Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ukaribu wa China, Afrika ni fursa ya kukuza uchumi baada ya uhuru

18275 Pic+china TanzaniaWeb

Thu, 20 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

China ilianza kushirikiana na Afrika katika vipindi vitatu tofauti. Cha kwanza kilianza baada ya kuundwa kwa Jamuhuri ya watu wa China mwaka 1949 mpaka wakati wa mageuzi ya kiuchumi mwaka 1978.

Katika kipindi hiki, China ilishiriki na kuelekeza nguvu zake kuzisaidia nchi za Afrika kupigania na kudai uhuru kutoka kwa wakoloni.

Kipindi cha pili kilikuwa kati ya mwaka 1978 hadi 2000 ambacho kulifanyika kongamano la kwanza la ushirikiano kati ya China na Afrika (Focac). Katika kipindi hiki, ushirikiano ulikuwa wa kiuchumi na zaidi.

Kipindi cha tatu kilianza mwaka 2000 mpaka sasa ambacho kinatilia mkazo zaidi kuanzisha ushirikiano wenye maslahi ya pamoja. Wakati huu, China haielekezi nguvu zake katika ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi tu, bali kwenye masuala ya kijamii na kitamaduni.

Katika vipindi hivyo tofauti, China imekuwa mshirika anayesaidia kupambana na umasikini na kujenga miundombinu imara ya kukuza uchumi. China imeelekeza nguvu zake kuyasaidia mataifa yanayoendelea huku Afrika ikipewa kipaumbele zaidi.

Wakati Afrika inapigana na wakoloni kudai uhuru, China ilikuwa nyuma yake, ilisaidia kutoa msaada wa kijeshi, kisiasa na kiuchumi. China ni mhanga wa ukandamizaji kama sisi, imekaliwa na majeshi ya kigeni katika mipaka yake, hivyo imepitia mateso na maumivu kama tuliyopitia.

Vilevile, China si mshirika wa G7 bali mataifa maskini na yanayoendelea hivyo ina kila sababu ya kundeeleza ushirikiano wake na Afrika. Pia, China inataka kuona Afrika yenye uchumi imara ndio maana inawekeza kwa nguvu kwa kutoa misaada ya fedha au ya kiufundi.

Mbali na hayo, bado China ina maslahi yake kihistoria na ya kimkakati na ikiwa rafiki ni lazima itegemee kunufaika kutoka kwetu kwa sera ya kuzinufaisha pande zote mbili.

Moja ya maslahi hayo ni kisiasa. China inahitaji kuungwa mkono hasa linapokuja suala la ushawishi katika sera zake za kimataifa, kama vile kuungana na Taiwan na migogoro wake katika Bahari ya Mashariki na Kusini mwa China.

Kuna masilahi ya kiuchumi, China inahitaji rasrimali za Afrika kwa ajili ya mahitaji yake muhimu. Limekuwa jambo la kawaida kusikia baadhi ya watu au mataifa yakipiga kelele kuhusu uwapo wa China barani Afrika.

Wengi wanasema inataka kuitawala Afrika na kuirudisha katika ukoloni, haya ni mawazo hasi na fikra finyu. Wakoloni walichukua kila kitu bure kutoka Afrika, hakukuwa na makubaliano lakini China haichukui bure, inanunua na inaingia mikataba na Serikali husika.

China inahitaji ushirikiano wa karibu sana na Afrika ili kuishirikisha katika masuala ya kimataifa. Ikumbukwe, China si mshirika wa mataifa tajiri duniani haa yaliyoendelea kiviwanda ingawa yenyewe ni tajiri kuliko mengi yaliyo katika umoja huo.

Ni mshirika wa mataifa maskini na yanayokua kiuchumi, ndio maana inahitaji ushirika wa karibu ili kuyasaidia kuimarika zaidi. Aidha, China inaihitaji Afrika kuuza bidhaa zake.

China na Afrika zinatakiwa kuwa washirika wa kweli, waanaoaminiana kukuza uchumi, utamaduni, siasa na ulinzi. Tofauti kati ya China na baadhi ya mataifa ya Ulaya na marekani ni kwamba, mataifa hayo yanaiona Afrika kama mzigo kiuchumi.

China inaiona na kuichukulia Afrika kama bara lenye fursa kubwa kutokana na utajiri mkubwa wa rasilimali zake. Hivyo, inaamini Afrika sio maskini ndio maana haina sera kandamizi za utegemezi.

Kupitia jukwaa la China na Afrika (Focac), China iliahidi kutoa Dola 60 bilioni za Marekani kuyawezesha mataifa ya Afrika kuwa na uchumi imara ili baadaye yasiwe tegemezi.

Ushirikiano wa hivi karibuni kati ya China na Afrika ni matokeo ya urafiki uliodumu tangu miaka ya 1980 kipindi ambacho Afrika ilikuwa imesahauliwa na nchi za magharibi.

Kuanzia mwaka 1991, China iliendeleza urafiki huu kwa mawaziri wake wa mambo ya nje kufanya ziara za kwanza kila mwaka barani Afrika. Ili kudumisha ushirikiano, China na Afrika zimekuwa zikifanya makongamano ya pamoja pia.

Malengo ya makongamano haya ni kuratibu na kuweka mipango ya kimkakati jinsi ya kuimarisha uhusiano. Kabla ya makongamano hayo, maofisa wa China huwa wanauliza na kuhitaji ushauri kutoka kwa viongozi wa Afrika juu ya kuendeleza ushirikiano wenye matunda zaidi.

Sababu nyingine inayoifanya China kuwa na uhusiano wa karibu na Afrika ni suala la Taiwan. Mpaka sasa, ni mataifa manne tu ambayo hayana uhusiano na China. Hivyo China inataka kupunguza pengo hilo kwa kupata ushawishi mkubwa litakapokuja suala la kuirudisha Taiwan ndani ya mipaka yake au kuizuia Taiwan kujitangazia uhuru wake yenyewe. Kuna sababu nyingi zinazoifanya China kuwa mshirika wa karibu na Afrika, kwanza, China ni taifa linalojitokeza kuwa na nguvu kiuchumi, kisiasa na kijeshi.

Kwa hiyo Afrika inahitaji mshirika mpya mwenye mawazo mapya na chanya, yenye mbinu mpya na isiyoingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine. Mshirika anayeheshimu mipaka ya nchi nyingine na rafiki wa kweli atakayekuwa naye bega kwa bega katika kukuza uchumi wa Afrika.

Aidha, Afrika inahitaji rafiki atakayelinda na kutetea masilahi na raslimali zake, atakayekuwa mshauri mzuri kisiasa na kiuchumi pia. Pili, Afrika inahitaji mshirika mbadala atakayeisaidia kuondokana na umasikini ulioitesa miaka mingi.

Tatu, Afrika inahitaji mshirika mpya kiuchumi asiye na ubaguzi wala upendeleo. Nne, Afrika inahitaji mshirika atakayeionyesha njia mpya kuyafikia maendeleo na mageuzi mapya ya kiuchumi.

Mshirika huyu si mwingine bali ni China, umuhimu wa China tunaweza kuuona kwa macho tu. Baadhi ya mataifa ya Afrika uchumi wao unakuwa kwa kati ya asilimia tano hadi sita kwa mwaka, nchi hizi ni zile ambazo China imewekeza sana.

Aidha, Afrika inahitaji kujifunza kutoka kwa China kama kweli inataka kuendelea kukua kiuchumi na kibiashara.

Siasa na uchumi

Afrika inaiangalia China kama ni nchi yenye nguvu kiuchumi na kisiasa na inahitaji kuwa nayo karibu ili isaidie kuleta maendeleo na kutimiza Malengo ya Milenium (MDGs).

Hii ni faida kubwa kwa Afrika kwa sababu, uwepo wa China na ushawishi wake kisiasa katika kukuza uchumi wa Afrika, unatoa msukumo kwa mataifa ya magharibi na Marekani kuongeza misaada na uwekezaji barani Afrika inayohitaji uhusiano mwingine mpya hasa China.

Mbali na uhusiano mzuri uliodumu kwa miaka mingi na mataifa ya magharibi, bado Afrika imeendela kuwekwa pembeni na kubaki nyuma kimaendeleo hivyo inahitaji kutafuta njia mbadala ili kuondoa vizingiti vinavyoifanya iendelee kuwa ombaomba na tegemezi kiuchumi.

Kutokana na ukuaji wa uchumi wa China na nia yake ya kuzisaidia nchi masikini, mataifa ya Afrika yanaiona fursa hiyo kuwa ni njia mbadala na sahihi ya kukuza uchumi wao.

Hii inatokana na nia ya kweli ya China kusaidia nchi za Afrika. Hivyo basi, ili Afrika ipate maendeleo ya kweli inahitaji zaidi biashara na uwekezaji kutoka China.

Ingawa mataifa ya Afrika hayawezi kuiga kila kitu kutoka China, lakini yanahitaji kujifunza na kujua siri za mafanikio yake.

Makubaliano ya China na Afrika (Beijing consensus) yanatoa nafasi ya kuchagua njia bora ya kuleta maendeleo ikiwa viongozi wa Afrika wataitumia fursa hiyo vizuri.

Faida ya China

Kuna faida nyingi zinazotokana na kuwa karibu na China...kwanza, mataifa yote yanajifunza kutoka kila upande na kutafuta njia bora na sahihi za maendeleo.

Kwa mfano, ushirikiano katika kilimo cha kisasa, viwanda na kuboresha miundombinu. Aidha, China inajishughulisha zaidi katika masuala ya amani na usalama katika mataifa mengi ya Afrika pamoja na ushirikiano wa kiusalama kati yake na Umoja wa Afrika.

Mbali na hayo, China na Afrika, zina mawasiliano ya mtu mmoja mmoja ambayo yanasaidia kujenga urafiki na uwekezaji. Katika ushirikiano huu, China na Afrika zimefika kiwango cha kubadilishana utamaduni na taaluma.

Hivyo, Afrika ina kila sababu ya kujivunia urafiki wake na China, mshirika wa karibu hata kabla ya uhuru na imeendelea kuwa karibu mpaka sasa. Hivyo basi, tuitumie nafasi iliyopo kuimalisha uhusiano utakaochochea kukuza uchumi.

Mwandishi ni mdau wa uchumi wa kimataifa. Anapatikana kwa namba 0754-699102

Columnist: mwananchi.co.tz