kabisa katika ardhi ya Uganda.

Lakini wakati ikikabiliana na matatizo ya Lukaya, jeshi la Tanzania pia lilikuwa linakabiliwa na hali ngumu katika eneo la Sembabule ambalo likikuwa kiasi cha kilomita 60 Kaskazini-Magharibi mwa mji wa Masaka.

Nini kilikuwa kinaendelea huko Sembabule? Tukutane toleo lijalo.



Columnist: mwananchi.co.tz