Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

VITA VYAKAGERA: Vita yaingia awamu ya tatu-14

33030 Vita+pic Tanzania Web Photo

Sun, 23 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

WANAJESHI wa Tanzania walipokuwa wamejipumzisha katika miji ya Masaka na Mbarara waliyoiteka walikuwa pia wakichora mpango wa awamu ya tatu ya vita. Lakini Rais Julius Nyerere, kwa kuhofia lawama za kimataifa alitaka jeshi la Tanzania lisijipeleke mbele sana bali liwaache waasi wa Serikali ya Idi Amin wafanye hivyo halafu JWTZ ije nyuma yao.

Hapo ndipo walipokuja kuingizwa akina Yoweri Kaguta Museveni, ambaye alipewa eneo la Mbarara ambako angewafundisha wapiganaji wake na Paulo Muwanga akapelekwa Masaka. Ingawa Muwanga ni wa kabila la Baganda kama wakazi wa Masaka, alionekana zaidi kuwa ni mtu wa Dk Milton Obote. Baada ya muda mfupi Museveni alifanikiwa kupata wapiganaji kiasi cha 2,000 kutoka Mbarara.

Wakati haya yakifanyika, JWTZ nayo ilikuwa inajipanga upya kutokana na hali ilivyokwenda. Ingawa tayari walikwishateka miji ya Masaka na Mbarara, Idi Amin bado alikuwa madarakani na alikuwa mjini Kampala. JWTZ ikaanza safari ya kwenda Kampala aliko Amin.

Brigedi mbili za Minziro na ya 206 zikaungana kuunda kikosi kazi. Wakati huu ndipo Silas Mayunga alipopandishwa cheo kutoka brigedia na kuwa meja jenerali, kisha akakabidhiwa kikosi kazi hicho. Brigedia Roland Makunda, ambaye alikuwa mkuu wa jeshi dogo la maji alikabidhiwa kusimamia Brigedi ya 206, na Brigedia Ahmed Kitete akakabidhiwa Brigedi ya Minziro.

Baadaye kikosi kKazi kikagundua kuwa Kikosi cha Simba ambacho walikishambulia hawakukiteketeza chote. Baada ya kuukimbia mji wa Mbarara kikosi hicho pamoja na kingine kutoka Kambi ya Mountains of the Moon, walikuwa wamekimbilia Kaskazini mwa mji huo kujiimarisha.

Walishtukiwa baada ya kuanza kuwarushia mabomu wanajeshi wa Tanzania. Lakini JWTZ ilipojibu mapigo, walitoweka.

Jumatatu ya Machi 19, 1979 Redio Uganda iliripoti kuwa Idi Amin aliwatembelea wanajeshi wake “...walioko mstari wa mbele eneo la Mbarara...” na kujadiliana “mambo mengi” na makamanda wa vikosi vya Simba na Chui (Tiger) na kwamba walipanga “mikakati mipya ya kuwang’oa kabisa maadui kutoka ardhi ya Uganda.”

Lakini baadaye ilibainika kwamba redio hiyo ilitangaza uongo. Jambo hilo halikutokea. Lakini angalau hicho kikosi cha Simba kiliendelea kupigana huku kikikimbia. Divisheni ya 20 ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania, ambayo ilikuwa inaelekea Uganda, ikakumbana na tatizo jingine la miundombinu wakati kinakaribia eneo la Lukaya, kiasi cha kilomita 40 Kaskazini mwa mji wa Masaka.

Barabara yenye umbali wa kiasi cha kilomita 20 ilikuwa imeharibika vibaya. Kutokana na mvua iliyonyesha barabara hiyo ilijaa madimbwi makubwa ya maji na matope. Hakuna gari lolote lililoweza kupita barabara hiyo, mjia pekee ya kufika huko na kwa kutumia barabara hiyo.

Jijini Dar es Salaam bado Nyerere alikuwa anakuna kichwa. Aiteke Kampala na kumkamata Idi Amin halafu avumilie masuto ya jumuiya ya kimataifa? Au aepuke masuto hayo lakini arudishe majeshi yake nyuma na amwache Idi Amin akiendelea kutawala Uganda?

Idi Amin alijua mpango wa Tanzania wa kuiteka Kampala. Ilisemekana kuwa baadhi ya wanamkakati wake wa kivita walimshauri kuwa ili Kampala isitekwe [kwa urahisi] kama Masaka na Mbarara basi walipaswa kuharibu maeneo fulani ya barabara eneo fulani Kaskazini mwa Lukaya ili kuvunja mawasiliano ya barabara.

Waliambiana kuwa kwa kufanya hivyo kungeyachelewesha zaidi majeshi ya Tanzania kufika Kampala na hivyo majeshi ya Idi Amin yangepata muda mzuri zaidi wa kujipanga upya kukabiliana na maadui. Lakini Idi Amin hakukubaliana na pendekezo hilo, akitoa hoja kwamba ikiwa watavunja madaraja ili Watanzania wasivuke, hatimaye hata yeye mwenyewe hangeweza kuvuka kuwakimbia majeshi ya Tanzania kutoka kwenye ardhi ya Uganda.

Imani ya Idi Amin ya kuwafukuza majeshi ya Tanzania kutoka Uganda ilikuwa kwa kiongozi wa kijeshi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi. Tangu alipopashwa habari kuwa majeshi ya Tanzania yamevuka mpaka na kuingia Uganda, kila mara alikuwa katika mawasiliano na Gaddafi ambaye aliamini kuwa Uganda ni nchi ya Kiislamu ambayo imevamiwa na jeshi ya nchi ya Kikristo.

Kwa hiyo wakati Amin akikataa wazo la askari wake la kuvunja madaraja nchini kwao—kama walivyovunja lile la Mto Kagera—alikuwa tayari amepata ahadi kutoka kwa Gaddafi kwamba alikuwa anamwandalia askari na silaha ambao wangetumwa Uganda kupambana na Watanzania. Hii ilimpa Amin matumaini mapya. Sasa aliamini kuwa hatimaye ushindi ungekuwa upande wake. Kwa hiyo hakukuwa na sababu yoyote ya kuharibu madaraja mazuri ambayo wangelazimika tena kuyajenga baada ya Tanzania kushindwa vita.

Hadi kufikia wakati huu askari wa Libya walikuwa hawajaonekana vitani Uganda. Walioonekana ni Wapalestina waliokuwa wamevaa skafu za PLO na wengine walibeba vitambulisho. Jumanne ya Machi 13, 1979, kupitia Redio Uganda, Idi Amin alitangaza hadharani kuhusu ushiriki wa PLO kwamba, “majeshi ya Palestina yanapigana bega kwa bega mstari wa mbele.”

Kitendo cha Idi Amin kutangaza hadharani kiliwafanya PLO kushindwa kukanusha. Lakini walijaribu kujinasua. Walisema mamia ya watu wao waliopo Uganda walikuwa huko kwa ajili tu ya mafunzo ya kijeshi na si zaidi ya hapo. Lakini hawakuweza kukanusha kama walikuwa wanapigana bega kwa bega na majeshi ya Amin.

Hata hivyo PLO walifadhaika kiasi kwamba waliamua kutuma ujumbe wao mjini Dar es Salaam kusisitiza uhusiano mzuri na mwema na Tanzania. Jumatano ya Machi 21, 1979 ujumbe huo ukaitisha mkutano na waandishi wa habari na kusema, “Hakuna Mpalestina anayepigana bega kwa bega na majeshi ya Idi Amin.”

Lakini hilo halikuondoa ukweli kwamba ushiriki wa PLO katika jeshi la Amin ulikuwa mkubwa. Pamoja na ukweli huo, Rais Nyerere hakuvunja uhusiano kati ya Tanzania na PLO. Ni wakati gani askari wa Libya walliingia.

Tukutane toleo lijalo.



Columnist: mwananchi.co.tz