Kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi hakujua uwezo wa kijeshi iliokuwa nayo Tanzania. Askari wake walipata tabu kubwa walipokuwa Uganda.
Jarida la Africa Research Bulletin la Aprili 1—30, 1979 linasema katika mapigano ya siku mbili ya Entebbe, kiasi cha askari 400 wa Libya waliuawa na wengine zaidi ya 40 walichukuliwa mateka.
“Tanzania pia ilikamata kiasi kikubwa cha silaha nzito za Libya na ndege kadhaa za kijeshi za Jeshi la Uganda,” linasema.
Kitabu cha War in Uganda kinasema mradi wa Muammar Gaddafi nchini Uganda uligeuka kuwa ni maafa kwa askari wake.
Makumi ya askari wa Libya waliojeruhiwa walipelekwa katika Hospitali ya Mulago mjini Kampala na baadaye waliondolewa nchini humo wakitokea kwenye Uwanja wa Ndege wa Nakasongola. Silaha kali za kivita zikiwamo zile za kisasa zikaangukia mikononi mwa askari wa JWTZ.
Askari wapatao 60 wa Libya waliotekwa na askari wa JWTZ, kwa mujibu wa kitabu cha Idi Amin Speaks: An Annotated Selection of His Speeches, walipelekwa Tanzania.
Hata hivyo waliachiwa baada ya miezi mitatu na waliobakia waliachiwa baada ya miezi tisa.
Kitabu cha An Encyclopedic Dictionary of Conflict and Conflict Resolution, 1945-1996 cha John E. Jessup katika ukurasa wake wa 769 kinasema, “Mei 15, 1979, Libya iliilipa Tanzania Dola milioni 40 ili iwaachie mateka wa kivita wa waliokamatwa wakati wa mapigano nchini Uganda.”
Lakini kitabu cha War in Uganda: The Legacy of Iddi Amin katika ukurasa wake wa 122 kimeandika: “Hadithi za kwamba Nyerere aliwauza mateka kwa Gaddafi hazina ushahidi wowote. Gaddafi hakuonekana kama anajali ikiwa mateka watarudi nyumbani au hawatarudi. Nyerere aliahidi ‘Libya itawapata mateka wote. Hatutawauza Hatutafanya biashara ya kuuza wanadamu kwa ajili ya fedha. Sisi ni maskini sana. Tunajali sana heshima ya utu.”
Hata baada ya kuonekana dhahiri kuwa Gaddafi hakuweza kumuokoa Iddi Amin, bado Amin alizililia nchi za Kiarabu akitaka zimsaidie kupambana na Tanzania. Katika matangazo fulani ya redio alilalama kuwa, “Tanzania na rafiki zake Wayahudi” wanapambana na Serikali ya Uganda.
Akasema: “Huu ni wakati ambao nchi za Kiarabu zinapaswa kuisiadia Uganda kifedha na kwa mali.” Lakini Nyerere, kwa upande mwingine, alijitahidi kuhakikisha kuwa dunia haitaona kuwa haya ni mapambano ya Waafrika dhidi ya Waarabu.
Hadi kufika jioni, kikosi cha Luteni Kanali Salim Hassan Boma kikawa kimeiteka Entebbe. Askari wa Iddi Amin walikuwa wamekwishakimbia wakiwaacha wenzao wa Libya wakipata tabu.
Asubuhi ya Jumapili ya Aprili 8, 1979 askari wa Tanzania walianza kuvinjari katika mji wa Entebbe. Walipofika katika kanisa moja walikuta kiasi cha askari 200 wa jeshi la anga la Iddi Amin wamejikunyata, wakiwa wamevalia nguo za kiraia, wakiwa wamejiandaa kujisalimisha.
Maduka kwenye Uwanja wa Ndege wa Entebbe, yalikuwa yameshaporwa na askari wa Iddi Amin wakati wakikimbia. Kulikuwa na ndege tisa za kivita aina ya MiG-21 ambazo kwa mujibu wa kitabu cha Three Thousand Nights of Terror, askari wa Tanzania walidai kuwa hiyo ni zawadi ya vita. Ndege hizo zilichukuliwa na kupelekwa Tanzania. Lakini wakati zikiwa zinatua, moja ilianguka na kumuua rubani wake.
“Watanzania sasa walikuwa wamedhibiti vita na Ikulu ya Entebbe ilikuwa imeangukia mikononi mwao... Walikuta Ikulu ikiwa imejaa silaha na bidhaa nyingi kama redio, pombe, televisheni,” kimeaendika kitabu cha Three Thousand Nights of Terror.
Sasa askari wa Tanzania walikuwa wanavinjari ndani ya Ikulu ya Entebbe. Meja Jenerali David Msuguri aliwasili Ikulu ya Entebbe saa 3:30 asubuhi.
Mpango wa mwisho wa kuivamiana na kuiteka Kampala ulifanyika kwenye chumba cha chakula cha Ikulu ya Entebbe. Batalioni ya 19 ya Brigedi ya 208 iliyokuwa chini ya Kanali Benjamin Msuya ikapewa jukumu la kuiteka Kampala ambayo sasa ilikuwa umbali wa kama kilomita 35.
Sasa huu ulikuwa ni mpango wa jeshi la nchi moja kuteka makao makuu ya nchi nyingine. Ni historia ya kipekee sana katika Bara la Afrika. Tangu mwanzo wa vita, hakuna askari hata mmoja chini ya Msuya ambaye alikuwa amepoteza maisha kwenye mapigano, na sasa alikuwa amenuia kuiteka Kampala bila kumpoteza askari wake hata mmoja.
Brigedi za 201, 207 na 208 zilijipanga kwa kazi hii muhimu. Wakati mipango ya kuiteka Kampala ikifanyika katika Ikulu ya Entebbe, Idi Amin naye alikuwa mjini Kampala na maofisa wa jeshi lake wakipanga namna ya kuulinda mji huo.
Mapambano makali kati ya askari wa Amin na wale wa Tanzania yalifuata. Hali ya hewa ilikuwa mbaya na mvua ilikuwa ikinyesha bila kukoma. Ingawa mvua ilikuwa inanyesha na askari wa JWTZ wakiwa wamelowa chapachapa, ari yao ilionekana kuwa juu sana.
Baada ya tabu yote ya mapambano ya usiku kucha kuelekea Kampala, asubuhi Msuya na kikosi chake walifika mahali wakafungua redio kusikiliza sauti ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) wakasikia taarifa kutoka Nairobi kwamba waandishi wanne wa habari, raia wawili wa Sweden na wawili wa Ujerumani Magharibi, wanaaminika kuwa wameuawa na askari wa Iddi Amin walipokuwa wakijaribu kuvuka Ziwa Victoria kwa mashua wakitokea Kenya kwenda kuandika habari za vita nchini Uganda.
Baadaye ilijulikana kuwa waandishi hao ni Arne Lemberg wa gazeti la Sweden liitwalo Expressen, Karl Bergman wa gazeti jingine la Sweden linaloitwa Svenska Bagvladet, Hans Bolinger ambaye ni mpigapicha wa shirika la habari la Gamm na Wolfgang Steins wa majarida ya Stern na Geo.
Waandishi hawa waliuawa na askari wa Amin kwa kupigwa risasi. Walikodi mashua ndogo kutoka Bandari ya Kisumu ambayo waliitumia kuvuka ziwa, lakini walipofika upande wa Uganda wakajikuta wameangukia kwenye mikono ya askari wa Amin.
Soma zaidi: VITA YA KAGERA: Mashambulizi yaingia katika jiji la Entebbe -19
Itaendelea kesho