Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ukosefu wa vifaa unavyoongeza maumivu katika majanga ya moto

14432 Pic+vifaa TanzaniaWeb

Wed, 29 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Matukio ya moto ni miongoni mwa ajali ambazo zimeligharimu Taifa, jamii na familia kwa ujumla, mbali na upotevu na uharibifu wa mali, yapo matukio yaliyosababisha vifo, ulemavu na uharibifu wa mali.

Hivi karibuni imetokea ajali iliyohusisha magari matano ya mizigo ambayo yaliteketea kwa moto katika kituo cha forodha Rusumo wilayani Ngara mkoani Kagera mpakani mwa Tanzania na Rwanda.

Chanzo cha ajali hiyo ni gari la lililobeba mafuta ya petroli kupoteza mwelekeo na kuligonga gari jingine baada ya kuwa na matatizo katika mfumo wa breki.

Moto huo umesababisha kifo cha dereva mmoja huku mtu mwingine anayetajwa kuwa ni utingo wa gari ambalo lilikuwa chanzo cha ajali hiyo akiwa amepata majeraha makubwa.

Mkuu wa wilaya ya Ngara, Luteni Kanali Michael Mtenjele amekaririwa na vyombo vya habari akibainisha kuwa ukosefu wa kikosi cha zimamoto ni changamoto inayowakabili kutokana na matukio ya ajali ya moto kuongezeka na ombi lilishatumwa serikalini lakini utekelezaji wake haujafanyika.

Wakati wa ajali hiyo wananchi wameshuhudia video zinazoonyesha nchi jirani ya Rwanda ikijitolea kuzima moto kwa kutumia helikopta, pamoja na kwamba hazikufanikiwa kuuzima lakini ilipunguza kasi ya kuenea kwa moto huo kwani ungeweza kuenea na kusababisha madhara au maumivu makubwa zaidi kwa wananchi.

Hata hivyo kwa upande wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lilipatwa na changamoto ya kushiriki kuzima moto huo, hawakuwa na magari (mtambo) ya kuzima moto jirani na eneo hilo, badala yake magari ya kuzimia moto yalitokea Karagwe na kupitia kwenye barabara ya vumbi hadi kufika Ngara.

Kutoka Karagwe hadi kufika Ngara ni umbali wa zaidi ya kilomita 100, ni dhahiri kwamba hadi gari kufika Ngara moto hautasubiri, utakuwa umeteketeza sehemu kubwa ya eneo hilo.

Kibaya zaidi ni kwamba ubovu wa barabara ya eneo hilo unazidi kuifanya safari kuwa ndefu na hivyo kulifanya tatizo kushindwa kudhibitiwa mapema na hata kupunguza madhara.

Kabla ya tukio la ajali ya moto Ngara, ajali nyingine iliyohusisha meli ya kampuni ya Ocean Enterprises Limited ya Zanzibar iliungua moto wakati ikiwa imeegeshwa kwenye ufukwe wa Bahari ya Hindi huko Bagamoyo mkoani Pwani, wakati meli hiyo ikiwa imepaki ili kupakia mizigo mbalimbali.

Mkuu wa Jeshi la Zimamoto kituo cha Bagamoyo, Iward Mwanza alisema kuwa walipokea taarifa ya moto huo saa 12:24 asubuhi na askari walifika eneo la tukio hilo saa 12:30.

Alibainisha kuwa walianza kuudhibiti moto huo ili usilete hasara zaidi na hatimaye walifanikiwa, uchunguzi wa awali ulibaini kuwa chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme.

Jeshi la Zimamoto limejipangaje?

Kamishna wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye amesema jeshi hilo lina mkakati wa nchi nzima wa kupambana na ajali za moto ikiwamo kununua magari na vifaa vya uokoaji.

“Niseme ni kwa sababu ya ajali hizi mkakati si wa mkoa wa Ngara pekee bali ni nchi nzima kuhakikisha tunatoa elimu na kupunguza ajali hizo,” anasema.

Kuhusu kununua helikopta ya kuzima moto kama walivyofanya Rwanda, alisema hakuna mpango huo bali zaidi wamejikita kwenye magari na vifaa vingine vya zimamoto.

Pia Kamishna Andengenye anafafanua namna ya kupambana na ajali za moto kwenye shule za bweni na kusema, kunahitajika vifaa vya kutambua moto (smoke detector) ili kusaidia kuudhibiti moto kabla ya kuwa mkubwa.

“Tunatakiwa kutumia vifaa vya kubaini moto, hii itasaidia kuugundua moto mapema na kuudhibiti. Shida inayotukuta mara nyingi ni moto kuzuka na kushindwa kudhibitiwa,” anasema.

Anasema moto hutokea mara nyingi na hata kinamama majumbani huudhibiti lakini unapokuwa mkubwa ni vigumu kuuzima hata ukiwa na vifaa bora.

Kamishina Andengenye anasema hakuna sababu moja maalum inayochangia moto kwenye shule za bweni bali ni mchanganyiko wa sababu.

Kampuni binafsi kushiriki kuzima moto

Mkuu wa Kitengo cha moto cha Kampuni ya Ulinzi ya Ultimate Security, Donald Diwani anaeleza kuwa wanashiriki kwa namna mbili ikiwamo kuwa sehemu ya huduma kwa wateja wao, lakini pia hushirikishwa kwa kuitwa.

“Kwa wateja wetu tumewaunganisha kwenye mitambo ambayo ni maalum kama linatokea tatizo kwenye eneo lake akibonyeza kitufe tunatoa taarifa kupitia kwenye control room yetu nasi tunakwenda haraka,” anasema Diwani.

Anabainisha kuwa pia wamekuwa wakipigiwa simu na watu wengine kuombwa kutoa huduma hiyo ambapo hutoa na baada ya hapo wanaorodhesha gharama za malipo ambapo inatengemea na vifaa vilivyotumika.

“Mara nyingi unaweza kukuta gharama zimeanzia shilingi milioni mbili au zaidi lakini mtu huyo anapewa nafasi ya kujieleza kutokana na athari alizopata ikiwamo kutaja mali zake zilizoteketea,” anasema.

Diwani anasema kwamba wana magari ambayo wanaamini yanaweza kujitosheleza kuhudumia wateja wao kuzima moto kwa urefu hadi wa ghorofa 6. Kuhusu helkopta anasema kuwa bado hawajanunua.

Ajali za moto zilizowahi kutokea nchini

Baadhi ya matukio makubwa ya ajali za moto ambayo yamesababisha hasara na maumivu makali kwa taifa na jamii kwa ujumla ni pamoja na ule uliozuka katika Shule ya Sekondari ya Shauritanga Juni mwaka 1994 ambapo wanafunzi 42 walipoteza maisha kwa moto.

Aprili 2015, abiria 15 waliteketea kwa moto baada ya basi la Kampuni ya Nganga walilokuwa wakisafiria kugongana na lori (fuso) na kuwaka moto.

Ajali hiyo ilitokea eneo la Ruaha wilayani Kilosa mkoani Morogoro. Kutokana na abiria hao kuungua sana miili yao na hata sura kutotambulika, wote walizikwa katika kaburi moja kwenye makaburi ya Msamvu, Ruaha.

Agosti, 2009 wanafunzi 12 wa Shule ya Sekondari Idodi, iliyopo tarafa ya Idodi, Iringa, waliteketea kwa moto na wengine 22 walijeruhiwa baada ya moto kuzuka kwenye bweni walilokuwa wamelala.

Julai mwaka jana, Soko la Sido mkoani Mbeya liliungua moto na kuteketeza mali za wafanyabiashara wa soko hilo.

Machi mwaka huu, Soko la Mbagala Rangi Tatu jijini Dar es Salaam, maarufu kama Kampochea liliwaka moto ambao ulisababisha mabanda 673 yaliyokuwapo eneo hilo kuteketea kwa moto huo.

Columnist: mwananchi.co.tz