Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Utekelezaji ahadi ya Sh50 milioni kila kijiji unapimwaje?

71452 Elius+Msuya

Thu, 15 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Sura ya tano ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-20 inazungumzia uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Ibara ya 57(d) ya sura hiyo inaahidi “Kutenga kiasi cha Sh50 milioni kwa kila kijiji kama mfuko wa mzunguko kwa ajili ya kukopesha vikundi vya wajasiriamali kupitia ushirika wa kuweka na kukopa katika kijiji husika.”

Ahadi hii sasa imezua mjadala mpana miongoni wa viongozi na makada wa CCM hasa wanaposema fedha hizo zimeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.

Kwa mfano, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amenukuliwa hivi karibuni akisema ahadi hiyo haikumaanisha kugawa fedha nyumba kwa nyumba, badala yake ni kuzitoa kupitia miradi ya maendeleo na ya kijamii.

Si yeye peke yake, bali wapo viongozi waliojaribu kutetea utekelezaji wa ahadi hiyo wakiwemo mawaziri. Wengine wanasema ahadi hiyo haikuwa na muda maalumu, wakati wanajua kuwa ilani yenyewe ina muda maalumu wa miaka mitano.

Kimsingi, kifungu hicho kinazungumzia uwezeshaji wa wananchi kiuchumi na kinataja kutoa Sh50 milioni kama mfuko wa mzunguko kwenye vyama vya kuweka na kukopa.

Pia Soma

Ni kweli zile siyo fedha za kugawa nyumba kwa nyumba, bali ni za kukopeshana. Yaani lengo la zile fedha ya kukopeshwa zinatakiwa zirudi kwa wakati tena na zikiwa riba.

Ikiwa zile fedha zingetolewa, leo kila kijiji kingekuwa na Saccos na kukopa na wananchi wangekuwa mbali.

Lengo lilikuwa zuri la kuwawezesha wakulima, wafugaji na wafanyabiashara kupata mitaji na kuzungusha zile fedha. Kwanza ingewasaidia kupata mitaji na ingeongeza hata ajira na Serikali ingepata mapato kwenye vyama hivyo.

Badala yake viongozi wa CCM wanasema zile fedha zimeshatolewa kwenye miradi mingine ya maendeleo, ambayo si ya kukopeshana.

Hatuna uhakika, lakini ukweli ni kwamba ahadi hiyo haijatimizwa. Kama ni hiyo miradi, mbona nayo iliahidiwa kwenye ilani hiyohiyo?

Kama ni elimu, afya, miundombinu, maji, kilimo na mifugo ilani imesema waziwazi, sasaiweje zile Sh50 milioni ndiyo zimeelekezwa hukohuko?

Na kama zimehamishwa kwenda maeneo mengine, tutapimaje kama kweli zinalingana na Sh50 milioni? Au kama ni zilezile zilizoahidiwa pia kwenye maeneo mengine? Lini Serikali ilitangaza kuwa imetenga fedha hizo kwenye bajeti au lini ilizitoa? Au kwa kuwa ahadi imeshindikana sasa ndiyo tunaelezwa fedha zinatekeleza miradi ya maendeleo?

Kweli, ilani si msahafu na inaweza kubadilika, lakini wananchi wana haki ya kuhoji na kuelezwa ukweli.

Wapo waliopiga kura kwa CCM wakiamini kuwa watapata mitaji ya biashara kwa fedha hizo.

Columnist: mwananchi.co.tz