Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Uhalisia wa maisha na zama za maradhi yasiyoambukiza

9871 Pic+uhalisia TZWeb

Sun, 24 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ripoti za kitabibu zimebaini kuwapo kwa ongezeko la maradhi yasiyoambukiza nchini. Maradhi hayo yako katika makundi mbalimbali. Yapo ya akili, saratani, mapafu, pumu, moyo na mishipa ya damu, kisukari na mengine ya kurithi ikiwamo wa selimundu. Kwa kiasi kikubwa, maradhi haya husababishwa na mfumo wa maisha. Waandishi wetu, Herieth Makwetta na Lilian Timbuka walifanya mahojiano na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohammed Janabi.

Swali: Chanzo cha maradhi yasiyo ya kuambukiza ni nini hasa?

Jibu: Watu hawafanyi mazoezi. Ulaji wetu umekuwa mbaya, miaka ya karibuni wengi wanakula zaidi vyakula vya wanga na mafuta, unywaji pombe umekuwa wa kiwango cha juu, sigara pia inakuja kwa kasi ingawa haijafika juu sana. Hasa ukitazama uzito wa wagonjwa tunaowahudumia kila siku uko juu, hivi vyote vinachangia. Lakini kwa bahati mbaya tunatumia chumvi nyingi sana kwenye chakula. Chumvi ina tabia ya kukusanya maji mengi sana mwilini, ambayo hufanya presha inakwenda juu na ndiyo tatizo linaloongoza kwa maradhi ya moyo ambayo ni shinikizo la damu na lile la juu.

Swali: Hali halisi ya maradhi haya ikoje kwa sasa nchini?

Jibu: Kuna utafiti tuliufanya hapa Kisarawe (wilaya mkoani Pwani) na wenzangu kutoka Marekani, tulishangaa, kwa sababu katika kila watu 100, 28 walikuwa na shinikizo la damu. Kisarawe ni kijijini na tunategemea watu wake kwanza wawe na afya zaidi kuliko wa mjini, ila imekuwa tofauti kwa sababu ukikuta watu 28 kati ya 100 kijijini, wana shinikizo la damu bila kujijua, hii ni hatari. Siku ya moyo duniani mwaka jana, tulitoa huduma ya kupima bure. Katika watu 400 walifika, zaidi ya 300 bila kujijua walikutwa na tatizo moja au lingine la moyo, likiwamo la shinikizo la damu.

Swali: Wakati kukiwa na ongezeko hili, vipi kuhusu gharama za matibabu ya maradhi ya moyo?

Jibu: Bahati mbaya katika nchi zetu za Afrika, ukiacha maradhi yasiyoambukiza, maradhi ya kuambukiza pia yapo. Malaria, typhoid, ebola, sasa ukichanganya huo mchanganyiko, tunaweza kumaliza bajeti zetu zote za afya kutokana na gharama zake. Tatizo maradhi yasiyoambukiza siyo kama malaria ambayo dawa zake kidogo zina bei nafuu. Hapa ukikuta mshipa umeziba, gharama yake ni Sh6 milioni kuweka chuma au ukikuta tunaowabadilisha kwa kupandikiza mishipa, upasuaji wake ni Sh30 milioni, hivyo nchi zetu zinabidi zijitayarishe kwa sababu kama tusipochukua hatua za kujikinga, maradhi haya yasiyoambukiza yatakwangua bajeti kabisa.

Swali: Inakuwaje kwa wale ambao wanatumia dawa maisha yao yote? Hawa wanaweza kupata madhara gani?

Jibu: Hakuna dawa duniani ambayo haina madhara, iwe ni dawa za kupunguza maumivu, dawa ya presha au dawa ya moyo, binafsi ninapima vitu viwili, madhara ya dawa na faida, kama faida ni kubwa kuliko madhara tunamwandikia mgonjwa aendelee kutumia dawa hizo maisha yake yote. Lakini niwathibitishie, hakuna dawa ya moyo ambayo ina madhara kuliko faida, mfano pata shinikizo la damu liende zaidi ya 200 chini ya 100 au 220 chini ya 100, kinachofuatia ni kuanguka, kupata kiharusi, au utapooza upande mmoja, kwa hiyo kama una ndugu yako atalazimika kukaa na wewe siku zote za maisha yako zilizobaki. Hizi hadithi kwamba kuna madhara ni za upande mmoja, watu hawazungumzii upande mwingine kwamba, kama hutumii dawa unapobainika kuwa na tatizo basi, kifo cha mapema kinakuita. Sasa unapotazama kwamba dawa zina madhara itakupa labda kizunguzungu, labda kwa wanaume nguvu za kiume zitapungua, kinamama hamu ya kufanya tendo la ndoa itapungua, na ugonjwa wenyewe wa presha unasababisha vitu hivyo hivyo vitokee, macho yatakufa, hamu itapotea, moyo utapata shida, figo zitakufa. Ni rahisi kubadili matumizi ya aina za dawa kuliko kuacha kutumia.

Swali: Ni wajibu wa nani kumweleza mgonjwa faida na madhara ya dawa?

Jibu: Labda tatizo pia lipo kwetu wahudumu wa afya kutokaa na wagonjwa na kuwaeleza kwa kina kuhusu madhara na faida ya dawa. Lakini madhara ya dawa ni nadra sana na huenda kwa baadhi yasitokee. Lakini ukiwa na watu 100 wenye ugonjwa wa shinikizo la damu, si wote ambao watatumia dawa bila kupata tatizo la muda mfupi, hivyo ni wajibu wa sisi watoa huduma kuwaelimisha wagonjwa madhara na faida kubwa za dawa.

Swali: Vipi kuhusu idadi ya wagonjwa na uwiano wa madaktari au wataalamu?

Jibu: Hakuna uwiano. Tunapata wagonjwa wengi wenye matatizo ya moyo kutoka kila kona ya nchi kwa mfano Congo, Malawi, Kenya, Uganda, Comoro na sasa hivi karibu balozi zote zinakuja kutibiwa hapa JKCI, hata kile kipindi cha kikao cha mawaziri wa SADC kilichofanyika hapa Dar es Salaam, Waziri wa Afya wa Afrika Kusini alianguka, huduma ya kwanza aliipata hapa. Kwa hiyo tunahudumia watu wengi kutoka nje ya nchi, tunawaona wagonjwa 300 hadi 400 kwa siku na kwa sababu kliniki yetu ni ya kipekee, tunaanza kliniki saa 12 asubuhi hadi saa mbili usiku. Lakini tuna madaktari 12 tu waliobobea kwenye maradhi ya moyo na kuna vitengo vingi. Hivyo huwa inatubidi tujigawe hivyo hivyo, wa kwenda kufanya upasuaji wa wakubwa, wa watoto, ugawe watakaokwenda kupita wodini, upasuaji mdogo, kufanya chunguzi zingine kama eco na bado ugawe watu watakaobaki kliniki, ni kazi kubwa. Sisi kwa Afrika ukiangalia upasuaji tuko namba tatu, lakini bado tunahitaji madaktari zaidi na kuna madaktari 28 wanasoma hapa Tanzania na nje kwa sasa. Tunahitaji tuwapate zaidi ili tuweze hata kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na kutembelea mikoani.

Swali: Watoto wanaozaliwa na tatizo la moyo, lipo kwa ukubwa gani nchini hivi sasa?

Jibu: Tatizo hili ni kubwa. Mfano mwaka jana walizaliwa watoto milioni 2, lakini kati yao Laki nne walifariki kwa sababu mbalimbali, ikiwamo ya shida za wakati wa kujifungua na nyinginezo. Kwa hiyo unabakia na milioni 1.6 ambao asilimia moja watakuwa na ugonjwa wa moyo, ambao ni kati ya 13,000 hadi 15,000 na kati yao, asilimia 15 watahitaji upasuaji wakati fulani katika maisha yao, kwa wale watakaopata bahati, lakini wengine wataishia kutajiwa kuwa wanaugua maradhi mengine.

Swali: Licha ya kwamba JKCI inatoa matibabu Je? Kuna tafiti zozote zinazofanywa chini ya taasisi hii?

Jibu: Tunafanya sana machapisho, tayari tunayo 25 ya kidaktari na kwa sasa tuko kwenye jarida la wagonjwa wa moyo la Afrika ambalo sisi ni sehemu mojawapo kati ya wanaoliandaa. Tafiti tunafanya sana. Tatizo tafiti nyingi zimefanywa ulaya, hizi ni za wazungu. JKCI tunaona tukifanya tafiti zetu kwa Afrika, tunaweza kuwa na kitu tofauti. Tunafanya chunguzi nyingi ili tuweze kuwa na data zetu wenyewe.

Swali: Mwamko kwa watu kujitokeza kwa ajili ya matibabu ukoje kwa sasa?

Jibu: Watanzania wengi sasa hivi wanajitokeza sana kupima afya zao. Ufahamu kuhusu maradhi ya moyo sasa hivi imeongezeka, lakini la pili ni msaada wa vyombo vya habari, kwa sababu kila watu wanapopata taarifa kuhusu upasuaji unaofanywa na JKCI inawaongezea imani.

Mtakumbuka miaka michache iliyopita mtu alikuwa akimwambia mtu unakwenda kufanyiwa upasuaji Muhimbili, anaogopa. Kwa sasa mambo yamebadilika na huduma nyingi zinatolewa, tuko kwenye eneo la Muhimbili lakini humo ndani kuna taasisi nne kubwa na Taasisi ya Moyo ya JKCI ambayo ndiyo pekee kwa Tanzania. Taasisi zetu zinategemeana.

Swali: Wakati matibabu ya moyo yakigharimu fedha nyingi, mnawezaje kutoa huduma kwa wagonjwa wa msamaha?

Jibu: Changamoto kubwa kuliko zote ni hiyo, karibu asilimia 46 ya wanaokuja kutibiwa wanategemea msaada. Kwa hiyo tunalazimika kutumia fedha za wale wachache wanaolipa. Kinachonitia moyo ni kwamba, wananchi wengi wameanza kuamka kuhusu suala la bima, japokuwa bado idadi yao ipo chini kwa asilimia 35 ya Watanzania ndiyo wenye bima. Tiba zetu zina gharama kubwa. Kwa mfano, nikitaka kukuweka betri kwenye moyo, hiyo betri tu inauzwa Sh8 milioni, taasisi itazitoa wapi kama watu 10 tu ni Sh80 milioni? Tayari tumeshawawekea betri watu zaidi ya 105. Ninawashauri wananchi wabadili mtindo wa maisha, wafanye mazoezi na wale vyakula vile tu vinavyojenga siha njema ili kuepuka maradhi haya yasiyoambukiza. Wakifanya hivi, basi tutapunguza sana gharama za matibubu zitokanazo na maradhi haya.

Columnist: mwananchi.co.tz