Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

VITA VYA KAGERA 1978-1979: Uhalifu waingia mitaani-25

Fri, 4 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Toleo lililopita tuliona askari wa Iddi Amin waliobakia katika mji wa Kampala walivyohaha kutoroka bila kujulikana. Waliingia mitaani maeneo ya raia wakiwa ama mmoja mmoja au katika makundi ya askari wachache wakitafuta nguo za kiraia, chakula na—la maana zaidi kwao—magari ambayo wangeweza kuyatumia kukimbia mji.

Pia walitumia silaha walizokuwa nazo kufanya uporaji na raia ambao hawakutii matakwa ya askari hao na wengine ambao hawakupewa nafasi ya mjadala, waliuawa. Hata hivyo hatimaye walielemewa. Sasa endelea...

UKIACHA uporaji uliokuwa ukiendelea na mtupiano wa risasi wa hapa na pale uliokuwa ukifanywa na askari wa Iddi Amin waliokuwa wanatafuta njia ya kuikimbia Kampala, baadhi ya wapiganaji wa Jeshi la Ukombozi wa Uganda (UNLA) nao walijikuta wakilipiza visasi kwa vibaraka wa Amin.

Baadhi ya waliokuwa wameukimbia utawala wa Iddi Amin lakini sasa wakawa wamerudi walianza kuwawinda na kuwaua wale ambao wao walidhani kuwa waliwasaliti au familia zao miaka iliyopita katika utawala wa Amin. Askari wengine wa UNLA waliua kila Mnubi au Mkakwa waliyekutana naye.

Usiku wa Jumanne ya Aprili 10 kuamkia Jumatano, siku ambayo Kampala ilikombolewa, wafuasi wa Amin waliyakimbia makao makuu ya polisi wake wa siri (State Research Bureau—SRB) yaliyokuwa eneo la Nakasero. Lakini wakati wanaondoka walirusha mabomu ya mkono kwenye vyumba walimokuwa ‘wafungwa’ ambao awali walikuwa wamenusurika kufa kwa njaa, mateso na adhabu za vifo.

Ilipofika asubuhi ya kesho yake maeneo ya maegesho ya magari kwenye ofisi za SRB yalikuwa yamefurika raia waliofika kuangalia kama kuna ndugu zao waliokuwa wanashikiliwa humo.

Baadhi ya walionusurika kufa walikuwa wamekonda kupita kiasi. Wapo wengine waliotoka walijikuta wakipata tabu juani kutokana na kuona jua kwa mara ya kwanza katika kipindi cha muda mrefu kwa sababu walikuwa wamefungiwa ndani.

Kwa mujibu wa kitabu cha Escape from Idi Amin’s Slaughterhouse cha Wycliffe Kato, miili ya raia waliokuwa wanashikiliwa katika makao hayo makuu ya SRB ilikuwa imetapakaa karibu kila eneo. Harufu kali ya miili iliyooza ilielekea kutovumilika. Raia wa Uganda waliingia ndani ya vyumba vya mateso vya SRB kutafuta miili ya wapendwa wao.

Miili mingine ilikuwa ni ya watu ambao ndiyo kwanza walikuwa wameuawa saa chache kabla ya askari wa Amin kukimbia wakati mingine ilikuwa ni ya muda mrefu uliokuwa umepita. Mingine ilikuwa imekatwa mikono na miguu.

Kitabu cha War in Uganda kinasema kwenye sakafu ya chini ya ardhi ya jengo hilo kulikuwa na silaha kali za kivita na mabomu yaliyokuwa na uwezo wa kuangamiza mji mzima.

Ikiwa mabomu hayo yangetumiwa kuvunja madaraja ya kusini mwa Uganda huenda yangewachelewesha askari wa Tanzania kwa miezi kadhaa kuifikia miji iliyoteka.

Ghorofa ya juu ya jengo hilo kulikuwa na kompyuta kadhaa na majalada yaliyokuwa na habari muhimu za kiitelijensia na nyingine zisizo za muhimu zilizohusu shughuli za maelfu kwa maelfu ya Waganda waliokuwa ndani na nje ya nchi na utiifu wao kwa Serikali ya Uganda.

Pia kulikuwa na maelfu kwa maelfu ya majalada yenye taarifa za wageni waliokuwa wakiishi Uganda au walioitembelea Uganda.

Kwa mujibu wa kitabu hicho, jalada moja lilionyesha kuwa wakala mmoja wa SRB alikuwa akilipwa posho ya Dola 58,500 za Marekani kwa ajili ya kumwezesha kupata taarifa.

Kitabu cha War in Uganda kimeandika kuwa faili moja katika maelfu ya mafaili yaliyokutwa katika ofisi hizo lilikuwa na muhtasari wa vikao vya siri vya baraza la mawaziri la Tanzania, moja likiwa na kiambato kilichosema “Rafiki yetu wa Dar es Salaam anataka 5,000 nyingine mwishoni mwa mwezi ... Inawezekana kilicho tatizo zaidi katika ghorofa ya juu ya ofisi za SRB ni nakala ya waraka wa siri wa jeshi la Tanzania ukieleza kinaganaga mpango wa kuishambulia Kampala. Waraka huo ulionyesha njia zitakazotumika na kila mahali ambako kila kikosi kitakuwa ... muda uliowekwa katika mkakati huo ni wiki mbili hadi kuingia mji mkuu wa Uganda.”

Kwa jeshi lililokuwa likiulinda mji wake kama hilo la Amin, halikuwa na kitu cha thamani zaidi ya kupata mbinu za siri za jeshi la uvamizi.

Kwa jeshi lolote duniani ambalo lilikuwa limeshaupata mpango wa siri wa jeshi la adui ingekuwa ni rahisi kwao kuweka mtego na kuliangamiza jeshi la adui.

Lakini jeshi la Idi Amin halikuweza kutumia taarifa hizo za kiitelijensia. Huenda walizipata taarifa hizo wakiwa tayari wameshaelemewa na hivyo haikuwa rahisi kwao kuzitumia ilivyopaswa. Isitoshe, taarifa hizi hazikukutwa jeshini bali zilikutwa kwa polisi wa siri wa Amin.

Ilionekana kuwa SRB walikuwa mbali sana katika kukusanya taarifa za kiitelijensia. Pengine tatizo lilikuwa katika kuzichanganua taarifa hizo na kuzifanyia kazi.

Kwa upande mwingine, Kanali Salim Hassan Boma na askari wake walifika kwenye Gereza la Luzira ambalo lilikuwa na sifa mbaya kwa mateso. Liko kwenye viunga vya Kampala.

Maofisa na walinzi wote wa gereza hilo walikuwa wameshakimbia wakiwaacha wafungwa wakiwa wamefungiwa ndani ya gereza bila chakula na bila kujua kilichokuwa kikiendelea nje ya gereza. Kanali Boma aliamuru gereza hilo lifunguliwe na wafungwa waondoke.

Miongoni mwa wafungwa hao alikuwamo kapteni wa ndege za kijeshi aliyepata mafunzo nchini Urusi.

Baada ya kuendesha ndege aina ya MiG-21 katika zile siku za mwanzo za vita, aligoma kuendelea na kazi na baadaye akakimbilia kijijini kwake ambako baadaye aligundulika na kukamatwa.

Mahakama ya kijeshi ilimhukumu kifo na Jumatano ya Aprili 11, 1979—siku ambayo Kampala ilikombolewa na majeshi ya Tanzania—ndiyo ilikuwa tarehe iliyokuwa imepangwa yeye kuuawa kwa kupigwa risasi.

Aliposikia vishindo vya nyayo za miguu vikielekea lango la gereza alilokuwamo asubuhi ya Aprili 11, hakuwa na namna yoyote ya kujua kama hao waliofika gerezani hapo ni wauaji wake wamewasili kumchukua. Lakini kwa mshangao akakuta ni binadamu waliokuja kumweka huru.

Askari wa Tanzania walihisi hawakuwa na la kufanya zaidi ya kuwaachia huru kila mfungwa waliyemkuta katika Gereza la Luzira kwa sababu hawakuwa na namna ya kuwalisha maelfu ya wafungwa na wakati huohuo wakiendelea na mapambano ya kumaliza vita.

Lakini kuachiwa kwa wafungwa hao kwa ujumla wao kulikuja kusababisha matatizo baadaye. Baadhi ya wengine walioachiwa walikuwa wahalifu sugu ambao baadaye walichangia kuongezeka kwa uhalifu nchini Uganda.

Itaendelea kesho



Columnist: mwananchi.co.tz