Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ukaribu wenye maswali wa polisi na vyama vya kisiasa

68575 Pic+siasa

Sun, 28 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katiba ya Jamhuri ya Muungano ibara ya 147(3) inasema, “Itakuwa ni marufuku kwa mwanajeshi yeyote kujiunga na chama chochote cha siasa, isipokuwa tu kama atakuwa na haki ya kupiga kura iliyotajwa katika ibara ya 5 ya Katiba hii.”

Na kifungu cha nne cha ibara hiyo, kinaeleza maana ya “mwanajeshi” kuwa ni askari aliyeajiriwa kwa masharti ya muda au ya kudumu katika Jeshi la Ulinzi, Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza au Jeshi la Kujenga Taifa.

Pamoja na suala hilo kuzuiwa katika Katiba, siku za hivi karibuni kumekuwapo na matukio yanayoambana na kauli za viongozi yakiashiria matumizi ya baadhi ya wanajeshi kushiriki au kushirikishwa katika shughuli za kisiasa, huku CCM ikionekana kunufaika na utaratibu huo.

Hali hiyo inayozua mjadala inajidhihirisha kupitia kauli za baadhi ya viongozi wa Jeshi la Polisi, mfano ile ya kamanda wake wa Mkoa wa Arusha, Jonathan Shanna akiwa katika mkutano wa ndani wa CCM.

Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa AICC, Kamanda Shanna akieleza kuwa vyombo vya dola ni sawa na CCM.

“Kuna hesabu darasa la nne inasema kama A ni sawa na B na B ni sawa C, kwa hiyo A ni sawa na C. Maana yake A ni chama tawala na B ni Serikali halali na C ni vyombo vya dola ndiyo sisi. Sasa kama chama tawala, Serikali, vyombo vya dola, sasa wewe jiulize A kama is equal to C maana yake nini?”

Pia Soma

Kamanda Shanna pia anakumbukwa alipokuwa RPC wa Mwanza alionekana akiwafundisha wananchi jinsi ya kutoa salamu ya CCM “kidumu Chama cha Mapinduzi” wakati wa hafla ya kumbukizi ya miaka 19 ya kifo cha Baba wa Taifa, iliyofanyika Butiama mkoani Mara Oktoba 13, 2018.

Akiwa katika mashindano ya Mwalimu Nyerere Historical Marathon yaliyohusisha mbio za riadha, baiskeli na matembezi ya kilomita mbili yaliyofanyika Butiama, Kamanda Shana alisema salamu hiyo ni maalumu kwa sababu ni ya chama kilichoasisiwa na kuongozwa na Mwalimu Nyerere.

Kabla ya kutoa salamu hiyo, kamanda huyo aliyemwakilisha Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro katika hafla hiyo, aliwaeleza waliohudhuria kuwa ana salamu maalumu ambayo angependa kuwafundisha na kuwataka waitikie kama ishara ya kumuenzi Mwalimu.

Huku akipunga ngumi ya mkono wa kulia hewani na kuwahimiza wahudhuriaji nao kufanya hivyo, Kamanda Shanna alisikika akisema, “Leo naomba niwafundishe salamu mpya, nikisema kidumu Chama cha Mapinduzi mnatakiwa kuitikia kidumu milele.

Hata kauli ya hivi karibuni ya Rais John Magufuli wakati akizindua ujenzi wa nyumba za askari polisi mkoani Geita, nayo inajadiliwa, hasa hapa pale aliposema “majeshi ya ulinzi na usalama yanafanya kazi kwa masilahi mapana ya CCM.”

“Huu mpango wa kujenga nyumba kwa majeshi yote tutaendelea kuutimiza kwa sababu majeshi haya yanasimama kwa ajili ya kulinda masilahi mapana ya chama chetu cha mapinduzi,” alisema Rais Magufuli.

Akizungumzia kauli hizo, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga anasema hiyo ni hali inayosikitisha hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.

“Sisi tunasikitishwa sana na hizo kauli, kwa sababu madhumuni ya majeshi yoyote ni kulinda usalama wa raia kama ni polisi ni usalama wa raia, kama ni wanajeshi ni usalama wa nchi na kama ni magereza ni usalama wa wafungwa... tunapoelekea kwenye uchaguzi, inawezekana wananchi wasiende kuchagua kwa sababu ya kuogopa wanajeshi. Wengine wanaogopa hata kwenda kwenye mikutano, mtu akiona tu polisi anaweza asiende kwenye mkutano.”

Anasema LHRC imekuwa inafanya mikutano ya mashauriano na Jeshi la Polisi ambalo limeonekana kuchukua ushauri wao, “Ila kwenye utekelezaji inawezekana kukawa na changamoto. watu wake (IGP) wanaweza kumwangusha, ila tunamkumbusha kuheshimu haki za binadamu.”

Hata hivyo, Katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji anasema kwao kauli hizo siyo kitisho, badala yake wanaendelea na mikakati ya ushindi katika uchaguzi ujao.

“Hizo ni hulka za kisiasa tu zinazotolewa ili kututisha. Sisi tunajiandaa na programu zetu za uchaguzi. Kama ni kukamatwa na polisi ni kutokana na mifumo ya kijamaa, wanataka kututisha, lakini kwetu siyo vitu vigeni,” anasema Dk Mashinji. Mbali na kauli na matendo ya baadhi ya polisi, lawama zinatupwa kwa jeshi hilo kuwa limeonyesha upendeleo kwa kuvunja mikutano ya vyama vya upinzani na kukamata viongozi wake, huku viongozi wa CCM wakiendelea na mikutano yao bila bugudha.

Tukio la kuvunjwa kwa mkutano wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha) mkoani Shinyanga uliokuwa ukiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza hilo, Halima Mdee.

Mbali na Sinyanga Mdee ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Kawe jijini Dar es Salaam akiwa pamoja na katibu wa Bavicha, Grace Tendega ambaye pia ni mbunge, na mbunge wa viti maalumu, Anatropia Theonest waliamriwa kuripoti kituo kikuu cha polisi Bukoba mkoani Kagera na kuhojiwa baada ya kufanya mkutano wa ndani mjini humo.

Columnist: mwananchi.co.tz