Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Utalii wa ndani unapaswa kuanzia darasani

11810 Joseph+Chikaka TanzaniaWeb

Tue, 14 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kumekuwapo changamoto kubwa katika jamii ya Kitanzania kushiriki kufanya utalii wa ndani ama wa nje ya nchi. Watanzania wamekuwa wakisemana vibaya kuwa hawana utamaduni wa kufanya utalii wa ndani.

Sababu kadhaa zimetajwa kuwa kikwazo cha watu kufanya ziara hizo. Baadhi ya sababu hizo ni umasikini, kutojengewa utamaduni huo tangu awali (yaani shuleni au vyuoni), gharama ya viingilio na kutokuwa na taarifa za kutosha mathalani kuhusiana na utalii wa ndani hasa maeneo yenye vivutio na namna ya ufikaji wake.

Utalii ni kitendo cha mtu kwenda kutembelea na kujifunza kuhusu nchi na maumbile yake kijiografia. Pia, utalii ni hali ya kusafiri huku na huko ili kuyafurahia mandhari.

Wengine husema kwamba hata kile kitendo cha wenyeji kusaidia au kushughulikia watalii na kuwahudumia nacho ni utalii. Utalii unahusisha kusoma desturi, tabia, utamaduni, miiko, matambiko na historia ya nchi au sehemu husika.

Kuna aina mbalimbali za utalii kama vile utalii wa kibiashara, kidini, mikutano, mapumziko, utamaduni na historia na kimazingira.

Utalii wa ndani

Utalii wa ndani ni kule kutembea kutoka mahali pamoja hadi pengine ndani ya nchi husika. Tabia ya watu kuthamini na kufanya utalii wa ndani inaweza kuchochewa kwa kuwapo sera za utalii wa ndani kuanzia ngazi ya shule, vyuo, taasisi za dini na katika ofisi mbalimbali za umma na binafsi.

Shule na vyuo zina nafasi kubwa ya kuhamasisha kwa sababu zenyewe ni mojawapo ya wakala mkubwa wa mabadiliko na maendeleo katika jamii. Kwa mfano, ni watu wangapi wanaofahamu kuwa kuna aina rahisi ya utalii wa kufanywa kwa kutumia baiskeli?

Shule zinawezaje kuwa wakala wa utalii wa ndani?

Ziara za mafunzo ni mbinu au njia mojawapo ya kujifunza na kufundisha. Wanafunzi hupata uelewa mkubwa wanapotazama mazingira ya nchi kwa uhalisia.

Wanafunzi katika shule na vyuo wanaweza kufanya utalii wa ndani endapo shughuli hii itapangwa katika kalenda zao za mwaka.

Pia, shughuli hii inapoonyeshwa katika ratiba kuu ya masomo inatoa fursa kwa kamati ya ziara ya shule au chuo husika kuandaa ziara za kimafunzo kwa madarasa tofauti kwa kila kipindi cha likizo za masomo.

Zipo njia nyingi zinazoweza kutumika katika maandalizi ya ziara. Moja, ni kamati ya ziara kuratibu maandalizi kwa kutuma mwalimu kwenda kuona sehemu watakazopata malazi na chakula, watakazotembelea na kama kuna shule wangependa kufanya mtihani wa pamoja wa kujipima na kujua kiasi cha gharama.

Mbili, ni utaratibu wa kutumia kampuni za utalii. Matumizi ya kampuni za utalii huokoa muda wa walimu kwenda kufanya mchakato wa maandalizi ya ziara husika. Pia, kunapotokea dharura yoyote ile safarini ni rahisi kwa kampuni kutatua kwa sababu wao kila siku wako katika michakato hiyo na ndiyo sehemu ya kazi zao.

Mbinu za shule kuwezesha utalii wa ndani

Shule na vyuo zinaweza kuwa mabalozi wa utalii wa ndani kwa kutumia mbinu zifuatazo: moja, kuwapa ufahamu na uelewa wanafunzi wake. Wanapofanya hivyo huiwezesha jamii kufahamu faida za utalii wa ndani na namna watu wanavyoweza kufanya.

Wanafunzi ni mabalozi wakubwa wa mabadiliko katika jamii. Wanapopata elimu huweza kuifikisha kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla.

Kupitia shule na vyuo, tabia ya watu kupenda kufanya utalii wa ndani hukuzwa kwa sababu ya uhamasishaji kutoka kwa wadau mbalimbali wenye uelewa wa utalii na kampuni zote zinazojishughulisha na utalii.

Mbili, mamlaka ya hifadhi za taifa zinaweza kutia chachu utalii wa ndani kwa kutoa punguzo za viingilio kwa wanafunzi na wanachuo. Unafuu huo usiwe tu katika kipindi cha sherehe za Sabasaba au Nanenane pekee; ambapo wanufaika wengi huwa wale tu ambao wamepata fursa ya kutembelea maonesho.

Tatu, shule kueleza fursa ambazo zinaweza kuwanufaisha wanajamii ambao wameizunguka hifadhi ya taifa.

Nne, kupitia uhamasishaji kutoka katika vyombo vya habari na mawasiliano ambavyo ni sawa na shule isiyo rasmi.Vyombo vya habari na mitandao ya kijamii vinaweza kuhamasisha utalii wa ndani.

Tano, mitalaa yetu ya elimu katika ngazi zote kuweka suala la utalii wa ndani kama suala mtambuka. Ikiwezekana suala la utalii wa ndani lichopekwe katika masomo mbalimbali.

Mtaalamu wa masuala ya utalii na uhifadhi wa tamaduni kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Ismail Swaleh anaeleza kuwa sekta binafsi inayojishughulisha na utalii kama kampuni za utalii, bado hazijachangia katika kuhamasisha jamii ya Kitanzania juu ya utalii wa ndani tofauti na wanavyofanya kwa watalii kutoka nje.

Anasema ni wakati sasa wa mamlaka kuziwezesha kampuni binafsi na vyama vya kijamii vinavyokuza utalii. Pia, kwa shule kuwajengea wanafunzi misingi ya kupenda na kuthamini utalii wa ndani tangu wakiwa watoto na vijana.

Siyo rahisi kwa mtu ambaye hakujengewa tabia ya kutumia kipindi cha likizo kwa kufanya utalii, akategemewa tu kuibuka ukubwani na kuanza kutembelea vivutio hata kama ana rasilimali za kumwezesha.

Utalii wa ndani unapaswa kuanza kuchochewa tangu darasani. Ni wajibu wa kila shule na chuo kuhakikisha kuwa wanafunzi wake wanapata fursa ya kufanya utalii wa ndani mara nyingi zaidi.

Wanapowezesha wanafunzi wao kujenga tabia ya kutumia likizo kutalii, watakuwa wameiwezesha jamii yote.

Columnist: mwananchi.co.tz