Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Unataka kazi ya mshahara mkubwa, omba hii

21926 Kazi+pic TanzaniaWeb

Fri, 12 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kama una ndoto ya kutengeneza fedha zaidi kupitia ajira, basi ushauri mkubwa unaoweza kupewa ni kwenda kusomea taaluma inayohusika na masuala ya fedha na bima, utafiti umebainisha.

Sekta hiyo imejitokeza kuwa miongoni mwa kazi inayolipa vizuri nchini na kwamba wale waliojikita kwenye eneo hilo wamekuwa wakiondoka na mishahara minono tofauti na hali ilivyo katika sekta nyingine.

Ripoti iliyotolewa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) baada ya kufanya utafiti uliohusisha ajira katika sekta rasmi na viwango vya mishahara Tanzania Bara, inaonyesha wastani wa mshahara kwa mfanyakazi aliyeko kwenye sekta ya fedha ni mkubwa.

Ripoti hiyo inaonyesha kiwango cha mshahara kwa mfanyakazi huyo kilipanda hadi kufikia Sh1.388 milioni mwaka 2016 kutoka kile cha awali cha mwaka mmoja nyuma (2015) kilichokuwa Sh1.198 milioni.

Baadhi ya wachunguzi wa mambo wanasema sekta hiyo imekuwa ikikabiliwa na uhaba wa wataalamu hali ambayo inawalazimu waajiri wengi kupandisha viwango vya mishahara kusudi kuwavutia wafanyakazi zaidi.

“Kwa mfano kuna chuo kimoja tu cha elimu ya juu ambacho kinatoa shahada katika masuala ya bima.....Waajiri mara zote wanashindana kuwasaka wahitimu wachache wanaopatikana na hii inasababisha wapandishe mishahara,” alisema ofisa mtendaji mkuu wa kampuni ya Bima ya Britam, Stephen Lokonyo.

Wataalamu wa rasilimali watu wanaamini kuwa kwa vile mishahara inazingatia namna sekta husika inavyozalisha na ujuzi wake, hivyo tofauti hiyo ya mishahara inaashiria kuwa sekta inayolipa vizuri ndiyo yenye waajiriwa wenye ujuzi zaidi na ambao hupata ujira mnono.

Ripoti hiyo ambayo ilitolewa wiki mbili zilizopita inaonyesha watumishi wa umma walioko kwenye nafasi za utawala, ulinzi na mifuko ya lazima ya hifadhi ya jamii ndiyo wanaofuatia kwa kulipwa vizuri zaidi nchini, huku mishahara yao ikipanda kutoka Sh997,058 katika mwaka 2015 hadi kufikia Sh1.293 milioni mwaka 2016.

Sekta ya nishati ya umeme, gesi na sekta ya usambazaji viyoyozi ndiyo inayoshika nafasi ya tatu katika mtiririko wa zinazolipa vizuri, wafanyakazi wake wakipokea kuanzia Sh933,227 mwaka 2015 hadi Sh1.021milioni kwa mwaka 2016.

Katika mtiririko huo, nafasi ya nne wako wale wanaofanya kazi za kitaaluma, wanasayansi na kazi za ufundi ambao wastani wa mishahara yao katika kipindi cha mwaka 2016 ilikuwa ni Sh987,634 .

Hata hivyo, katika ripoti yake NBS inasema kumekuwa na pengo kubwa la kipato kwa waajiriwa wanawake na wanaume walioko kwenye sekta zinazohusika na utawala wa utumishi wa umma na ulinzi.

Kama unataka kujiingiza kwenye kazi za kuhudumia malazi na huduma za chakula, basi jiandae kuwa mmoja wa wafanyakazi wanaolipwa kiasi cha chini, takwimu kwenye ripoti hiyo zinaonyesha.

Wafanyakazi kwenye sekta hiyo hulipwa wastani wa Sh200,881 kiwango ambacho hata hivyo kilipandishwa kutoka kile cha awali kilichotolewa mwaka 2015 Sh159,753.

Wafanyakazi katika sekta ya uzalishaji viwandani wanashika nafasi ya pili miongoni mwa wanaolipwa ujira mdogo zaidi, ikiwa wastani wa mishahara yao Sh271,976 mwaka 2016 ikiwa imeshuka kutoka Sh298,348 ilivyokuwa mwaka 2015.

Nafasi ya tatu kwenye kundi hili ni watu binafsi wanaofanya kazi za usaidizi zinazohusiana na mambo ya utawala na huduma nyingine ambao mishahara yao ni Sh305,480 mwaka 2016, kiwango ambacho kimeshuka kwa kiasi kikubwa kutoka Sh424,420 kilichokuwa mwaka 2015.

Columnist: mwananchi.co.tz