Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Usafiri, miundombinu vinavyokwaza haki ya kupata elimu kwa walemavu

15704 Pic+usafiri TanzaniaWeb

Thu, 6 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

“Pamoja na jitihada zinazofanywa kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanapata elimu kama watoto wengine, bado jitihada hizo hazijazaa matunda,” anasema Juma Mussa, mkazi wa Mgenihaji Mkoa wa Kusini Unguja.

Mussa ambaye ni mzazi wa Mwaka Juma Mussa, mtoto mwenye ulemavu wa macho anasema zinahitajika juhudi kubwa kati ya Serikali na jamii ili kundi la wenye ulemavu nalo lipate elimu ya kutosha.

Anasema kwa mtoto wake ambaye ni mlemavu wa macho pamoja na juhudi kubwa anazofanya kuhakikisha anapata elimu bado anakabiliwa na changamoto mbalimbali za kufikia mafanikio katika elimu ikiwamo uhaba wa vifaa vya kuso-mea, miundombinu ya shule kutokuwa rafiki na ushirikiano mdogo kati yake walimu, wanafunzi na jamii kwa ujumla.

Anasema ameitikia wito wa elimu ya mjumuisho kwa kumpeleka mtoto wake shule ya Uzini lakini ni kama vile anakwenda shule kukamilisha wajibu na si kufanikiwa kusonga mbele kielimu.Mwanaisha Shaaban mkazi wa Tunguu ambaye mtoto wake, Fatma Suleiman (21) ana ulemavu wa viungo na anasoma kida-to cha pili, anasema ukosefu wa usafiri wa uhakika kwa mtoto wake ni jambo ambalo limekuwa likimkatisha tamaa.

Anasema awali walikuwa na gari ambalo hulitumia pia kumpeleka mtoto wao shuleni Kiembesamaki lakini baada ya gari kuharibika mtoto huyo amekuwa akipata tabu katika magari ya kawaida.“Kuna wakati machozi hututoka kuto-kana na madhila anayopata mtoto wetu katika usafiri wa kwenda shule na kurudi nyumbani,’’ anasema.Mwanafunzi mwenye ulemavu wa macho, Maimuna Idd anasema baadhi ya walimu shule aliyokuwa akisoma walifu-rahi wakati anamaliza masomo wakisema afadhali mzigo umewaondokea.Anasema pamoja na jitihada zake za kuhakikisha anapata elimu kama watoto wengine bado anaona ni kama hakuna ulazima wa kusoma kwa watu wenye ule-mavu kwa jinsi jamii inavyowatenga.

Anasema pia miundombinu ya shule nayo haipo rafiki kwa wanafunzi wenye ulemavu, akitoa mfano wa vyooni, mada-rasani na mazingira ya shule. “Unajua nina hamu ya kusoma lakini mazingira ya kusomea hayajawa rafiki ukiachilia mbali vifaa lakini pia baadhi ya walimu nao wamekuwa wakitukatisha tamaa kwa maneno na vitendo hili nalo linauma,” anasema Maimuna.

Maimuna anaishauri Serikali kufuatilia kwa makini shida za watu wenye ulemavu hasa mashuleni ili kuzitatua.

Walimu watoa neno

Mwalimu mkuu wa Shule ya Sekondari Umoja ya Uzini, Vuai Saburi Muya anasema katika shule yake kuna wanafunzi wawili wasioona, mmoja yupo kidato cha kwanza na mwingine cha pili lakini bahati mbaya wanafunzi hao wanaonekana kukosa elimu ya msingi ya mjumuisho.

Anasema pamoja na jitihada wanazofanya ili kuona wanafunzi wanafaulu vyema lakini ni wazi kufanikiwa kwa wanafunzi hao ni lazima wapatiwe elimu inayofuata taratibu za wenye ulemavu kabla ya kuingia elimu ya sekondari.

Mwalimu aliyepewa jukumu la kufundisha wanafunzi wenye ulemavu wa uoni katika shule hiyo, Rajab Sudi Hassan anasema changamoto zinazowakabili wanafunzi hao ni nyingi ikiwemo ukosefu wa vifaa vya kufundishia.

Akitolea mfano anazitaja mashine za kurekodi sauti ambazo ni muhimu kutumiwa na wanafunzi hao wanapokuwa nyumbani kwa mazoezi ya kujisomea ya ziada.

Changamoto nyingine ni uhaba wa walimu wenye utaalamu wa kusomesha wanafunzi wenye ulemavu hasa wa uoni akisema katika shule hiyo kuna mwalimu mmoja tu ambaye akiondoka wanafunzi hawana walimu wa kuwasomesha.

Viongozi wa walemavu wanena

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wasioona Zanzibar (Zanab), Adil Mohammed Ali, anasema Serikali kupitia Wizara ya Elimu ina kazi ya ziada ya kuifanya elimu mjumuisho kuwafikia wenye mahitaji maalumu popote walipo.

Anasema walemavu wanahitaji uungwaji mkono wa hali ya juu na ipo haja kwa Wizara ya Elimu kuboresha zaidi mitaala, kuongeza vitendea kazi, walimu na kuimarisha miundombinu ya kufikia shuleni kwa wanafunzi wenye ulemavu.

Anasema pamoja na jumuiya hiyo kufanya jitihada za kuwasaidia wanachama wake lakini kwa ruzuku ya Sh 1.8 Milioni wanayoipata kutoka serikalini ni wazi hawawezi kusaidia kundi hilo lenye wanachama zaidi ya 1,000.

“Naipongeza Wizara ya Elimu kwa kuanzisha elimu ya mjumuisho mwaka 2004 pamoja na sera yake katika mwaka 2006 lakini bado kuna changamoto kubwa ya walimu na vifaa vya kusomea wanafunzi wenye ulemavu hasa wa kuona,’’ anasema.

Mkurugenzi wa Idara ya Watu wenye Ulemavu Zanzibar (UWZ), Abeda Abdalla Rashid alikiri kuwa watu wenye ulemavu wanakabiliwa na mazingira magumu hasa kielimu.

Anasema mfumo wa elimu hasa vifaa na wataalamu bado unahitaji kufanyiwa kazi kwa kuwa haukidhi mahitaji.

“Watoto wenye ulemavu ni sawa na wengine, wana haki na fursa sawa kwa kila kitu, kuwakosesha elimu inayofaa kutokana na mahitaji yao kwa kiasi kikubwa ni kinyume na Katiba,’’ anasema.

Hoja ya wadau wa elimu

Yunus Kassim Khatib ni mwenyekiti wa watu wenye ulemavu wilaya ya Kati, yeye anaitaka Wizara ya Elimu kuimarisha elimu mjumuisho ili kundi hilo nalo liweze kupiga hatua kimaendeleo.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kati Unguja, Mohamed Salum Mohamed anasema wameanza kutekeleza ugatuzi sekta ya elimu, afya na kilimo na katika mwaka wa fedha 2018/19 wamejipanga kutekeleza agizo hilo.

Anasema katika utekelezaji wa majukumu yao watahakikisha majengo yote ikiwemo shule na vituo vya afya vinakuwa rafiki kwa wenye mahitaji maalumu ili wapate huduma muhimu za kibinaadamu.

Naye Ofisa elimu jumuisho wilaya ya kati katika kituo cha elimu ya mafunzo Dunga TC Unguja, Dude Mussa anasema shule 26 zimetambuliwa kuwa na wanafunzi wenye ulemavu kati ya shule 52.

Pia anasema wapo walimu 52 ambao tayari wamepata mafunzo ya elimu jumuisho huku walimu 3,705 wakipewa mafunzo ya ngazi mbali mbali katika kusomesha wanafunzi wenye mahitaji maalumu wakiwamo 83 wa ngazi ya diploma. Ofisa elimu wilaya ya Kati Unguja, Ali Muhsin anasema kuhusu miundombinu, baadhi ya shule zilizojengwa hivi karibuni zimezingatia hilo .

Anatolea mfano wa shule ya Umoja iliyopo Uzini ambayo hadi vyoo, vipo viwili maalum kwa watu wenye ulemavu.

Hata hivyo anasema changamoto kubwa ipo kwa shule zilizojengwa miaka mingi, baadhi yake hazina mazingira rafiki ya kufikiwa na wenye ulemavu.

Mkurugenzi wa Chama wa Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa-Zanzibar), Dk Mzuri Issa ambao ni wasimamizi wa mradi wa kukuza uwajibikaji katika mikoa mitatu ya Zanzibar.

Anasema watahakikisha wanaielimisha jamii na Serikali wenye ulemavu na mahitaji maalum nao wafanikiwe katika kupata huduma mbalimbali ikiwamo elimu.

Kupitia mradi huo ulishirikisha Jumuiya za Maendeleo Zanzibar (Wahamaza) na Jumuiya ya Uhifadhi misitu ya Ngezi (Ngeraneco) watahakikisha wanapita kila mkoa kutoa elimu ili kila mwananchi afahamu vyema haki za msingi kwa kundi la watu wenye mahitaji maalum.

Serikali yasema

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mmanga Mjengo Mjawiri anasema pamoja na jitihada zinazofanywa lakini wizara tayari imetoa vifaa mbalimbali vilivyogharimu zaidi ya Sh133 Milioni kwa lengo la kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu wanaondokana na changamato wakati wanapopatiwa haki yao ya msingi kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Miongoni mwa vifaa vilivyotolewa na wizara hiyo kupitia mradi wa Global Partnership Education (GPE) ni vifaa vya maandishi maalumu kwa wasioona (nukta nundu), kompyuta, madaftari maalumu kwa wasioona, kalamu, vifaa vya michezo na vyerehani, mashine ya kutolea karatasi (printer), redio maalumu za kurekodia kwa wasioona na vinginevyo.

“Pamoja na hatua hizo pia mtaala utazingatia masuala ya ufundi na mambo mengine ya amali ya vitendo yanafundishwa kwa kundi la wenye mahitaji maalum,” anasema.

Anasema katika kuwasaidia wanafunzi wenye ulemavu wa akili wizara imeanzisha darasa maalumu la wanafunzi hao Shule ya Msingi Jang’ombe.

Mjawiri pia anasema katika kuhakikisha wanatimiza malengo ya uboreshaji wa elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu, Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza) kinafanya utafiti ili kujua namna gani wanapaswa kufundishwa watoto hao ili kuona wanapata elimu iliyo bora kwa maslahi yao na taifa kwa ujumla.

Sambamba na hilo waziri huyo anasema kwamba kwa walimu wanaofundisha watoto hao katika mazingira magumu, wizara inaangalia namna ya kuwapatia motisha ili kuwajengea ari na bidii ya utekelezaji majukumu yao.

Aliitaka jamii kuungana na taasisi zinazoshughulikia kundi la watu wenye ulemavu kufanya kila linalowezekana ili wanafunzi wenye mahitaji maalum nao wapate elimu ya kutosha kama wanafunzi wengine.

Sheria ya watu wenye ulemavu Zanzibar ya mwaka 2006 inazungumzia nafasi ya watu wenye ulemavu kupewa haki sawa katika kupata elimu na mafunzo kwa mpango uliowekwa na kufaidika na utafiti kama ilivyo kwa raia wengine.

Pia sheria hiyo inataka mtoto au watoto wenye ulemavu kupatiwa huduma inayofaa kutoka kwa walimu wanaofaa katika kuwawezesha kujumuika kadri itakavyowezekana mambo ambayo ni dhahiri hayajafanyika kama inavyotakikana.

Columnist: mwananchi.co.tz