Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

VITA YA KAGERA: Gharama za vita na waliouawa-29

Mon, 7 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kwa kuwa kila chenye mwanzo hakikosi kuwa na mwisho, Vita ya Kagera nayo ilikuwa na mwisho wake. Ilimalizika hatimaye. Lakini haikumalizika Aprili 11, 1979 baada ya kukombolewa kwa jiji la Kampala, bali ilimalizika Juni 3, 1979 kwa kukombolewa kwa mji wa Arua, ambao ni nyumbani kwa Iddi Amin.

“Juni 3, (1979) majeshi ya Tanzania yalifika kwenye mpaka wa Uganda na Sudani, na vita ikaonekana imemalizika,” kinasema kitabu ‘Arms and Warfare: Escalation, De-escalation, and Negotiation’ cha Michael Brzoska na Frederic Pearson.

“Utawala wa kifashisti wa Iddi Amin ulikoma Aprili 11, (1979) baada ya Jiji la Kampala kuanguka (lakini vita haikumalizika baada ya kutekwa kwa kampala.) Baada ya kukamatwa kwa mji wa Arua, kijiji cha nyumbani kwa Amin Juni 3, vita iliyodumu kwa miezi tisa ikamalizika,” kinaandika kitabu ‘From Jerusalem to the Lion of Judah and Beyond: Israel’s Foreign Policy in East Africa’ cha Steven Carol.

Jarida ‘America and the World 1979’ likaandika baada ya mji wa Arua kunyakuliwa “vita ikatangazwa kumalizika rasmi.”

Hadi kufikia Jumapili ya Juni 3, 1979, wanajeshi wa Tanzania walikuwa wameshatembea kilomita 12,000 kwenye uwanja wa vita tangu ilipoanza Oktoba, 1978. Tanzania ilishinda vita hiyo na kumwondoa Amin madarakani, lakini ikabakiwa na gharama kubwa za kulipa.

Gharama ambayo Tanzania ilitumia katika vita hiyo ni dola milioni 500 za Marekani. Waandishi wa kitabu ‘Development Centre Studies: Conflict and Growth in Africa Kenya (Volume 2)’, Klugman Jeni, Neyapti Bilin na Stewart Frances katika ukurasa wa 72 wameandika:

“Vita dhidi ya Uganda iliongeza matumizi kwenye usafiri na ulinzi kutoka asilimia 12.3 (za pato la ndani) za mwaka 1976/77 hadi asilimia 24.4 katika mwaka wa fedha wa 1977/78... Vita ya Uganda iliigharimu Tanzania kiasi cha dola za Marekani milioni 500 (kiasi cha asilimia 15 ya Pato la Taifa la mwaka 1978).”

Kitabu ‘Agriculture in Tanzania Since 1986: Follower or Leader of Growth?’ kinasema ingawa uchumi wa Tanzania uliimarika sana mwaka 1976, kuimarika huko kulikuwa kwa muda mfupi tu. Kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mwaka 1977 kulisababisha biashara kudorora, lakini kilichofanya hali kuwa mbaya zaidi ni hii Vita ya Kagera.

Kuanzia hapo, hali nzuri ya uchumi wa Tanzania haikutulia tena. Tanzania “ilizidi kutumbukia kwenye madeni,” kinasema kitabu ‘The Rough Guide to Tanzania’ cha Jens Finke (uk. 719).

“Nyerere alijikuta katika hali ngumu na mawazo yake ya kijamaa. Mbali na siasa ya ujamaa na kujitegemea, Tanzania ikaanza kuwa tegemezi kuliko ilivyokuwa awali. Uchumi ulikuwa umeanguka. Mazao ya kilimo hayakutosheleza mahitaji ya chakula na uchumi ukaelemewa na madeni … theluthi moja ya bajeti yote ya Tanzania ikategemea mikopo kutoka kwa nchi wafadhili na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF),” anaandika Jens Finke katika kitabu chake, ‘The Rough Guide to Tanzania’.

Kitabu ‘War in Uganda: The Legacy of Idi Amin’ kinasema askari wa Tanzania waliouawa katika mapigano kwenye vita hiyo ni 373. Kwa mujibu wa gazeti ‘Daily Monitor’ la Uganda la Jumapili ya Aprili 27, 2014, askari 93 miongoni mwa hao 373 waliuawa na jeshi la adui lakini wengine walifariki dunia kutokana na ajali na majanga ya asili. Jeshi la Umoja wa Kuikomboa Uganda (UNLA) lilipoteza askari wake 150.

Kwa mujibu wa ‘Daily Monitor’, askari wa Libya nao waliokufa kwa wingi katika Vita ya Kagera. Kiasi cha askari 600 miongoni mwa 3,000 waliotumwa kwenda Uganda kumsaidia Amin waliuawa. Lakini waliokufa kwa wingi kuliko askari wa upande wowote ni wale wa Uganda.

Amin alipoteza zaidi ya askari 1,000. Katika ukurasa wa 567, kitabu ‘Warfare and Armed Conflicts: A Statistical Encyclopedia of Casualty and Other Figures, 1492—2015’ cha Micheal Clodfelter kimeandika kuwa “takribani raia 1,500 wa Tanzania na 500 wa Uganda waliuawa” katika vita hiyo.

Raia hao wa Tanzania waliuawa wakati majeshi ya Amin yalipovamia Kagera, lakini raia wa Uganda waliouawa ilikuwa ni wakati vita ikiendelea na waliuawa ama kwa bahati mbaya au kwa makusudi wakati wa mapambano.

Kutokana na ushindi wa Tanzania dhidi ya Amin, Rais wa Tanzania alisema amejifunza mengi sana kuhusu vita kuliko wakati mwingine wowote katika maisha yake. “Nachukia vita sasa kuliko nilivyoichukia siku zote kwa sababu sasa naijua zaidi kuliko nilivyoijua mwanzo,” alisema Nyerere.

Alipoulizwa kuhusu Serikali ya Uganda, Nyerere alisema “Hatupendi kujihusisha sana na mambo ya ndani ya Uganda.” Lakini ukweli ni kwamba alishindwa kuacha kujihusisha kwa sababu bado Serikali ya Uganda haingeweza kufanya chochote bila kumshirikisha.

Kitabu ‘Uganda Since the Seventies’ cha Godfrey Mwakikagile kinamkariri aliyepata kuwa Rais wa Uganda, Godfrey Binaisa akisema: “Kati ya mwaka 1979 na 1980 Nyerere alikuwa (kama) Rais wa Uganda... Hata kama unataka kupiga chafya au kusogeza mguu wako lazima umjulishe Nyerere...”

Lakini pamoja na yote hayo, Watanzania na Serikali yao ndio waliolipa gharama kubwa ya vita hiyo. Ingawa hivyo, Meja Jenerali Benjamin Msuya, ofisa mwandamizi wa JWTZ aliyeiteka Kampala, alisema pamoja na gharama zote hizo vita hiyo ilikuwa ya lazima kupigana.

Alhamisi ya Aprili 12, 2007 gazeti LA ‘Daily Nation’ la Kenya likaripoti kuwa Uganda imeilipa Tanzania dola za Marekani milioni 67 kama fidia ya hasara ambayo iliipata kutokana na vita hiyo.

Gazeti hilo, likimkariri mkurugenzi wa mawasiliano wa Benki Kuu ya Uganda, Juma Walusimbi, akithibitisha kumaliza kuilipa Tanzania deni lake.

Je, Serikali mpya ya Uganda iliweza kuendelea bila kuhitaji msaada wa Tanzania?

Itaendelea….



Columnist: mwananchi.co.tz