Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

VITA VYA KAGERA: Mwl Nyerere amgomea Muammar Gaddafi-18

33615 VITA+PIC.png Tanzania Web Photo

Thu, 27 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wakati Tanzania ikiwa imejiandaa kuiteka miji ya Kampala na Entebbe, rafiki mkubwa wa Iddi Amin, Kanali Muammar Gaddafi, alijaribu kumtisha Rais, Julius Nyerere kwa kumwambia ayaondoe majeshi yake nchini Uganda ndani ya saa 24.

Alhamisi ya Machi 29, 1979 Rais Nyerere alilitangazia Taifa kuwa Libya imeitaka Tanzania iyaondoe majeshi yake nchini Uganda katika muda wa saa 24 la sivyo itaingia vitani kikamilifu kumsaidia Amin.

Akizungumza na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Mwalimu Nyerere alisema: “Jumamosi hii iliyopita, Kiongozi wa Libya, Kanali Gaddafi, alimtuma mjumbe wake kuniletea risala. Na risala hiyo inasema hivi, ‘Tangu mgogoro umeanza baina ya Tanzania na Uganda tumejitahidi sana kusuluhisha, lakini sasa baada ya uchunguzi wa muda mrefu, tunaamini Watanzania ndio wachokozi.

“Watanzania ndio waliomvamia Amin, walioivamia Uganda na kwamba vita vinavyoendelea ndani ya Uganda sasa ni vita vya Watanzania wanaoipiga Uganda na wala hakuna Waganda ndani yake…’ Kwa hiyo inasema risala hiyo, ‘naiomba Tanzania itoe majeshi yake nchini Uganda na tunataka majibu katika muda wa saa 24.

“Nilimjibu. Nitaeleza majibu hayo baadaye. Lakini leo nimepata risala nyingine kutoka kwa Kanali Gaddafi. Anasema tuondoe majeshi yetu nchini Uganda katika muda wa saa 24 la sivyo Libya itaingia vitani upande wa Amin.

“Sasa napenda kutoa majibu niliyompelekea Kanali Gaddafi. Nimemwambia balozi wake ampelekee.

“Nimesema, vita hivi vimeanza Oktoba 1978. Vilianzishwa na Amin kwa kuivamia Tanzania na kuchukua eneo lake na kuitangazia dunia kwamba eneo hilo sasa ni sehemu ya Uganda na kwamba kitendo hicho kilikuwa kinatimiza shabaha ambayo Amin alikuwa ametangaza tangu mwaka 1971.

“…Na usuluhishi ulianza wakati uleule. Na sisi tulikuwa tayari kukubali usuluhishi. Na masharti ya usuluhishi tuliyatamka. Tukasema kwanza Afrika ikitambue kitendo hicho kuwa ni kibaya. Ni kitendo cha uvamizi.

“Akemewe huyo. Kusudi kesho na keshokutwa akijaribu kitendo hicho tena ajue atakemewa. Ushahidi wa kumkemea mvamizi uwepo. Pili, aahidi, akane kwamba hataki sehemu yoyote ya Tanzania. Na, tatu, aahidi kulipa fidia kwa uharibifu alioufanya.

“Nitaeleza kwamba haya mawili ya mwisho yangekuwa hayana maana, mtu mwenyewe hana dhamana, lakini lile la kwanza ni la muhimu.

“Nilimweleza balozi kuwa yangetokea tungesikilizana. Tungeafiki. Hayakutokea. Lakini yeye Amin akaendelea kututishia kuwa si tu sehemu aliyoikalia, lakini anajiandaa kukalia sehemu nyingine zaidi za Tanzania.

“Tukaona ushahidi kuwa kweli anajiandaa. Tukaamua kumpiga tena. Tukaamrisha apigwe. Na ndivyo vita hivyo vinaendelea. Na ni vilevile vinaendelea.

“Kwa hiyo nikamwambia balozi amwambie ndugu yetu Gaddafi kuwa kama vita hivi vilikuwa halali wakati vinapigwa katika ardhi ya Tanzania, haviwezi kugeuka na kuwa haramu wakati vinapigwa katika ardhi ya Uganda. Ni vita vilevile.

“Na kwamba vita tunavyopigana sisi ni vita vya usalama wa nchi yetu. Hatukusudii kumtoa Amin. Ni uongo kuwa tunataka kumtoa. Tumeishi naye miaka minane. Tunataka kuwa na hakika kuwa anajua kuwa vita si lele-mama. Kuwa vita si mchezo. Si jambo la kuingia katika nchi ya watu halafu unakwenda unasema uliichukua kwa dakika 25.

“Ajue hivyo. Tunataka ajue kuwa vita si lelemama. Vita si mchezo. Akishajua hilo, madhali tuliishi naye miaka minane, tuko tayari kuishi naye miaka mingine minane.

“…Ndugu Gaddafi alishaniletea ujumbe, na siku hiyo ukarudiwa ujumbe ule. Ukarudiwa siku ya Jumamosi, kwamba tumwamini Gaddafi. Kwamba yeye anachukua dhamana kuwa Uganda haitaishambulia tena Tanzania. Dhamana hiyo anachukua Gaddafi.

“Nilimwambia ndugu balozi amweleze ndugu Gaddafi ugumu wetu sisi kukubali dhamana hiyo. Nilieleza sababu mbili.

“Sababu ya kwanza, Amin haaminiki. Nikamwambia (balozi) amuulize ndugu Gaddafi yeye anamwamini? Sema mimi namuuliza yeye (Gaddafi) anamwamini Amin? Anaweza kuchukua Msahafu akasema kwa jina la Allah namwamini Amin? Anaweza?

“Hakuna mtu mwenye akili anaweza kumwamini Amin. Yeye Gaddafi anamwamini? Kwa nini ananiomba mimi nimwamini? Kesho na keshokutwa atamgeuka huyo. Urafiki uliopo baina ya Uganda na Libya kesho utageuka kuwa uhasama.

“Nitamuuliza nani kuhusu usalama wa nchi yangu? Nitamwendea nani kumuuliza wakati huo Amin amekwishamgeuka Gaddafi?

“Nikamwambia balozi, ndugu balozi, mimi nimefurahi sana tangu mwanzo wakati nilipokuwa naupokea ujumbe wa Libya kujaribu kusuluhisha ugomvi baina yetu na Uganda, lakini yalikuwa yanatokea maneno kuwa mpo ndani ya Uganda mnapigana bega kwa bega na Iddi.

“Sisi tumekataa kutangaza habari hii. Tumekataa kuipokea rasmi na kuitangaza. Kwa nini? Kusudi muendelee na shughuli za usuluhishi…

“Pili, huyo Amin ni mkorofi huyo. Sitaki amani naye. Tunataka ajifunze kuwa vita si lele-mama. Akishajifunza tutakuwa na amani baina ya Tanzania na Uganda. Lakini hawezi kujifunza ikiwa anajua kwamba mali ya Libya iko nyuma yake.

“Hayo ni majibu kwa ufupi niliyompelekea ndugu yangu Gaddafi. Na leo amerudisha ya kwake. Amesema tutoe majeshi yetu Uganda, na kama hatukufanya hivyo nchi yake itatoa msaada kwa Uganda.

“Lakini wakiamua kuwa wanamsaidia Amin, pamoja na kwamba wanaongeza uzito katika vita, hawawezi kubadilisha msimamo wa Tanzania. Amin atabaki yuleyule mshenzi, muuaji, haaminiki.

“Ila sasa najua atavimba kichwa zaidi kwa kujua kwamba ana nguvu na nchi tajiri nyuma yake. Na nguvu hiyo sasa imetamkwa rasmi.

“Kwa hiyo hatari kwetu itakuwa ni kubwa zaidi, si inakuwa ndogo. Na kwa hiyo tutajifunza zaidi kumkabili. Lakini tunamkabili Amin. Nataka ndugu zangu wa Libya wajue hivyo. Hatuna ugomvi na Libya. Tunapigana na Amin. Hatupigani na Libya.

“Lakini usalama wa Tanzania ni dhamana ya Watanzania. Utalindwa na Watanzania. Siwezi kumwomba mtu mwingine nimkabidhi usalama wa nchi yangu. Nitaendelea kupambana na wote wanaohujumu usalama huo….

Itaendelea kesho



Columnist: mwananchi.co.tz