Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Unahitaji mkataba hata kama upo kwenye matazamio

13505 Justine+Kaleb TanzaniaWeb

Fri, 24 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kwa mujibu wa sheria, mkataba ni makubaliano kati ya pande mbili zenye nguvu ya kisheria. Kwa lugha nyingine, ni makubaliano ambayo pande zote mbili zinawajibika kisheria.

Mkataba ni moja ya mambo muhimu sana kati ya haki za mfanyakazi wakati mwingine kuliko hata kiasi cha fedha na marupurupu anayopaswa kulipwa.

Mkataba wa kazi hutoa mwelekeo wa ajira ya mfanyakazi, huonyesha usalama wa ajira, haki na wajibu wa mfanyakazi pamoja na haki na wajibu wa mwajiri, hueleza majukumu ya msingi ya mfanyakazi, muda na mahali pa kazi na masuala mengine muhimu kisheria.

Kukosekana kwa mkataba wa kazi huhatarisha usalama wa ajira yenyewe. Hivyo ni wajibu wa kila mwajiri na mwajiriwa kuhakikisha anapata mkataba wa ajira ikiwezekana hata kabla hajaanza kufanya kazi yenyewe na kulipwa mshahara wake wa kwanza.

Pamoja na uwapo wa kipindi cha matazamio hilo haliondoi umuhimu wa kuwapo kwa mkataba wa kazi. Baadhi ya waajiri wasio waaminifu hutumia kipindi cha matazamio kama kigezo cha kutompa mfanyakazi mkataba wa ajira bila kutambua kwamba inawezekana mtu akasaini mkataba unaoeleza kipindi cha matazamio kitakuwa cha muda gani japo kisheria hakipaswi kuzidi miezi sita.

Katika kipindi cha matazamio, mwajiri anayo haki ya kusitisha mkataba wa kazi endapo hataridhishwa na utendaji wa mfanyakazi au kwa sababu nyingine zozote zinazokubalika na ambazo ni halali kisheria.

Aina ya mkataba wa kazi huonyesha mustakabali wa ajira, humpa mfanyakazi na mwajiri fursa ya kufahamu haki na wajibu wa kila upande hivyo kujenga mazingira mazuri ya utekelezwaji wake kwa kulinda maslahi ya kila mmoja.

Mkataba wowote lazima uwe na vigezo vikuu vinavyojumuisha makubaliano ya pande mbili, malipo na lengo halali kisheria, uwezo wa kuingia mkataba na hiyari ya wahusika. Bila kujali ni aina ipi ya mkataba wa kazi mliosaini, kama kimojawapo kati vigezo hivyo kitakosekana, kinaufanya mkataba kuwa batili tangu mwanzo.

Kwa mujibu wa Sheria ya ajira na uhusiano kazini ya mwaka 2004; kuna aina tatu za mikataba ya ajira ambayo ni usiokuwa na muda maalum, wa muda maalum kwa wataalam na kada ya uongozi pamoja na mkataba wa kazi maalum.

Mkataba usiokuwa na muda maalum unasainiwa kati ya mwajiri na mwajiriwa ambao unaweza kuonyesha tarehe uliyosainiwa lakini hauonyeshi au hauelezi utaisha lini. Mikataba ya namna hii mara nyingi huwa katika taasisi za umma na baadhi ya taasisi binafsi.

Mkataba wa muda maalum kwa kada ya uongozi huhusisha zaidi kada ya uongozi au mwajiriwa mwenye fani ya aina fulani ambaye huajiriwa kushika wadhifa fulani wa juu katika utekelezaji wa majukumu yake.

Hata hivyo aina nyingine za waajiriwa wanaweza pia kuwa na mkataba wa muda maalum bila kujali kada anayotoka kulingana na mahitaji ya mwajiri.

Mkataba kwa kazi maalum unaweza kupewa kipindi maalum cha kuisha au mara nyingi kuisha kwake hutegemea kukamilika kwa kazi husika a.

Hii yaweza kuhusu utekelezaji wa mradi fulani au shughuli maalum ambayo kuisha kwake huashiria kufikia mwisho kwa mkataba wa ajira.

Jambo la muhimu na la kuzingatia ni kwamba Sheria inamtaka kila mwajiri na mwajiriwa kuhakikisha kabla ya kuanza kazi, ana mkataba wa maandishi uliosainiwa kati ya pande hizo mbili.

Baadhi ya waajiri huingia kwenye makubaliano mapya ya mkataba na mfanyakazi kila baada ya miezi kadhaa kukwepa baadhi ya gharama zikiwamo malipo watakayowajibika kumlipa mfanyakazi kwa mujibu wa sheria jambo ambalo halikubaliki kisheria. Usikubali kuanza kazi bila mkataba.

Columnist: mwananchi.co.tz