Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ukichelewa basi, ukachukua bodaboda utakutana na haya

64997 Boda+pic

Tue, 2 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Uchungu anaokutana nao abiria yeyote anayechelewa usafiri wa basi ni kuona fedha yake ikipotea, mipango yake kuvurugika na kuwaza namna ya kupata nauli nyingine ili afike aendako.

Hilo ni miongoni mwa mambo yanayochangia kumfanya mtu asikate tamaa, badala yake atafute namna nyingine ikiwamo kukodi pikipiki (bodaboda) ili kulikimbiza basi lililomuacha na hatimaye ndoto yake ya kusafiri itimie.

Hata hivyo, uamuzi huu mara nyingi humjia mtu bila ya kuwaza athari gani zinazoweza kumpata akiwa katika harakati za kuwahi basi kwa kulikimbiza kwa bodaboda.

Ukikutana na hali kama hiyo ya kuchelewa basi ukaamua kuchukua bodaboda kulikimbiza, utarajie mambo matatu yanayoweza kujitokeza au kukupata ambayo ni mwendo mkali wa madereva wa bodaboda jambo linaloweza kusababisha ajali na kumuathiri mwendeshaji na abiria.

Jambo la pili ni kuingia gharama kubwa ya safari tofauti na matarajio kwa kukodi bodaboda.

Suala la tatu linaloweza kujitokeza ni usumbufu kwa abiria waliomo kwenye basi hilo ambao unaweza kuwachelewesha hasa pale bodaboda anapolifikia na kulisimamisha.

Pia Soma

Baadhi ya wadau wa usafiri akiwamo Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Enea Mrutu anakiri kuwepo kwa matukio ya abiria kuchelewa mabasi na kulazimika kukodi bodaboda ili kuyakimbiza.

Anasema hali hiyo inatokana na uzembe kwa kutozingatia muda wa safari kama inavyoelekezwa kwenye tiketi “Huwa tunawaambia muda wa kufika kituoni ni saa 11:30 alfajiri, lakini baadhi hufanya tofauti. Kwa wanaopandia basi njiani hasa kituo cha Mbezi tunawaambia muda wa kufika kituoni hapo ni saa 12:15 asubuhi lakini wengine huja saa 12:30 muda ambao mabasi yanakuwa yameshapita.

“Hili jambo la kufukuza mabasi silipendi hata kidogo, kwa sababu linahatarisha maisha ya abiria. Muda mwingine huwa nawashauri abiria ni bora waahirishe safari kama haina ulazima na watoe taarifa kwa mabasi husika ili wasafri siku inayofuata,” anasema Mrutu.

Hata hivyo, Mrutu anasema baadhi ya kampuni za mabasi zimekuwa na utaratibu mzuri wa kuchukuliana abiria inatokea wameachwa.

Mwenyekiti wa Chama cha Kutetea Abiria Tanzania (Chakua), Hassan Mchanjama anasema baadhi ya bodaboda wa Ubungo wamekuwa mstari wa mbele kuvizia abiria wanaochelewa mabasi.

“Tunashauri mamlaka husika ziangalie suala hili, kukimbiza basi kwa bodaboda ni hatari kwa usalama na maisha ya abiria na wengineo,” anasema Mchanjama.

Mkuu wa operesheni wa kikosi cha usalama barabarani, Abdi Isango anakiri kuwepo kwa suala hilo huku akiwataja wanawake kuongoza kwa uchelewaji, kufukuza mabasi kwa bodaboda.

Kamanda Isango anawashauri wamiliki wa mabasi kuongeza muda wa abiria kuripoti vituoni badala ya saa 11:30 iwe saa 11:00 ili kufidia dakika 30 wanazochelewa wengi na kusema kufanya hivyo kutapunguza changamoto hiyo.

Waliokimbiza waelezea

Aboubakar Yusuf aliyekuwa akisafiri kwenda Songea, anasema alichelewa kufika kituo kikuu cha mabasi cha Ubungo hali iliyomlazimu kutumia Sh20,000 kwa ajili ya kukimbiza basi husika kwa kutumia bodaboda.

“Kutoka Ubungo hadi Mbezi nilitoa Sh5,000 kwa sababu dereva aliyenibeba tunafahamiana. Hata hivyo nilipofika Mbezi na kuingia stendi nilielezwa basi limeshaondoka. Ilinilazimu kuchukua bodaboda nyingine ili nilikimbize tena ingawa ni hatari.

“Kabla sijapanda usafiri, dereva wa bodaboda alinieleza kuwa kufukuza basi la mkoani si chini ya Sh10,000 na ikifika Kibaha inazidi kidogo hadi kufikia kati ya Sh15,000 au 20,000,” anasema

Baada ya maelezo hayo nilikubaliana naye, nikapanda na kuanza kulikimbiza basi husika, nikafanikiwa kulikuta stendi ya Maili Moja, Kibaha.

Abiria mwingine Joyce Mapunda (si jina lake halisi), anasema alipanga kupandia basi Mbezi Mwisho akienda Ruvuma, lakini kwa bahati mbaya alipofika saa 12 inakwenda na nusu basi hilo lilikuwa limeshapita.

“Nilichelewa dakika chache tu pale kituoni, lakini kutokana na umuhimu wa safari ilinibidi nichukue bodaboda kwa ajili ya kulikimbiza, ilinilazimu kulipia Sh20,000. Nililipa kiasi hicho cha fedha kwa sababu nilichukua pikipiki mbili moja ilibeba mabegi yangu na nyingine nilipanda.

“Ukichelewa basi utajikuta unaongeza gharama tofauti na matarajio. Mfano nauli ya Ruvuma ni Sh 46,000 na mimi nilitumia Sh20,000 utaona jinsi gani unavyopata hasara kwa sababu ya uzembe au bahati mbaya inayojitokeza na kukufanya uchelewe kufika kituoani,” anasema Mapunda.

Columnist: mwananchi.co.tz