Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Usimpe mtoto jina la Lowassa, Ridhiwani

48921 Pic+ridhiwani

Wed, 27 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Siasa za nchi hii zina mengi. Ukitafakari sana unagundua kwamba wanasiasa wengi wanatuona sisi kama si wendawazimu, tuna akili za kitoto au mapunguani. Hali hii tumeiruhusu sisi wenyewe kuonekana hamnazo mbele ya macho yao kwa kulipokea kila litokalo kwenye vinywa vyao.

Edward Lowassa akiwa CCM alitupiwa madongo mengi akiitwa na wapinzani kuwa fisadi. Alipohamia upinzani akaitwa mwenye makandokando mengi asiyefaa siyo tu kuwa rais wa nchi, bali kuishi na wanachama wa CCCM.

Leo CCM wanadai upinzani wamemsafisha huo wao (upinzani) wakidai CCM wamepokea uchafu wao. Wameshaona sisi ni mabwege.

Mpaka sasa naamini Lowassa ni mtu safi ila anasingiziwa. Unakumbuka ya Ridhiwani? Acha kabisa. Machinga Complex tuliambiwa yake. Kampuni ya Lake Oil nayo yake. Mwendokasi tuliaminishwa ni ya kwake, hata mji Mpya wa Kigamboni uliofeli, wakasema ni mipango na mradi wake. Hivi mnakumbuka?

Ndo ujue wanasiasa wanatuona mabwege mtozeni sana. Kinara wa taarifa hizi alikuwa Dk Willibrod Peter Slaa akiwa kwenye ubora wake pale Mtaa wa Ufipa Kinondoni. Akasema Home Shopping Centre mmiliki wake ni yeye. Diamond Platinumz huku mitaani pia wakadai kuna mkono wa Ridhiwani.

Kila chenye mkwanja au jambo lenye mvuto na matumizi makubwa ya pesa tulielezwa kuwa Ridhiwani anahusika. Sasa watu tukajiuliza kama zote hizo ni mali zake mbona katika orodha ya matajiri Afrika hayumo? Watu ili kutowaangusha wanasiasa wao wakakoleza kuwa siyo utajiri wa halali ila ni utajiri wake. Tukaamini kuwa dogo ni tajiri balaa.

Dewji, Mengi, Bakhressa, Rostam hata Manji ni matajiri waliofahamika sana Bongo na nje ya Bongo. Lakini jarida la Forbes halikuwahi kuwataja wakati huo kama matajiri sana Afrika. Ila ukiangalia mali tulizoambiwa = Ridhiwani hakuna hata mmoja kati yao aliyemfikia. Tukasubiri Mtanzania mwenzetu atangazwe na jarida la Forbes.

Huwezi kuamini. Lakini ndio ukweli kuwa kila lori la mafuta lililopita barabarani tuliambiwa lake. Vituo vya mafuta pembezoni mwa barabara ya Dar, Moro, Iringa mpaka Mbeya tulijua vya Ridhiwani. Ndivyo ilivyo kwa vituo vya Dar mpaka Mwanza au Arusha. Akaanza kuhesabika kama tajiri anayeweza kuimiliki Yanga na wafuasi wake achana na wanachama.

Siwezi kumpa jina la Ridhiwani au Lowassa mwanangu. Yanasingiziwa sana. Ni shetani pekee nchi hii anayewazidi Ridhiwani na Lowassa kwa kusingiziwa.

Maana mtu akifanya kosa husingizia “shetani kanipitia.” Hata haya niliyoandika wakati ule watu wangesema nimetumwa na wenyewe. Watu bwana, utasikia lisemwalo lipo, kama halipo laja.



Columnist: mwananchi.co.tz