Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Uchaguzi uliompatia Nyerere madaraka ya kuongoza Serikali

99412 Pic+uchaguzi Uchaguzi uliompatia Nyerere madaraka ya kuongoza Serikali

Thu, 19 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Baraza la kwanza la Mawaziri la Tanganyika liliundwa na kuwa chini ya Gavana wa Kiingereza, Sir Richard Gordon Turnbull ambaye alikuwa mkuu wa nchi akisaidiwa na naibu wake, John Fletcher-Cooke.

Baraza hilo lilikuwa na Wazungu wanne na Mwasia mmoja. Wengine wote walikuwa Waafrika. Katika baraza hilo, kulikuwa na John Sydney Richard Cole (53) ambaye aliteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu mpya wa Serikali ya Tanganyika.

Alikuwa miongoni mwa wale Wazungu wanane walioingia kwenye Baraza la Kutunga Sheria baada ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 30, 1960.

Cole aliyekuwa mzaliwa wa Ireland alikuwa mmoja wa watumishi wawili wa Serikali ya Tanganyika chini ya Waingereza. Alisoma Chuo Kikuu cha Belfast, Ireland Kaskazini na Trinity cha Dublin, Jamhuri ya Ireland.

Baada ya kufanya kazi katika idara ya sheria kwenye nchi mbalimbali, aliingia Tanganyika mwaka 1956.

Nchi nyingine ambazo aliwahi kufanya kazi ni Mauritius, Nigeria na visiwa vya Bahama alikokuwa mwanasheria mkuu wa serikali.

Pia Soma

Advertisement
Kama ilivyokuwa kwa Tanganyika katika kipindi hicho, nchi zote hizo zilikuwa ni makoloni ya Uingereza.

Mzungu mwingine aliyeteuliwa katika baraza hilo ni M. J. Davies. Wakati wa uteuzi wake alikuwa na umri wa miaka 41. Aliingia Tanganyika mwaka 1940, alipata elimu yake katika Chuo Kikuu cha Oxford nchini Uingereza.

Alikuwa katibu wa magavana wawili wa Tanganyika kabla ya kuitwa London, Uingereza kuwa katibu wa makoloni.

Aliporejea Tanganyika baadaye, aliteuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Mikindani, Mtwara na baadaye Arusha.

Kati ya mwaka 1958 na 1959, alipelekwa New York, Marekani kuwa msaidizi wa mjumbe maalumu wa Tanganyika katika Umoja wa Mataifa.

Mwaka 1959 aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Utawala wa Tanganyika, lakini baada ya miezi miwili tu aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Usalama na Uhamiaji.

Historia inaeleza hiyo ilikuwa ni kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Huduma ya Habari katika serikali mpya ya Mwalimu Julius Nyerere.

Mzungu mwingine aliyekuwa katika baraza hilo, au halmashauri kama wenyewe walivyokuwa wakiita enzi hizo, alikuwa Sir Ernest Albert Vasey.

Aliingia Afrika Mashariki mara ya kwanza mwaka 1936 akiwa mfanyabiashara wa nchini Kenya. Miaka miwili baadaye, 1938, alichaguliwa kuwa diwani wa manispaa ya Nairobi.

Kwa vipindi viwili tofauti vya 1941-42 na 1944-46, alikuwa Meya wa Nairobi. Mwaka 1945 alichaguliwa kuingia kwenye Baraza la Kutunga Sheria la Kenya (Legco) na mwaka 1950 akateuliwa kuwa Waziri wa Elimu, Afya na Serikali za Mitaa.

Kati ya mwaka 1951-59, Sir Vasey alikuwa Waziri wa Fedha wa Kenya na mwaka uliofuata 1960, akateuliwa kuwa Waziri wa Fedha wa Tanganyika.

Kwa kuwa hakuwa na sifa za kutosha za kuishi Tanganyika na kumwezesha kuwa mjumbe wa Legco, Sir Vasey hakuwa mtumishi wa Serikali ya Tanganyika wala mjumbe wa kuchaguliwa katika Legco.

Aliteuliwa na Gavana Turnbull kwa maombi ya Mwalimu Nyerere kuingia katika Legco, kabla ya Nyerere kumteua kuwa Waziri wa Fedha katika Serikali mpya ya Tanganyika.

Mzungu mwingine katika baraza hilo alikuwa Derek Noel Maclean Bryceson. Yeye alikuwa mkulima, lakini aliteuliwa kuwa Waziri wa Afya na Masuala ya Wafanyakazi.

Kwa wakati huo alikuwa na miaka 37. Bryceson aliingia Tanganyika mara ya kwanza mwaka 1952 akitokea Kenya. Alipata elimu yake katika Chuo Kikuu cha Cambridge, Uingereza na alikuwa katika kikosi cha Jeshi la Anga la Uingereza wakati wa Vita Kuu ya II ya Dunia.

Mara ya kwanza aliingia serikalini mwaka 1957 kwa cheo cha waziri msaidizi wa kazi na starehe na baadaye Juni 1959, akawa Waziri wa Machimbo ya Madini na Biashara, na mwaka uliofuata, 1960, akaingia katika Serikali ya Mwalimu Nyerere.

Tofauti na wazungu wenzake waliokuwa katika serikali ya Nyerere, Bryceson alikuwa mjumbe wa kuchaguliwa wa Legco kutoka Dar es Salaam (Kaskazini).

Mhindi pekee aliyekuwa katika serikali ya kwanza ya Tanganyika na ambaye aliendelea kuwapo katika awamu mbalimbali za serikali ya Nyerere kwa miaka mingi baada ya Uhuru ni Amir Habib Jamal.

Jamal aliingia katika serikali hiyo a akiwa na umri wa miaka 38 akiwa Waziri wa Njia (mawasiliano), Simu na Majengo.

Alizaliwa Tanganyika na kupata elimu yake mkoani Mwanza na Dar es Salaam kabla ya kwenda Chuo Kikuu cha Calcutta, India, alikofuzu masomo ya uchumi mwaka 1958.

Kabla ya kuchaguliwa kuingia serikalini, Jamal alikuwa mfanyabiashara na Mkurugenzi wa Kampuni ya Habib & Company Ltd.

Juni 1959 alipoingia serikalini mara ya kwanza, aliteuliwa kuwa Waziri wa Tawala za Miji na Majengo katika serikali ya muda ya Tanganyika.

Uteuzi huo ulitokana na uchaguzi wa kura tatu mwaka 1958.

Waafrika katika serikali hiyo ya madaraka walikuwa ni Abdallah Said Fundikira ambaye kwa wakati huo alikuwa na umri wa miaka 38.

Fundikira aliteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Upimaji Ramani na Maji. Alisomea kilimo na kupata stashahada ya kilimo mwaka 1944 katika Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda.

Alihudhuria pia masomo ya muda mfupi ya kilimo katika Chuo Kikuu cha Cambridge, Uingereza mwaka 1953.

Kabla ya kukabidhiwa kiti cha utemi wa Unyanyembe Tabora, mwaka 1957, Fundikira alikuwa ofisa kilimo katika Wilaya ya Newala, Jimbo la Kusini.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1958, alichaguliwa bila kupingwa kuwa mjumbe wa Legco kutoka Jimbo la Magharibi (Tabora) na baada ya hapo, aliteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi na Upimaji Ramani katika serikali ya muda Julai 1959.

Mwafrika mwingine aliyeingia katika halmashauri hiyo ya mawaziri ni Clement George Kahama (32) kutoka Karagwe, Jimbo la Ziwa Magharibi, ambaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Usalama na amani ya nchi.

Kahama alipata elimu yake katika Sekondari ya Tabora na kisha Chuo cha Loughborough cha Uingereza kati ya mwaka 1952 na 1954. Alikuwa Mtunza Hazina wa chama cha wakulima cha Bukoba (BCU) na kiongozi mkuu wa kwanza wa ushirika huo mwaka 1956.

Alijishughulisha na halmashauri ya Mji wa Bukoba na halmashauri ya Buhaya na alichaguliwa kuingia katika Legco kutoka Jimbo la Ziwa Magharibi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1958.

Katika serikali ya muda aliteuliwa kuwa Waziri wa Starehe na Maendeleo, uteuzi huo ulifanyika Julai 1959.

Na katika serikali mpya ya Nyerere, aliteuliwa kuwa Waziri wa mambo ya ndani ya nchi.

Mwafrika mwingine katika halmashauri hiyo alikuwa ni Paul Bomani, aliteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo na maendeleo ya Ushirika.

Bomani, mzaliwa wa Ikizu wilayani Musoma, aliingia katika serikali ya Nyerere akiwa na umri wa miaka 35.

Kama alivyokuwa Kahama, Bomani naye alijishughulisha sana na masuala ya ushirika katika Kanda ya Ziwa na alikuwa kiongozi wa chama cha Ushirika cha Victoria Federation of Co-operative Unions (VFCU).

Bomani alipata elimu ya ushirika Chuo cha Loughborough, Uingereza na alipata safari nyingi za Ulaya kujifunza uendeshaji shughuli za ushirika. Mwaka 1958 alipita bila kupingwa kuwa mjumbe wa Legco.

Mwafrika mwingine katika halmashauri hiyo alikuwa Asanterabi Zephania Nsilo Swai. Yeye aliteuliwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara katika serikali hiyo. Kama walivyokuwa baadhi ya wengine, yeye naye alikuwa na umri wa miaka 35 wakati wa kuteuliwa kwake.

Swai alipata elimu yake katika vyuo vikuu vya Makerere, Uganda, Bombay, India na Pittsburg, Marekani, ambako alipata stashahada na Chuo Kikuu cha Delhi, India, ambako alipata shahada ya uchumi. Mbali na wadhifa huo wa uwaziri, Swai alikuwa mwenyekiti wa halmashauri ya uchumi na starehe ya chama cha Tanganyika African National Union (Tanu).

Mwingine katika halmashauri ya mawaziri hao alikuwa ni Oscar Salathiel Kambona. Yeye aliteuliwa kuwa Waziri wa Elimu akiwa na umri wa miaka 32. Kambona ambaye sasa ni marehemu, alikuwa mtoto wa kasisi na alipata elimu yake katika shule za Alliance zilizokuwa Dodoma na Tabora.

Rashidi Mfaume Kawawa aliteuliwa kuwa Waziri wa Serikali za Mitaa na Nyumba. Kadiri siku zilivyokwenda ndivyo Kawawa alipopanda cheo hadi kufikia wadhifa wa Makamu wa Pili wa Rais.

Baraza hili la mawaziri liliapishwa Septemba 4, 1960, ikiwa ni siku moja baada ya Nyerere kuapishwa na kuwa Waziri Mkuu wakati huo Gavana Turnbull akiwa bado mkuu wa nchi. Huu ulikuwa ni uchaguzi wa mwisho wa mfumo wa vyama vingi katika Tanganyika.

Columnist: mwananchi.co.tz