Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

VITA YA KAGERA: Majeshi ya Tanzania yashambulia vilima vitatu Uganda-12

Fri, 21 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

KABLA ya kupambazuka askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) walianza kushambulia vilima vya Kikanda, Nsambya na Simba. Majeshi ya Idi Amin yalijua wanajeshi wa Tanzania wangeingia Uganda kushambulia, lakini hawakujua kwa hakika shambulio hilo lingefanyika lini na wapi na kwamba lingefanyika kutokea upande gani.

Kwa jinsi mashambulizi yalivyokuwa makali na ya kushtukiza, Redio Uganda ilitangaza kuwa Uganda imevamiwa na majeshi ya Tanzania na Cuba. Ingawa Cuba ilikanusha habari hizo, Idi Amin aliendelea kuzisisitiza kiasi kwamba jarida la To the point international liliandika, “Dikteta wa Uganda anapiga kelele”.

Kwa mujibu wa kitabu cha War in Uganda, usiku mmoja kabla ya kushambulia vilima vya Simba, baadhi ya makamanda wa brigedi walikutana kwa mazungumzo na kupata kinywaji. Kwa wakati wote huu, kila upande—Tanzania na Uganda—ulikuwa ukijaribu kunasa mawasiliano ya upande wa pili.

Baada ya kupata kinywaji, makamanda wa brigedi walirejea katika vituo vyao na kuanza kucheza kitimbi. Kwa mujibu wa kitabu hicho, makamanda hao walianza kuwasiliana wenyewe kwa wenyewe kwa kutumia redio za upepo.

Mmoja akauliza, “Wacuba wameshakaa tayari upande wa kulia?” Halafu akajibiwa na askari mwingine: “Tayari afande.” Yule wa kwanza akauliza tena, “Waisraeli wameshajiweka tayari upande wa kushoto?” Halafu akajibiwa, “Wako tayari afande.” Kisha akaendelea, “Na je, Wamarekani nao wameshakaa tayari eneo la kati?” Akajibiwa, “Wako tayari afande.” Kisha akasema, “Haya. Twende kazi.”

Majeshi ya Idi Amin yalikuwa yanafuatilia mawasiliano hayo ya redio. Baada ya kusikia mawasiliano hayo, ndani ya dakika chache majeshi ya Uganda yakaanza kulikimbia eneo hilo mmoja baada ya mwingine.

Katika mawasiliano ambayo JWTZ iliyanasa kutoka Uganda walisikia kamanda wa vikosi vya eneo hilo akiwasiliana na makao makuu mjini Kampala akisema, “I see! Kweli wanakuja sasa.” Kisha sauti kutoka Kampala ikajibu, “Sawa. Wapigeni.” Kamanda aliyekuwa akiongea katika mawasiliano hayo alikuwa eneo la vita akiwasiliana na aliyepo makao makuu mjini Kampala. Alipoambiwa wapigeni, yeye akajibu, “Tubadilishane. Wewe njoo huku (vitani) na mimi nije huko (ofisini).”

Siku iliyofuata Idi Amin, kwa kuyaamini maneno ya makamanda wa brigedi waliotaja Wamarekani, Waisraeli na Wacuba, aliingia kwenye studio za Redio Uganda na kuanza kutangaza kuwa nchi yake imevamiwa na Watanzania, Waisraeli, Wacuba na Wamarekani.

Kusikia taarifa hizo, vyombo vya habari vya dunia vikashangazwa na madai ya Amin. Ingawa ilikuwa ni uongo kuwa kulikuwa na Wacuba, Waisraeli na Wamarekani walioivamia Uganda, ukweli ni kwamba Idi Amin alizipata habari hizo kutoka kwa wanajeshi wake ambao nao waliamini kile kitimbi kilichochezwa na makamanda wa JWTZ.

Ni kweli kwamba makamanda wa JWTZ ndio waliosema hayo, na hayo waliyoyasema yakanaswa na redio za mawasiliano za jeshi la Amin ambalo baada ya kuziamini walizipeleka kwa Amin ambaye naye aliziamini na kuitangazia dunia.

Lakini Meja Jenerali David Msuguri, ambaye kwa sasa ndiye alipokea kijiti kutoka kwa Brigedia Jenerali Tumainieli Kiwelu kushambulia majeshi ya Amin, alikemea kitendo cha makamanda hao. Hata hivyo kitimbi hicho kilifanikiwa sana kwa sababu kiliyatia kiwewe majeshi ya Amin.

Mashambulizi makali yakafanywa na JWTZ katika vilima vya Kikanda, Nsambya na Simba. Majeshi ya Idi Amin yalielemewa katika maeneo hayo. Mizinga mikubwa ya Tanzania ikavunja nguvu ya jeshi la Amin.

Upande wa Kaskazini mwa vilima ambako majeshi ya Amin yangeweza kupata mwanya wa kukimbia ulikuwa umezingirwa na brigedi za 201 na 208. Majeshi ya Amin hayakujua yalivyozingirwa.

Walishtukia tu wanashambuliwa na wakastaajabu zaidi kuwa hata walikokuwa wanakimbilia nako kulikuwa kumezingirwa na wapiganaji wa JWTZ. Katika shambulizi hilo moja la siku hiyo moja peke yake, kiasi cha wanajeshi 250 wa Idi Amin waliuawa.

Walipochunguza maeneo waliyoshambulia, makamanda wa Tanzania walitambua kuwa wenzao wa Uganda hawakujua namna ya kutumia vizuri maeneo yaliyoinuka kukabiliana na adui.

Katika kilima cha Nsambya, JWTZ ilikuta handaki moja na simu moja tu ya mawasiliano. Katika eneo la kilima cha Kikanda Watanzania walistaajabu sana walipogundua mizinga mikubwa ambayo makombora yake ndiyo yaliyokishambulia kikosi cha Luteni Kanali Salim Hassan Boma eneo la Mutukula, ilikuwa nyuma ya mlima badala ya juu ya mwinuko.

Wakati mapambano yakiendelea kwenye vilima hivyo, ndege za kivita za Amin zilijaribu kusaidia wanajeshi wake lakini bila mafanikio. Ndege hizo zilishindwa kuokoa jahazi kwa sababu kufikia wakati huo ndege nyingi za Uganda zilikuwa zimeshatunguliwa na JWTZ.

Tangu wapiganaji wa JWTZ walipovuka mpaka na kuingia ardhi ya Uganda Jumamosi ya Januari 20, 1979 na kuteka vilima vilivyotajwa hapo juu pamoja na kiwanja cha ndege za kijeshi cha Lukoma kilichoangukia mikononi mwa JWTZ Jumanne ya Februari 13, Tanzania ilikuwa imeshaangusha ndege 19 za Jeshi la Uganda.

Kilichoanza kumkatisha tamaa Idi Amin ni ile kasi ya Tanzania kuangusha ndege za jeshi lake. Kilichomtia kiwewe zaidi ni kasi ya kukamata silaha kutoka kwa majeshi yake. Baadhi ya marubani waliosikia ndege zao zilivyokuwa zikitunguliwa na majeshi ya Tanzania waliingiwa na kiwewe na hivyo wengine walitoroka kazini.

Kilichofanya Jeshi la Anga la Uganda lifikie katika hali mbaya kiasi hicho ni upungufu—na pengine ukosefu wa wataalamu, upungufu wa vipuri vya ndege na marubani wa ndege za kijeshi kukimbia.

Kwa hiyo wakati mji wa Masaka ukianguka mikononi mwa JWTZ tayari Jeshi la Anga la Idi Amin lilikaribia kuwa mahututi.

Hata hifadhi yake ya silaha nayo ilianza kuwa na mushkeli. Kwenye kilima cha Simba, JWTZ ilikamata vifaru sita.

Baadaye vifaru hivyo vilianza kutumiwa na jeshi la Tanzania. Silaha mbalimbali kuanzia bunduki za kawaida hadi mizinga mikubwa ilikamatwa eneo hilo.

Baada ya kukamilisha kazi ya kuteka vilima vya Kikanda, Nsambya na Simba sasa njia ikawa imesafishwa tayari kwa kuushambulia mji wa Masaka. Nini kilitokea?

Tukutane toleo lijalo



Columnist: mwananchi.co.tz