Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Ufanye nini unapochoshwa na ugumu wa maisha?

43497 Pic+mahubiri Ufanye nini unapochoshwa na ugumu wa maisha?

Mon, 25 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Bwana Yesu asifiwe mwana wa Mungu. Napenda kuchukua wasaa huu kukusalimia mahali popote pale ulipo.

Kabla sijaanza kuhubiri neno la Mungu Jumapili ya leo, naomba nijitambulishe kwako.

Jina langu naitwa Mchungaji Omega Kipemba kutoka kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) ‘ The house of Hope’ lililopo Temeke, jijini Dar es Salaam. Sasa naomba uchukue Biblia yako na usome pamoja nami kitabu kile cha Isaya:57-15.

Biblia inaandika hivi, ‘Maana yeye aliye juu, aliye tukuka akaaye milele ambaye jina lake ni mtakatifu asema hivi, nakaa mimi mahali palipoinuka, palipo patakatifu tena pamoja nayeye aliye na roho iliyotubu na kunyenyekea ili kuzifufua roho za wanyenyekevu na mioyo yao walio tubu’.

Mpendwa msomaji wa Mwananchi tuombe kwa ajili ya neno hili la Mungu.

Maombi: Ee Mungu wetu mwenye nguvu, Yehova uketiye mahali pa juu palipoinuka sana, wewe ni Yehova na ulipojifunua kwa Musa ukasema ‘mimi niko ambaye niko’, ninaomba siku ya leo wewe ‘niko ambaye niko’ uliye fanya ishara ya ajabu na miujiza kwa wana wa Israel toka utumwani, kutana na msomaji wetu ili utimize neno lako. Napokea shukrani maana utafanya kwa jina la Yesu. Amen.

Kichwa cha habari cha neno letu leo kinasema ‘ufanye nini wakati unapoona maisha yako yanayumba? Au unapochoshwa na ugumu wa maisha?

Yaani unafanyaje unapokabiliana na mambo magumu na mazito yanayosababisha akili ishindwe kuwaza vizuri?

Unafanya nini wakati dunia inaposema huwezi? Wakati wanadamu wanaposema huwezi kupita? Unapogeuka kulia na kushoto, unakimbilia kwa jirani kuona msaada kote inashindikana! Unafanyaje?

Ninalo neno la kukufariji Jumapili ya leo. Ukisoma Zaburi 34.14 neno la Mungu linasema ‘Mateso ya mwenye haki ni Mengi lakini Mungu humponya nayo yote’.

Ukirejea neno la mwanzo kabisa tulilosoma kutoka kitabu cha Isaya, neno hili linaonyesha ni mahali gani Mungu anaweza kukaa.

Wakati sijaokoka nilifikiri Mungu anakaa kwenye jengo moja refu au katika nyumba za ibada lakini neno la Mungu linaonyesha kwamba hukaa ‘Mahali palipo inuka na patakatifu’.

Pia anakaa pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na kunyenyekea ili kufufua roho za wanyenyekevu na mioyo ya walio tubu.

Mungu hafurahii kuona mtu anapotelea kwenye dhambi, anatamani kuona watu wakitubu na kukumbuka kwamba yupo Mungu anayeweza kuwapona na shida zote, mateso na kila magumu wanayopitia. Biblia hii hii inaonyesha kuwa mtu mnyenyekevu na anayetubu, Mungu anakaa hapo ili kuleta ufufuo.

‘Ufufuo’ ni neno zito. Natamani nikuambie ushangilie kwa sababu kupitia neno hilo naona kuinuliwa kwako, na kupitia neno hilo unaweza kustawi upya.

Kumbuka Mungu hukaa kwa mtu mnyenyekevu na aliye tubu. Kama unapitia jambo gumu, maisha hayaendi yakupasa unyenyekee na utubu ili Mungu akae kwako astawishe mambo yako yaliyokuwa yameyumba.

Msomaji wa Mwananchi, zipo nyakati unaweza kukata tamaa kabisa ukaona kila unachofanya hakifanikiwi, usisahau kwamba Mungu hukaa katikati ya mtu aliye tubu na kunyenyekea ili kuleta ufufuo yaani kusababisha kitu kiishi tena.

Unapaswa kukubali kwamba unamuhitaji Yesu katika maisha yako ili ukae karibu kabisa na Mungu yaani inakupasa utubu dhambi na kuokoka.

Ukitengwa na Mungu unahitaji kuishi tena kwa sababu tayari unakuwa umekufa kiroho.

Lakini ukitubu na kunyenyekea Mungu atakaa katikati yako ili asababishe uhai tena.

Neno moja ninaloweza kukuambia leo, mwambie Mungu kile unachopitia ukitubu na kunyenyekea hakika atasikia na kukuponya na tabu zako zote kwa sababu hiyo ndiyo ahadi naye na yeye hulitizama neno lake ili aweze kulitimiza.

Biblia inasema aliyemfufua Yesu Kristo anakaa ndani yetu naye anaweza kufufua kile kilichokufa.

Yapo yanayosababisha ufufuo au uamsho kwa mtu.

Jambo la kwanza ni kutubu. Neno hili maana yake ni kubadilika kitabia. Luka 19;8 utaona mtu mmoja anaitwa Zakayo ambaye alisikia Yesu anakuja na anapita katikati ya Yeriko.

Zakayo aliamua kupanda juu ya mti ili amuone Yesu kwa sababu alikuwa mfupi. Yesu aliamwambia Zakayo shuka leo hii nitakuja nyumbani kwako watu wakashangaa.

Yesu alimuangalia Zakayo kwa sababu alionyesha kunyenyekea na kutubu. Ukiamua kutubu Mungu atakaa nawe na watu watashangaa namna mambo yako yatakavyooka. .

Namaliza kwa kusema kwamba, unapoona mambo magumu na hayaeleweki mruhusu Mungu akusaidie.

Usisahau kuwa unatakiwa kutubu na kunyenyekea mbele zake.



Columnist: mwananchi.co.tz