DUNIA inaenda kwa kasi sana. Katika zama hizi, kila kitu kimebadilika. Kuanzia maisha ya kawaida mpaka yale ya soka. Soka la kisasa limelainishwa na kurahisishwa mno tofauti na lile la kina Pele. Leo makipa wanalindwa dhidi ya hila za washambuliaji watukutu. Washambuliaji wanalindwa dhidi ya mabeki wenye roho mbaya.
Mabeki wakorofi ambao kuna wakati waliweka utu kando na kuvaa uhayawani, kiasi cha kudiriki kuwarukia wenzao miguu ya shingo. Hawa kina Pascal Wawa, Aggrey Morris ama Kelvin Yondani wanaodaiwa wana matukio ya kitemi, ni sehemu ndogo sana ya mabeki wa kipindi cha nyuma. Salum Kabunda ‘Ninja’ hakupewa jina kishabiki tu. Alikuwa Ninja kweli.
Pia, ieleweke sio kama wachezaji wenye roho mbaya katika soka kwa sasa hawapo, la! Wapo tele, ila sheria zinawabana. Wachezaji wakorofi walianza zamani, lakini zilitengenezwa sheria kuwabana, ndio maana leo, Sergio Ramos na ubabe wake kuna wakati analainika.
Kuna marekebisho makubwa ya sheria juu ya faulo na mengineyo katika mchezo huo. Mabadiliko yaliyogusa hadi kwenye soko la nyota wa mchezaji huo. Soko la wachezaji nalo limerahisishwa na kupanuliwa mno. Leo wachezaji wanauzwa na kununuliwa kama bidhaa nyingine sokoni, kutegemeana na ubora wake. Wachezaji nao wameijua thamani yao na kuvitumia vyema vipaji vyao kupiga fedha. Japo mkoloni aliwalemaza wengi kwa kuwaaminisha mtu kuwa na elimu nzuri ndio kujitengenezea maisha, lakini ukweli haupo hivyo. Asilimia kubwa ya wanamichezo wanaishi kitajiri kuliko hata waliobukua vitabu vya kutoka katika elimu
Ukoloni uliwatia ujinga wengi. Walitengeneza mfumo wa kuwaaminisha watawaliwa kuwa ukisoma utaajiriwa na wengi wamelemaa hivyo. Hata hapa nchini bado elimu haijawa msaada mkubwa kwa wasomi. Haiwajengi wasomi kujiajiri kwa vile mitaala ya kikoloni imebaki kama ilivyo, yaani soma uajiriwe. Lakini, kwenye soka hali ni tofauti. Mambo yamebadilika.
Kadri unavyokuwa na kipaji kikubwa ndivyo unavyoweza kuvuna mamilioni ya fedha na kuuzwa ama kununuliwa kokote na yeyote! Wanaoishi kwenye nchi zilizoendelea na hata katika bara la Afrika, wanajua soka kwa sasa ni ajira na biashara. Biashara inayolipa, ndio maana matajiri wameamua kuwekeza kwenye biashara hiyo na wamekuwa wakivuna faida ya kutosha.
Pia Soma
- Samatta do or die Aston Villa
- Azam iliwapoteza Yanga hapa tu
- Pochettino ampa masharti Woodward kutua Man United
Wengi wao bado somo halijawaingia. Ndio maana unaweza kushangazwa na mambo wanayofanya baadhi ya nyota. Nyota ambao kwa kuviangalia vipaji vyao na bahati wanazozipata, unaweza kuwabashiria watafika mbali katika muda mfupi, lakini wapi!
Achana na Mbwana Samatta au Simon Msuva na wengineo ambao, kwa kupata kwao nafasi ya kutoka nje ya nchi, wameitumia vyema na kuzifungua akili zao. Kuonja kwao utamu wa kucheza nje ya nchi kumewafanya wasitamani kurudi nyuma. Hawafikirii kurudi Tanzania. Hakuna ubishi hata kina Samatta na Msuva, tunajua kuna siku watarudi nyumbani. Lakini ni kipindi watakuwa wamemaliza kile walichokifuata huko. Kwani Danny Mrwanda, Henry Joseph ama Abdi Kassim ‘Babi’ ilikuwaje? Si walizurura nje, lakini walipoona sasa imetosha na hawana maajabu waliamua kurejea nyumbani, kitu ambacho hata kina Samatta itafikia muda huo, ila, ni kitu kinachoshangaza mchezaji wa Kitanzania anapata fursa ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, anapambana kurudi nyumbani. Wachezaji wa hivyo ni wale wasiojua thamani ya miguu yao. Hawajui kama miguu na vipaji walivyonavyo ni dhahabu kama si almasi wanaotembea nazo, zinazoweza kuwatajirisha na kuwatoa kwenye lindi la umaskini!
Wakati Haruna Moshi ‘Boban’ alipoamua kurejea nchini akiachana na dili lake la Gefle IF, hatukumuelewa, hata alipotoa utetezi wake. Mrisho Ngassa, leo anasimangwa kila anapolalamikia hali anayokutana nayo Jangwani, kwa vile mwenyewe alikataa ofa ya kwenda El Merreikh ya Sudan. Alikubali kulipiga teke fuko la fedha kwa mapenzi ya Yanga. Leo Ibrahim Ajibu ananangwa kwa kuikacha ofa ya kwenda TP Mazembe ili arejee Msimbazi. Pengine sasa Shiza Kichuya akasimangwa zaidi, kwa kitendo chake cha kuamua kurejea Simba, baada ya kupata fursa ya kucheza Misri.
Mashabiki wa Msimbazi wanashangilia. Wanasema Mtoto karudi nyumbani, kiboko ya Yanga amerudi nyumbani. Wanakumbuka yale mabao matatu katika mechi tatu mfululizo za watani. Wanataka kuziona tena zile kona bao zake. Kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ huenda bado analikumbuka alivyotunguliwa katika pambano la watani la Oktoba Mosi, 2016. Ila kafanya haraka mno kurudi nyumbani. Sina hakika kama Simba ilikuwa inamhitaji zaidi Kichuya. Kikosini kuna wachezaji wa aina yake kibao. Kuna Francis Kahata, Deo Kanda, Luis Miquissone, Miraji Athuman, Juma Rashid na hata Hassan Dilunga. Simba ilikuwa inahitaji straika wa kuziba nafasi ya Wilker Da Siliva na sio Kichuya. Ila inawezekana kabisa Kichuya alikuwa akiihitaji zaidi Simba. Labda kule Misri alikosajiliwa katikati ya msimu uliopita hakupapatikiwa. Pengine Wamisri hawakuona maajabu yake tangu aende huko. Hawakuijua thamani ya miguu yake na pengine walimchukulia poa. Hapo ndipo alitakiwa kujiongeza na kutafuta mahali pengine ambako angepewa heshima. Lakini, hakutaka kujisumbua na hata mshauri wake hakutaka kujisumbua. Ndio maana akamshauri arudi nyumbani. Maisha ya ugenini labda yalimkifu Kichuya kama yalivyowahi kumkifu Boban. Nasema labda kwani sina hakika nalo, lakini bado najiuliza kitu gani kilichomkumba Kichuya hata akaamua kurudi tena Tanzania? Bado sijajua kitu kilichomrudisha nyuma. Samatta alipotimka kwenda TP Mazembe, hakurudi hadi misimu mitano ilipokatika, kisha akapaa zake hadi Ulaya. Bado yupo huko na sasa anajiandaa kutoka Ubelgiji ili atue England. Hii ndio akili ya wanasoka wa kisasa. Wanawaza kusonga mbele na sio kurudi nyuma. Msuva baada ya masimango na matusi mengi kutoka kwa mashabiki wa Yanga, alitimka zake Morocco. Difaa el Jadida ilimpa mwangaza, leo anatajwa kusajiliwa Benfica ya Ureno. Moja ya klabu kubwa Ulaya, sidhani kama anatamani kurudi Yanga kwa sasa hata kama mashabiki wake wameendelea kumlilia na kumuimba kwa sababu ya pengo alililowaachia klabuni kwao. Akili zake kwa sasa zimekuwa na zimekaa kisasa zaidi.
Simsimangi, Kichuya, kwani kupanga ni kuchagua. Simlaumu kwa vile kila mtu anaishi kwa jinsi ya mipango yake. Ukweli Ndivyo Ulivyo! Hata Boban leo hata mkimsema vipi kwa alichokifanya miaka kadhaa iliyopita na sasa kutangatanga katika klabu kadhaa za ndani, hawezi kuwaelewa. Alishajipangia akimbie Ulaya ili aje kuzichezea Mbeya City. Alitamani kuichezea Friends Rangers, alitaka akipige African Lyon na sasa ametua Singida United. Klabu iliyokimbiwa na nyota wa kimataifa kutoka nchi za Rwanda, Zimbabwe, Ghana na hata Ufaransa kwa ukata, yeye ndio kaipenda! Lakini Kichuya atakuja kuwaambia nini watu, mambo yakienda kombo Msimbazi! Sitaki kuamini nyota huyo amekosa washauri wazuri wa kumpa muongozo wa kuhakikisha hachezei kipaji alichonacho! Simba sio klabu ndogo, lakini mchongo alioupata Misri, ulipaswa umpe njia ya kusonga mbele. Leo Sekilojo Chambua tunamuelewa sana kwa kushindwa kwake kucheza soka nje ya nchi kwa sababu ya kauzibe alizokutana nazo kuanzia klabu yake ya Yanga hadi FAT, ila hawa kina Kichuya na wenzake watakuwa na visingizio gani? Hawawaoni wenzao kina Haruna Niyonzima, Jean Baptiste Mugiraneza, Besala Bokungu na hata Seleman Ndikumana kama sio Pascal Wawa wamekataa kurudi makwao na kukomalia Tanzania? Kwanini wanashindwa kuwa wavumilivu? Enewei, nimtakie tu, kila la heri kijana huyu wa Morogoro katika maisha yake mengine mapya Msimbazi, ila ajue wazi amewaangusha wengi walioamini alishaukata...! Wale waliokuwa wakipiga kelele vijana wa Kitanzania watoke nje ya nchi kucheza soka la kulipwa kwa manufaa ya Taifa. Amewaangusha waliamini Misri ilikuwa njia ya kwenda Ulaya...!
Kama sio shinikizo lake kutaka kurudi nyumbani, basi aliyemshauri na kumlazimisha kufanya hivyo ajue ataubeba mzigo wa lawama siku atakapokuwa akilalamikia kama Ngassa na Yanga yake!