Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Uvunaji maharage kizamani unavyomtia hasara mkulima

13043 Pic+maharage TanzaniaWeb

Tue, 21 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kwa wakulima walio wengi kazi ya shamba wanayoipa umuhimu ni kuandaa shamba, kupanda, kupalilia, baada ya hapo kipindi cha mavuno huonekana cha kawaida.

Hata hivyo ukweli ni kwamba uvunaji wa mazao nalo ni jambo muhimu linalotakiwa kupewa kipaumbele kama zilivyo shughuli nyingine kabla ya mavuno.

Tatizo la uvunaji lipo kwa baadhi ya wakulima wa maharage wilayani Ngara, Kusini Magharibi mwa mkoa wa Kagera nchini Tanzania ambao hupoteza mazao wakati wa uvunaji kwa kuwa mengine hudondoka chini na hivyo mkulima kujikuta akipata hasara kwa kupata maharage kidogo.

Inaelezwa kuwa sababu ya wakulima kupoteza maharage ni kutozifahamu njia bora za uvunaji, upulaji na upetaji lakini pia miundombinu ya barabara inachangia kumwagika kwa maharage.

Monica Lugesha, mkulima ambaye kwa sasa ana miaka 70.

akiwa amevaa kitenge cha rangi mchanganyiko bluu na njano kichwani akiwa kafunga kitambaa, anaonekana akitabasamu wakati akivuna maharage shambani kwake.

Bi Lugesha anaishi mtaa wa Mtakuja kata ya Lulenge wilayani Ngara, anaeleza kuwa anafuraha kwa kuwa ni msimu wa uvunaji ambao wakulima wengi huonekana shambani wakivuna maharage, moja ya chakula kikuu kwa wakazi wa Ngara.

Bi Lugesha anaeleza kuwa huwa anavuna maharage kwa njia za kizamani, huyan’goa na kuyarundika kisha kuyafunga kwa kamba na kuyabeba kichwani kupeleka nyumbani kwake.

Anazitaja mbegu za asili za maharage zinazolimwa zinazotambulika kwa kabila la waangaza na washubi waishio wilayani humo kuwa ni Uluhunja ya rangi ya njano, Rose Koko, nyekundu yenye madoa na Ugwela ambayo ni nyeupe.

Nyingine ni Kamusheli (nyeupe), Uluvunan’kingi, (nyekundu kubwa), Uluvuzovuzo (ya rangi ya kijivu), Amanyarane (kahawia ndogondogo) Amachimbatala (kijivu mchanganyiko na nyeupe), Kadunduri, Shushamazi, Kweza, Manyurane, Mavondolo na Karahinda.

“Kweli unapovuna maharage mengine hudondoka, yapo yanayobaki shambani kwa kutoyaona ambayo hupasuka na kudondoka, tukishavuna tunabeba kichwani au kwenye baiskeli na pikipiki.

Lugesha anaongeza: “Unapoyasafirisha kwenda nyumbani hudondoka njiani, wakati wa kuyaanika ili yakauke napo pia hudondoka chini ya mchanga kwa kuwa hatuna mbinu bora za uvunaji.”

Bi Lugesha anasema kuwa huyapula maharage kwa kupiga kwa kutumia mti ambako maharage huruka juu na kudondoka na wakati wa kupeta yapo yanayomwagika hivyo yanapungua tofauti na yalivyokuwa bado hayajavunwa.

“Nikishayamenya maganda nayaanika kwenye kifaa cha kuanikia kwa kabila la Washubi tunaita Ikigara, yakikauka nayahifadhi kwenye mifuko au mitungi ya asili tayari kwa kuuza au matumizi ya nyumbani,’’ anasema.

Nicolous Kanuma (78) mume wa Bi Lugesha anasema sababu ya maharage kudondoka shambani inatokana na wakulima wengi kukosa elimu ya ulimaji bora na kisha kuvuna kienyeji, wanashindwa kuyaokota kwa kuwa waliyapanda kiholela, hawakupanda kwa mstari ili iwe rahisi kuona wakati wa uvunaji.

Adronizi Bulindoli (48) mkazi wa Nyarulama kata ya Kibogora anasema baadhi ya wakulima huvuna maharage yakiwa yamekauka sana na hivyo kupasuka na kudondoka wakati mwingine kabla hata ya kuvunwa.

Anaongeza kuwa ni vigumu kuokota punje zote, anawashauri kuvuna nyakati za asubuhi si wakati wa jua kali kwani hiyo itasaidia kuokoa mbegu lakini pia elimu ya uvunaji bora itolewe kupita mikutano ya hadhara.

Bi Mastidia Venus (40 ) mkazi wa kijiji cha Rwinyana kata ya Bugarama, Ngara mjini anasema katika eka moja inayovunwa kilo 10 za maharage hupotea wakati wa usafirishaji, maharage hudondoka kutokana na umbali uliopo kutoka shambani hadi nyumbani.

Anasema akishavuna mazao yake huyauza soko la Songambele, kilomita mbili kutoka kwake kijiji cha Rwinyana na kilomita nne kwenda kijiji cha Bugarama.

Kilo moja ya maharage ya njano huuzwa kwa Sh 1,200 hadi 1,500 na maharage mchanganyiko ni Sh600 hadi 1,000 wakati wa msimu wa mavuno.

Sophia Metusera (44) mkazi wa kijiji cha Kumuzuza, kata ya Mabawe, akiwa na wanawake wenzake wakiwa wamejitwisha mifuko yenye maharage vichwani anasema wao huvuna na kuyapulia shambani na kubeba yakiwa tayari.

Anasema wanafanya hivyo ili kunusuru maharage yanayodondoka njiani wakati yakisafirishwa yakiwa kwenye maganda yake.

Akizungumzia hilo, ofisa kilimo mamlaka ya mji mdogo wa Rulenge, Essau Nyamziga anasema wakulima hupoteza mazao mengi shambani kwa kuwa wanachelewa kuvuna.

Hata hivyo anasema uhaba wa watumishi unawafanya washindwe kuwafikia wakulima wote pamoja na gharama za usafiri ambazo pia zinawakwaza maofisa kilimo na shughuli zao.

Diwani kata ya Rulenge, Hamis Baliyanga anasema ni vyema wakulima wakanunua vifaa vya kuweka maharage wakati wanapovuna na kupula ikiwamo turubai ambalo litasaidia maharage yasidondoke na kupotea.

Naye ofisa kilimo wilaya ya Ngara, Constatine Mdende anawataka wakulima kuvuna mazao na kuyabeba kwenye mifuko ili yasidondoke na wanapoyapula yawe ndani ya mifuko badala ya chini na yanapodondoka wayaokote.

Mbali na hilo, ofisa huyo pia anahimiza umakini wakati wa kupanda maharage.

“Wakulima wapande kwa mistari ili iwe rahisi kuvuna, watu wa shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na kilimo la Agra wameleta mbegu bora ambazo tayari zinafanyiwa majaribo na tumeandaa mashamba darasa na mbegu hizo msimu ujao zitatawanywa kwa wakulima,’’ anasema.

Anazitaja mbegu hizo kuwa ni Uyole njano, Seliani 97, Lyamungo 90, Liamungo 85 na Jeska ambayo mbali na kuwa chakula lakini pia inatajwa kuongeza nguvu za kiume.

Mdende anasema wilaya ya Ngara ina kaya 56,964 zinazolima mazao mbalimbali na halmashauri ya wilaya hiyo ina hekta 374,400, zinazofaa kwa kilimo lakini ni hekta 104,550 tu zinazotumika.

Anaongeza kuwa eneo lililolimwa hekta 72,671 sawa na asilimia 69.5 ya eneo lote linalofaa kwa kilimo na kati ya hizo hekta 23,239 zimelimwa maharage huku ikiwa na idadi ya maofisa kilimo 45.

Pia anasema kuwa tani za maharage 46,479 zinategemewa kuvunwa msimu huu lakini kati ya hizo tani 2,324 za maharage yatapotea.

Mkuu wa wilaya ya Ngara Michael Mtenjele anasema kuwa wakulima walio wengi hawana elimu hivyo ni vyema wataalamu wakatoa elimu namna gani mkulima alime na kuvuna kwa ubora lakini pia wakulima wafike ofisi za wataalamu wa kilimo kupata elimu .

‘’Ili biashara ikubalike lazima iwe ya kiwango iliyokidhi ubora, maafisa kilimo muende kwa wakulima mkatoe elimu. Usafiri isiwe kigezo cha kutofanya kazi, pia watu wasikilize vipindi vya redio, televisheni na wasome magazeti ili wapate elimu ya kilimo bora,’’ anasema.

Columnist: mwananchi.co.tz